Kampa Talaka Mkewe Kwa Fatwa Ya Shekhe Kuwa Ndoa Haisihi Baada Ya Kumuingilia Kwa Nyuma

 

SWALI:

Asalamu alaykum,

Ilikuwa ni talaka ya mwisho imebakia, nilikuwa nina wasi wasi juu ya jambo hili kuhusu ndoa yetu,kuna baadhi ya siku mke wangu akiwa katika hedhi napenda kumuingilia kwa nyuma, nikenda kwa sheikh kuulizia akaniambia kwamba tayari talaka imeshapita,hivyo hapo hapo nikaandika talaka kwa mke wangu, nikakaa muda baadae nikenda zaidi kuulizia kwa sheikh mwengine akaniambia kwamba talaka kwa tendo hilo sio talaka bali ni haraam, sasa swali langu ni kwamba nilimuacha mke wangu bila ya kukusudia na ninampenda sana kwa sababu nimeshazaa nae watoto na ni msaidizi wangu kwa kila kitu, hivyo naomba munisaidie jee ikiwa tayari talaka nimeshaiandika na ni ya mwisho bila kuwa na elimu nayo, na siwezi kuishi bila ya yeye hivyo Sheikh nifanyeje ili nirudiane na mke wangu mpendwa, tafadhali  naomba jibu haraka.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu maisha yako na mkeo. Tumesoma kwa kustaajabu kuwa unasema kuwa huwezi kuishi bila ya mkeo kinyume na uhakika kuwa tayari ulikuwa umempatia talaka mbili na pia kumuingilia nyuma!! Hii ni ishara ya kuwa yapo matatizo ambayo hutaki kuyazungumzia. Vipi utampenda mtu na kisha uwe utatoa talaka yenye kuvunja ndoa yako, na pia kumuingilia kinyume cha maumbile tena zaidi ya mara moja? Je, kweli ndugu yetu wewe unampenda, kumjali na hata kumuheshimu huyo mke?? Ingawa suala la talaka ya tatu ina utata kwani kumuingilia mkeo kwa nyuma hakusababishi talaka bali ni madhambi makubwa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala).

 

Kilichostaajabisha zaidi ni kuwa mtu anaweza kumpenda mkewe zaidi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) jambo ambalo ni kinyume na Uislamu kabisa. Vipi mtu atakwenda kinyume na maagizo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kumpenda mkewe?

 

Ndugu zetu inatakiwa tutahadhari sana kwenda kwa Mashaykh ambao hawajamakinika katika elimu zao au watu wanaojiita Mashaykh lakini hawana sifa hiyo. Pia tunapotolewa maamuzi yenye uzito kama talaka inatakiwa tuende tupate ushauri kwa Shaykh mwengine au mwanachuoni mwenye kujulikana na kuaminika elimu yake, kama alivyofanya muulizaji hapa lakini amechelewa na doa tayari lishaingia. Mashaykh pia watahadhari kutoa fatwa haraka haraka kabla ya kuyakinisha jambo lenyewe na wala wasione hayaa kusema hawajui. Imaam Maalik amesema kusema sijui kwa jambo ambalo hulijui kweli ni nusu ya elimu. Ni afadhali maradufu kusema sijui kuliko kupotosha watu katika mas-ala ya Dini yao.

 

Huu ndio utabiri aliotupatia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa kutakuja Mashaykh wa uongo ambao watapotea wao na kupoteza wengine, na hii ni alama mojawapo ya siku ya Qiyaamah. Amesema ‘Abdillaah bin ‘Amru bin al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘Anhuma): Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Hakika Allaah haichukui elimu kwa kuing’oa (toka katika nyoyo) za watu. Lakini Anaichukua elimu kwa kuwafisha wanazuoni. Mpaka kutafika wakati hakutabakia mwanachuoni hata mmoja. Watu watawaweka viongozi wajinga ambao watakuwa wanaulizwa (maswali ya Dini), na watatoa majibu bila ya ujuzi, watapotea (wao wenyewe) na wanapoteza (watu wengine)” (al-Bukhaariy, Muslim na at-Tirmidhiy).

 

Katika talaka hii vipo vipengele viwili ambavyo vinatakiwa vitazamwe kabla ya kutoa uamuzi wa suala hilo. Hata hivyo, ikiwa yale yaliyosemwa na muulizaji si hakika atambue kuwa madhambi yote yatarudi kwake.

 

Kipengele cha Kwanza: Talaka ya aliyekosea nayo ni ile ya mtu ambaye hajakusudia kutamka talaka kwa uhakika wake, kwani yeye alikusudia lafdhi nyingine ulimi ukamtangulia kwa neno la talaka bila kukusudia. Mfano ni kutaka kusema mtu kwa mkewe: Anti Twaahir (Wewe ni tohara?), akakosea kwa kusema: Anti Twaaliq (Wewe umeachwa).

 

Kuhusu hili jamhuri ya wanazuoni isipokuwa Abu Haniyfah wamesema kuwa talaka aina hii huwa haikupita kwa njia ya Dayaanah (yaani baina ya mja na Allaah) wala kwa Qadhwaa’ (itakapopelekwa kwa Qaadhi kesi hiyo ahukumu) ikithibiti kukosea kwake. Ikitothibiti kukosea kwake talaka itakuwa imepita kwa Qadhwaa’ na siyo kwa Dayaanah. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘Anhuma) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah Amenisamehea Ummah wangu kukosa, kusahau kwao na waliyotendeshwa nguvu” (Ibn Maajah na al-Bayhaqiy, na imesahihishwa na al-Albaaniy).

 

Prof. Muhammad Saalim Badamana katika kitabu chake, Hadiyth Arbaini Nawawi: Tafsiri na Sherehe Yake, uk. 122 kuhusu Hadiyth ya hapo juu amesema: “Kusudio la neno makosa hapa ni mtu mwenye kufanya jambo kinyume na Sharia kwa ujinga au kutojua. Mfano wa kutojua ni mtu kula nyama ya nguruwe akifikiria ni ya ng’ombe au kondoo. Ama kuwa mjinga wa Shari‘ah ni lazima yawe mambo yenyewe si yale maarufu sana hukumu yake kwa Muislamu. Kwani mambo ya kawaida ni wajibu kwa Muislamu ayajue”. Kusahau pia kunasamehewa kwa mujibu wa Qur-aan inayotufundisha tuwe ni wenye kuomba kila wakati: “Ewe Mola wetu Mlezi! Usitupatilize tukisahau (tukaacha yaliyo mema) au tukikosa (tukafanya mabaya)” (2: 286).

 

Kulingana na maelezo ya muulizaji ni kuwa nia yake si talaka na bado anamtaka mkewe kwa udi na uvumba, hivyo inaingia katika kipengele hichi cha kwanza.

 

Kipengele cha Pili: Hii talaka pia inaweza kuingia katika kule kutenzwa nguvu, kwani yule Shaykh wa awali alimwambia kuwa kumuingilia mkeo kwa nyuma huwa talaka imepita japokuwa ni kinyume na hivyo. Kwa minajili hiyo muulizaji akalazimika kutoa talaka ambayo ndiyo ya mwisho. Jamhuri ya wanazuoni wakiwemo Maswahaba kama ‘Umar, ‘Aliy, Ibn ‘Umar, Ibn az-Zubayr (Radhiya Allaahu ‘anhum), pia Maimamu kama Maalik, ash-Shaafi‘iy, Ahmad, al-Awzaa‘iy, Ishaaq, Abu Thawr, Abu ‘Ubayd, Ibn Taymiyah na kipote cha watangu kinaona kuwa talaka haipiti.

 

Wanazuoni kama Ibn Taymiyah, Ibn Rajab al-Hanbaliy na Ibn ‘Uthaymin (Allaah Awarehemu wote) wametueleza kuwa talaka yoyote inayotolewa kwa maelezo au maalumati ya kimakosa huwa haikupita. Kwa ajili hiyo bado huyo ni mkeo lakini tunakunasihi uwe una tahadhari ya hali juu ikiwa kweli ulliyoyasema ni kweli.

 

Kwa hiyo yaliyoelezwa hapo juu ni kwa mujibu wa hali aliyotueleza muulizaji nasi hatuna elimu ya ghaibu kwa uhakika wa jambo lenyewe. Kwa maelezo hayo imeonekana kuwa talaka hiyo haikupita, lakini ikiwa maelezo siyo sawa kama alivyoeleza muulizaji naye ni mjuzi wa ukweli wenyewe afahamu kuwa atakuwa ni mwenye kupata madhambi na talaka itakuwa imepita. Hivyo, akiendelea kukaa na mtalaka wake atakuwa anazini.

 

Pia hapa tunataka kukupatia nasaha kuwa kwa maelezo ya awali uliyoelezwa kwa madhambi anayopata mja kwa kumuingilia mkewe kwa nyuma inabidi ukome na hilo.

 

Soma maudhui yafuatayo ujue ubaya na uchafu ulioufanya:

 

Mume Wangu Ananitaka Njia Isiyo Ya Halali

 

Ni muhimu kwako kurudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kikweli kweli, utubie kwa madhambi uliyofanya, uazimie kutorudia tena na ufanye mema kwa wingi. Pia kuonyesha kuwa kweli umejuta kwa kitendo ulichofanya unahitajia kumwambia mkeo awe ni mwenye kukataa katakata ombi lako ikiwa unataka kustarehe naye kwa njia ambao imekatazwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Fanya juhudi na bidii za ziada ili usitumbukie katika shimo hilo mara ya pili.

 

·                     Maana ya Tawbah (Toba)

·                     Tawbah Ya Kweli Na Masharti Yake

·                     Wakati Bora Wa Kuomba Tawbah

·                     Vipi Kuomba Maghfira Na Tawbah?

 

Tufahamu kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasamehe madhambi yote. Pia ufahamu kuwa mbali na kuwa talaka haikupita lakini umebakisha talaka moja peke yake. Ikiwa unasema unampenda kweli mkeo na huwezi kuishi bila yeye usiwe ni mwenye kucheza nayo. Ifahamike kuwa ikishatolewa talaka ya tatu hamuwezi kurudiana tena mpaka mtalaka wako aolewe na mume mwingine kisha aachwe na mume huyo baada ya kuingiliwa.

 

Na fahamu kuwa mkeo ana haki sana ya kukataa kuishi na wewe au kurudiana na wewe kutokana na matendo hayo machafu ya Liwaat, kwa sababu hafanyi hayo ila mtu muovu na asiye na khofu na Mola wake.

 

Tunakuombea maghfirah kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala), na Akuongoze kwenye njia ya sawa na Akupe Iymaan na khofu Kwake na baada ya mabaya hayo uwe ni mja mwema na mfanya mazuri inshaAllaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share