Zingatio: Bado Hujafikia Kuwa Na Kibri

Zingatio: Bado Hujafikia Kuwa na Kibri

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

 وَلَهُ الْكِبْرِيَاءُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴿٣٧﴾

37. Na Ukubwa, Uadhama, Ujalali ni Wake Pekee mbinguni na ardhini; Naye Ndiye Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote.  [Al-Jaathiyah:37]

 

Ya Allaah wewe ni Muweza na ni muhali Kwako kukosekana. Tambua ewe kiumbe dhaifu mwanaadamu kwamba ipo siku ulikuwa hupo duniani na kama leo upo, tambua kuwa ipo siku utakosekana. Yeye ni Mtangu, Hana mwanzo wa kuwepo Kwake. Unaweza kunibishia huijui siku yako ya kuzaliwa? Na kama huijui una upungufu. Allaah Atabakia milele, Qiyaamah chako kipo tu, na mimi au wewe atamtanguliza mwenziwe kaburini.

 

Utukufu ni Wake pekee! Leo Muislamu unatengeneza na kukivumbua kitu na kinakugeuka wewe mwenyewe. Tumuhudia tukibuni vyombo vya kupima upepo, hali ya hewa na juu ya yote bado havitoshelezi kutupasha habari kwa wakati. Lakini Allaah! Ndiye Mkuu wa yote, kwani Allaah Hakhalifiani na vyenye kuzuka katika Alivyoviumba. Sisi binaadamu tunahitaji kuneemeshwa, katu hatuwezi kusimama kwa dhati yetu. Hatujitoshelezi kwa chochote na ndio maana kuna mzunguko wa mmoja kuhitaji kwa mwengine. Kama ni mfanya biashara wa nguo utahitaji kutoka kwa mkulima na kadhalika. Allaah Pekee Anasimama kwa dhati Yake.

 

Binaadamu ni sisi, tumejaa kila aina ya upungufu. Mbora wetu ni yule aliyetenda ovu akarudi kwa Muumba Ambaye hatuwezi kuichukua kibri Yake hata kidogo. Na wala tusithubutu kwani tutashindwa tu. Yeye Allaah Ametakasika kwa kila upungufu na Aliyetukuka ni mmoja tu katika dhati Yake, sifa Zake na vitendo Vyake. Hana mshirika. Asimame afiriti yeyote kuigeuza Qur-aan atakavyo, abadan hatoweza. Lakini Allaah ni muweza wa kila kitu.

 

Naye ndiye Anayeulinda huu Ulimwengu kwa viumbe vilivyo dhahiri na visivyoonekana pia! Wala Hahitaji kulazimishwa kwa chochote. Akisemacho Yeye ni kun fayakuun (Kuwa basi kitakuwa). Je, sisi binaadamu tunayo amri kama hiyo? Binaadamu tumejaa ujinga wa kutojuwa mambo na ndio maana tunajazana darasani kusoma elimu ambayo ni fardhi kuisoma. Lakini Allaah Hahitaji kufundishwa, ujinga upo mbali na Yeye Mtukufu pekee.

 

Ee binaadamu, liangalie jina lako vizuri. Una asili ya Adam na ndio maana ukaitwa mtoto wa Aadam. Na yuko wapi baba yako asili Aadam? Utakufa tu. Ipo siku utakuwa maiti ukitaka usitake. Wewe, mimi, yule sote tutakuwa maiti. Lakini Allaah pekee Yupo mbali kabisa na siku Atakayogeuka maiti.

 

Wapo wenzetu maelfu kwa maelfu ni viziwi. Allaah Awape subira ya kweli. Wapo wengine wanaambiwa wazito wa kusikia. Tupo mimi na wewe ambao tunaamini tunasikia, lakini mbona tunaenda kwenye maovu? Kwa sababu hatusikii. Kama hivyo haitoshi, tutaambiwa lakini bado hutokea kuuliza "Ulisema nini?’ ‘Sijakusikia, hemu rudia tena.’ Allaah abadan Hana sifa ya uziwi kamili wala nusu uziwi wala chembe ya kasoro ya kusikia. Anajua namna Anavyosikia kwani kila kiumbe kinachosema kwa sauti kubwa au ya chini wote Anawasikia.

 

Tena Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)...

 

Anaona kila kitu,

hakuna kimpitacho kitu.

Ni sisi binaadamu vinatupita tele vitu,

hatuoni chao wala chetu.

Tukitaka tusitake hizo kasoro tu,

Rabb Hatumpati chembe katu.

 

Ipo siku kilikushika kigugumizi ukawa sawa sawa na bubu. Lakini sifa hiyo hana Allaah Muweza wa kusema kwa namna Aijuayo mwenyewe. Wala Hashindwi kwa chochote. Tukusanyike binaadamu sote tuseme tunataka kufanya mapinduzi ya Kumpindua (wa nauudhu biLlaahi min dhaalik) hatufanikiwi hata kidogo. Ni nani mwenye mapenzi ya mtoto zaidi ya mama mzazi? Basi tambua kwamba hayo mapenzi ya mama kwa mtoto ni madogo kuliko yale Aliyokuwa nayo Allaah kwa viumbe Vyake.

 

Allaah Anajua yanayopita ndani ya nafsi, hata yaliyofichikana ndani ya hiyo nafsi. Anaelewa hata ucheza wa macho (eye blink). Binaadamu hana sifa hiyo ya kutambua uhakika wa hata kinachopita ndani ya nafsi yake akiwa macho au akiwa amelala. Uhai ndio msingi wa maisha, na kinyume chake ni mauti. Basi Yeye Muumba ndiye Atakayebaki hai maisha ya kudumu. Hana mwanzo wala Hana mwisho. Daima Atabaki ni mwenye kusikia, kuona na kusema kwa namna Anavyojuwa Yeye Mwenyewe Khaaliqu kulli shay-in (Muumba wa kila kitu) Tutaendelea kusikia au kuona kile kilicho mbele yetu lakini hatuwezi kuona kilicho hata nyuma ya pazia. Tunaona kimoja wala hatuna uwezo wa kuona viwili kwa wakati mmoja.

 

Daima Allaah Utabaki Kuwa Mkubwa Juu Ya Wakubwa

Allaahu Akbar Ukisema “Kun” (Kuwa)

Basi Hapo Hapo Huwa

 

Share