Nakaribia Kuzini na Mke wa Ndugu Yangu Vipi Nijiokoe?

 

SWALI:

Assalaam aleykum. Mimi nikijana,ila nina tatizo kubwa ambalo linalo nifanya huwa nakosa raha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wangu.mimi naishi na kaka yangu.ambaye ananisaidia kwa sasa, kutoka na nina matatizo katika hiyo nchi tunayo ishi.ila ndugu yangu yeye ameowa,na anawatoto. Ila kuna jambo ambalo limekuwa,limenifanya kuwa karibu sana na mkewe kutokana huwa na msaidia sana kazi zake.mpaka ikawa ananieleza matatizo yake na ndugu yangu.na kwa mujibu ya maelezo yake,ndugu yangu alikuwa anamakosa,ya kuwa ya kumuuzi mkewe. kama kwenda nje ya ndoa,ilifikia mpaka mkewe alitaka kuachika.ila nilijitahidi kuongea na shemeji yangu alinisikiliza na kuacha hizo fikira mbaya.ila baadae mambo ya kabadilika tukajikuta mimi na shemeji yangu, tumeingia kwenye mtihani wa kupendana.na kufikia mpaka tukaanza  kupigana mabusu,ila hatujawahi kuzini hata siku moja kwa kumuogopa Mola wetu.kwani mimi na shemeji yangu tunaswali.je unaweza kutusaidiaje kuliacha hili tatizo?na tofauti gani ya kukurubia zinaa na kuzini?

 

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani ndugu yetu kwa swali lako zuri kuhusu mas-ala nyeti kama hiyo. Pia shukrani zetu kwako ni kuwa umeliona lipo tatizo na hivyo kutaka usaidizi wa kuweza kutatua tatizo hilo kabla hujapitiwa na wakati na kuingia katika madhambi ambayo huenda ikawa vigumu kujitoa kwayo.

 

Ujana ni wakati ambapo damu inakuwa moto na matamanio yanampelekea mja kujaribu mambo mengi pamoja na kuingia katika mambo ya maasi. Lakini inatakiwa kwetu sisi tuchukue vielelezo vya vijana walioelezwa na Allaah Aliyetukuka waliokataa kuingia katika madhambi aina yoyote. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatueleza kuhusu vijana wa pangoni:

 

Hakika wao walikuwa ni vijana waliomuamini Mola wao Mlezi. Nasi Tukawazidishia uongofu. Na Tukazitia nguvu nyoyo zao pale waliposimama mbele ya mfalme wakasema: Mola wetu Mlezi ni Mola wa mbingu na ardhi. Hatutamuabudu mungu mwingine badala Yake” ( – 14).

 

Utaona hapa vijana walisimama imara na kwa sababu hiyo Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Akawaongezea uongofu. Hilo halikutosha, hivyo wakaona ni afadhali waondoke katika sehemu yenye maasiya pamoja na kuomba usaidizi wa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) katika hilo. Anatuelezea Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) hilo pale Aliposema:

 

Mola wetu Mlezi! Tupe rehema zinazotoka kwako na Tutengezee uongofu katika kila jambo letu” ().

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatueleza kuhusu Nabii Yuusuf (‘Alayhis Salaam) na mitihani aliyopata kutoka kwa mke wa waziri alipokuwa kijana barobaro. Ikafika hadi ya kwamba mwanamke huyo anamtaka kwa nguvu lakini akakataa katakata jambo hilo la kuzini. Hapo Nabii Yusuf (‘Alayhis Salaam) kutaka kujiokoa na dhambi hilo alimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala):

Ewe Mola wangu Mlezi! Napendelea zaidi gereza kuliko haya wanayoniitia; na usiponiondolea hila zao nitawaelekea na nitakuwa miongoni mwa wajinga (wafanyao maasi)” ().

 

Maombi hayo yake ya ikhlaasw yakapokewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na hivyo kuondoka katika mazingira hayo mabaya.

 

Kosa lako ulilofanya ambalo ni aina mojawapo ya zinaa ni kukaa faragha na shemeji yako. Hilo ni jambo ambalo limekatazwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwani watatu wenu ni shetani. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

Tahadharini na kuingia kwa wanawake”. Akaulizwa: “Je, ham-wa (ndugu ya mume [shemeji])”. Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Huyo ni mauti” (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Na katika Hadiyth nyengine, akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakai faragha mwanamke na mwanamume isipokuwa watatu wao ni shetani. Hakika shetani hutembea kama damu mwilini mwa mwanadamu”.

 

Amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho, basi asikae peke yake na mwanamke asiyekuwa maharimu yake pamoja naye, kwani watatu wao ni shetani” (Ahmad).

 

Tunafahamu kuwa shetani ni adui wetu wa jadi na hatutakii mema na mazuri.

 

Kuwa kwako karibu na shemeji yako ndiyo kutakuletea matatizo zaidi kuliko kutatua baina ya hao wanandoa. Hiyo ni kwamba lau kakako atakuja jua ukaribu wenu wa namna hiyo sijui anaweza kukufanya nini? Je, ataanza kukuchukia na kuondoa usaidizi wake au vipi? Ikiwa uhasama unaweza kuwa namna hiyo je, hamujaogopa basi kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala)? Kisha kusikiliza mashtaka ya upande mmoja sio sawa kwani unapata shida anazokumbana nazo mmoja wao peke yake kati ya wawili hao. Inatakiwa kwako baada ya kuelezwa na kuyasikia ya shemeji yako umuite nduguyo naye akueleze ili upate toa uamuzi. Au uwalete wote pamoja umsikilize mmoja baada ya mwengine kabla ya kuwa unao uwezo ima ya kuwapatia nasiha au kutatua shida kutoka shinani mwake katika matatizo hayo. Ikiwa kumkalisha chini nduguyo ni vigumu usiwe ni mwenye kusikiliza malalamishi ya shemeji yako kwani itakuwa nadharia kama sasa kuwa nduguyo ni mkosa bila hata kufanya mengi yanayotakiwa katika kusikiliza kesi za watesi. Yatakiwa tuelewe kuwa msingi mkuu wa Uislamu ni: “Mtu anakuwa hana hatia mpaka ithibitishwe kinyume chake”.

 

Kuhusu kaka yako kwenda kuzini, je, upo ushuhuda wowote kuhusu hilo? Ikiwa hamna, hayo katika sheria yanachukuliwa ni masingizio na anayehusika kufanya hayo masingizio anapewa adhabu ya kupigwa mijeledi 80.

 

Hali hiyo ya zinaa baina yenu ni lazima itafika ikiwa tumeacha maagizo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na ukitojichunga utajikuta umezini kikweli na pengine shemejiyo abebe mimba yako. Ikifika hali hiyo, mnategemea nini na mtakuwa katika hali gain wakati huo? Je, mumefikiria yote hayo? Au ni vishawishi vya shetani vya muda mfupi vyenye kuwapumbaza?

Ni masikitiko makubwa kuwa mke anasema kuwa mumewe anazini na sasa nyinyi mnataka kutumbukia huko huko kwenye kitanda chake ndani ya nyumba yake!! Hili sijui mnalionaje nyinyi?

 

Hakika ni kuwa japokuwa hamjazini kwa kujamiiana lakini mmezini kwa njia nyingi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametueleza kuwa jicho kwa kuangalia linazini, masikio, midomo, mikono, miguu na viungo vyengine vyote vinazini. Na kwa kuwa mmefika hata kupigana mabusu mmekaribiwa zaidi na zinaa yenyewe.

 

Inawezekana kuwa Imani ipo lakini ikiwa mngekuwa mnamuogopa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kihakika hamgefika katika kupigana mabusu. Kuswali peke yake si hoja, kwani yapo madhambi ambayo yanafuta thawabu za Swalah. Swalah inatakiwa imuepushe mtu na machafu ambayo nyinyi mnayaendea polepole. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

 

Bila shaka, Swalah humzuiliya mtu mwenye kuiswali mambo machafu na maovu, na kwa yakini kumdhukuru Allaah ni jambo kubwa kabisa. Na Allaah Anajua mnayoyatenda” (29: 45).

 

Je, Swalah mnayoswali imewaepusha na machafu na maovu ikiwa mnapigana busu? Nadhani jawabu ya swali hili litatoka kwako.

 

Kwa hakika zifuatazo ni nasiha zetu ambazo zinaweza kuwasaidia sana:

 

(a)  Kuwa na niya nzuri na ikhlaasw katika matendo yako.

 

(b)  Tambua kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anakuona wakati wote. Katika hilo Atakupatia thawabu kwa mema unayoyafanya hata yakiwa ni wizani wa atomu na unapofanya maovu unaandikiwa madhambi. Ufahamu kuwa baadaye utahesabiwa na Aliye muadilifu na wala hutodhulumiwa.

 

(c)  Kukumbuka mauti, kwani maisha ya hapa duniani ni mafupi. Je, umejitayarisha vipi kukutana na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala)? Pia kujikumbusha Akhera kwa kuzuru makaburi.

 

(d)  Kutekeleza ‘Ibaadah kama inavyotakiwa kwa kufuata Sunnah za Bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

(e)  Kusoma Qur-aan kwa mazingatio na kujaribu kuyafuata maagizo yake katika maisha yako. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatueleza: “Na wanaposomewa Aayah Zetu huwazidishia Imani, na wakamtegemea Mola wao Mlezi tu” (8: 2).

 

(f)    Kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kwa wingi kwa kumtakasa kwa kusema (SubhaanAllaah), kumtukuza na kumsifu (AlhamduliLlaah), kumpwekesha (Laa ilaaha illa Allaah), Allaahu Akbar (Allaah ni Mkubwa). Pia kuleta nyiradi za asubuhi na jioni. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anaesema: “Wale walioamini na zukatulia nyoyo zao kwa kumkumbuka Allaah. Sikilizeni! Kwa kumkumbuka Allaah nyoyo hutulia” (). Pia: “Hakika wanaoamini kweli ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao hujawa hofu” (8: 2).

 

(g)  Kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Akuletee la kheri ili usiwe pale nyumbani wakati mwingi. Hilo ni ima kupata nafasi ya masomo ikiwa bado wewe unataka kuendelea na masomo, kibarua, kazi ya kudumu na kadhalika. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Akusaidie katika hilo.

 

(h)  Kuhama mazingira ya madhambi. Hapo ulipo unakaribia kila siku katika kuyaendea madhambi kwa njia moja au nyingine japokuwa huzini kwa kukutana kimwili na shemeji yako. Tumetoa mfano wa vijana wa pango, na pia Nabii Yuusuf (‘Alayhis Salaam) ambao walihama katika sehemu zao au kuomba kufungwa jela ili wapate kuepukana na madhambi. Nawe huna budi kutafuta njia yoyote ile ya kuwa anapotoka kakako hutakuwa nyumbani na utarudi tu anapokuwa amerudi. Hilo linaweza kufanyika ikiwa utajiunga na masomo au utapata kazi au utakuwa unatoka asubuhi na hurudi mpaka jioni. Ikiwa hutoweza kufanya hivyo, basi unapaswa uhame hapo haraka sana, maana huruhusiwi kuwa faragha na mke wa kaka yako ambaye si maharimu wako.

 

 

Soma makala hii muhimu sana inayohusiana na masuala hayo:

Ikhtilaatw (Kuchanganyika Wanaume Na Wanawake)

Ama kuhusu kuzini na kukurubia zinaa tunaweza kuelewa hilo kutokana na Aayah ifuatayo:

Wala msikaribie zinaa. Hakika hiyo zinaa ni uchafu mkubwa na ni njia mbaya sana” ().

 

Zinaa ni kitendo ambacho tupu mbili, ya mwanamme na mwanamke ambao hawajaoana kisheria zinaingiliana katika tendo la ndoa. Ama mkiwa mmevua nguo, kulala kwenye kitanda kimoja na mkawa mmejifunika shuka moja haihesabiwi kisheria kuwa ni zinaa. Kukaribia zinaa ni mambo yote yanayofanywa na vishawishi vyake ambavyo vinaweza kukupeleka katika zinaa yenyewe. Mfano wake ni kukaa faragha na mwanamke unayeweza kumuoa, kumuangalia mwanamke kwa matamanio, kutembea kwenda katika maagano na mwanamke, kumshika, kumbusu na kadhalika. Kwa ufupi ni kuwa kila kinachokupelekea katika zinaa ni kuikaribia.

Mshairi mmoja wa wakati huu amesema: “Mtizamo, kisha kutabasamu, kisha salamu, kisha mazungumzo, kisha ahadi na mwisho uharara wa kitandani (kujamiiana)”.

 

Ndugu zetu tutahadhari sana kwani hii dunia ina ghururi. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Akutoe katika janga hilo baya pia Atuepushe sisi na hayo.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share