Mume Anamtaka Ajimai Naye Njia Isiyo Ya Halali

SWALI:

Asalamu aleikum warahmatullahi wabarakatu.

kwanza kabisa mimi nimeolewa nina miaka 16, lakini kwenye ndoa yangu nina matatizo na mume wangu na ni kuhusu ya kwamba huwa ana tabia ya kutaka kuniingilia sehemu ambayo haijahalalishwa kidini na ni haraam na kila ninapojaribu kumueleza hayo anaapa na kusema kuwa hatorudia lakini hakuna faida ana rudia haya daima sasa sijui nifanyeje.  Naomba munipe nasiha itakayo nifaa mpaka Kesho Akhera.

Asalamu aleiykum.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ahli zake, Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka siku ya Mwisho.

Haya ni baadhi ya matatizo ambayo dada zetu wanakumbana nayo katika unyumba.  Hili tatizo hutokea kwa sababu ya malezi kwa mwanamme au mwanamke na pia kutofundishwa wajibu wa kisheria kwa wote wawili.  Hivyo mume mara nyingi anakuwa hajui wajibu wake na haki yake katika ndoa na vile vile mwanamke.  Hii hupelekea mmoja wao kuangukia katika haramu au kutotekeleza wajibu wake.  Mara nyingi haya matatizo hutokea kwa sababu wazazi hawakuchunguza kwa kina kabla harusi.

Kumuingilia mwanamke kwa njia ya nyuma ni haramu, bali amuingilie katika njia iliyohalalishwa kama ilivyo katika kauli ya Allaah سبحانه وتعالى:   

((نِسَآؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُواْ حَرْثَكُمْ أَنَّى شِئْتُمْ وَقَدِّمُواْ لأَنفُسِكُمْ وَاتَّقُواْ اللّهَ وَاعْلَمُواْ أَنَّكُم مُّلاَقُوهُ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ))

((Wake zenu ni kama konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo. Lakini jitangulizieni kheri nafsi zenu, na mcheni Allaah , na jueni kuwa hakika nyinyi mtakutana Naye. Na wape bishara njema Waumini)) [2:223]

Kama tunavyoona katika hiyo aayah, Mwenyeezi Mungu katolea mfano shamba akionyesha kuwa ni mahali panapolimwa, na penye kulimwa panawezwa kulimwa kwa njia nyingi ingawa lengo ni kutatarajiwa kutoa mazao, na makusudio hapa kwa mwanamke, ni pahali anapoingiliwa mwanamke ambapo ni sehemu anayozaliwa mtoto. Kwa hiyo mtu kapewa ruhusa ya kumuingilia mkewe kwa mitindo mbalimbali lakini kwa sharti pawe sehemu ya mbele ambayo ndiyo inayotoa mazao ambayo ni mtoto. Na kumuingia mke kwa njia ya nyuma kunakwenda kinyume na  fitrah (asili ya maumbile ya binaadamu). Vile vile mwanamke atakuwa amedhulumika kwa kupata sehemu yake ya kustarehe na mumewe  na sehemu ya nyuma ni sehemu inayotoa uchafu na pia kitendo ni kitendo ambacho kimeharamishwa na Mola Mtukufu.

Kwa jinsi kitendo hichi kilivyokuwa ni kiovu kabisa, tunaona dalili ya kuharamishwa kwake  kutoka katika Qur-aan na pia kuna dalili nyingi katika Hadiyth zifuatazo za Mtume صلى الله عليه وآله وسلم za kuharamishwa ambazo zina MAONYO MAKALI kabisa.  Hivyo inampasa Muislamu ajiepushe kabisa nacho kitendo hicho ili aepukane na laana, adhabu na ghadhabu za Allaah سبحانه وتعالى :  

 Hadiyth ya kwanza:  Haramu kitendo hiki:

عن خزيمة بن ثابت رضيَ اللَّهُ عنهُ انه قال:  قالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم: ((إِتْيَانُ النسَاءِ فِي أَدْبَارِهِنَّ حَرَامٌ)) الألباني  في السلسلة الصحيحة  

Imetoka kwa Khuzaymah bin Thaabit رضيَ اللَّهُ ambaye amesema: "Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Kuwaingilia wanawake kwa nyuma ni haraam)) [Shaykh Al-Abaaniy katika Silsilatus-Swahiyhah]

 Hadiyth ya pili: Allaah سبحانه وتعالى Hatomtazama anayefanya kitendo hiki: 

عن ابنِ عَبَّاس رضي الله عنهما  قال: قال رسول الله)) لا يَنْظُرُ اللَّهُ إلى رَجُلٍ أَتَى امْرَأَةً في دُبُرِهَا))

صحيح ابن حبان  

 Imetoka kwa ibn 'Abbaas رضي الله عنهما   ambaye amesema:  Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Allah Hatomtazama mwanamume anayemuingilia mwanamke kwa nyuma)) [Swahiyh Ibn Hibbaan]

Hadiyth ya Tatu: Amelaaniwa anayefanya kitendo hiki:    

قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( ملعون من يأتي النساء في محاشِّهن: أي أدبارهن    (( رواه ابن عدي وصححه الألباني في آداب الزفاف   

((Amelaaniwa anayewaingilia wanawake kwa njia ya nyuma)) [Imepokelewa na ibn 'Udayy na amesema ni sahiyh Shaykh Al-Albaaniy katika Adaabuz-zafaaf]

 

Hadiyth ya nne: Amekufuru anayefanya kitendo hiki:  

 عن أبي هريرة رضي الله عنه ((من أتى حائضا أو امرأة في دبرها أو كاهنا فصدقه بما يقول فقد كفر بما أنزل على محمد)) صحيح ابن ماجه  و قال الألباني إسناده صحيح  

Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه : ((Atakayemuendea (atakayemuingilia) mwenye hedhi au mwanamke nyuma au atakayemuendea mtabiri akamuamini anayomuambia, atakuwa amekufuru yaliyoteremshwa kwa Muhammad)) [Sahiyh ibn Maajah na kasema Shaykh Al-Albaaniy kuwa isnaad  yake ni Sahiyh]  

 

Hadiyth ya tano:

عن ابن عباس رضي الله عنهما قال:  جاء عُمَر بن الخطاب إلىٰ رسول الله فقال: يا رسول الله، هلكتُ! قال: (( وما الذي أهلكك؟)) قال: حَوَّلْتُ رَحْلِي الليلة، فلم يردَّ عليه شيئاً، فأُوْحِيَ إلىٰ رسول الله هذه الآيةُ: {نساؤكم حرث لكم فأتوا حرثكم أنىٰ شئتم} يقول: أَقْبِلْ، وأَدْبِرْ، واتقي: الدُّبر، والحَيضة   سنن النسائي الكبرى  

Imetoka kwa Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما ambaye amesema:  Alikuja 'Umar ibnul-Khatwaab kwa Mjumbe wa Allah akasema: Ewe Mjumbe wa Allah, Nimeangamia! Akasema: ((Nini kilichokuangamiza?)) Akasema: Nimepindua kipando changu usiku (nimemuingilia mke wangu  sehemu ya mbele lakini kwa kumgeuza) Lakini hakumjibu kitu. Akateremshiwa Aayah hii ((Wake zenu ni kama konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo)) Anasema: (unaweza kumuingilia) kwa mbele na kwa kumgeuza na chunga kumuingilia nyuma na wenye hedhi. [Sunnan An-Nasaail-Kubraa]

 

Hadiyth ya sita

عن أم سلمة قالت: لما قدم المهاجرون المدينة على الأنصار تزوّجوا من نسائهم، وكان المهاجرون يجبون وكانت الأنصار لا تجبي، فأراد رجل من المهاجرين امرأته على ذلك، فأبت عليه حتى تسأل رسول الله صلى الله عليه وسلم، قالت: فأتته فاستحيت أن تسأله، فسألته أم سلمة فنزلت: {نساؤُكُمْ حَرْثٌ لَكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنّى شِئْتُمْ} وقال: «لا إلاّ في صَمَّامٍ واحِدٍ»  . : مسند الإمام أحمد  

Imetoka kwa Ummu Salamah رضي الله عنها kwamba: Muhaajiriyn walipokuja Madiynah kwa Maanswaar waliwaoa wanawake wao. Wanawake Wa Muhaajiriyn walikuwa wakilala kifudifudi (wakati wa kujimai na waume zao) na wanawake wa Maanswaar hawakuwa wakifanya hivyo. Mwanamume mmoja Muhaajir alitaka mkewe afanye hivyo akakataa. Akaenda kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم lakini aliona haya kumuuliza swali hilo, kwa hiyo Ummu Salamah alimuulizia kisha Aayah ikateremshwa inayosema ((Wake zenu ni kama konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo))  Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  akasema: ((Hapana! (Sio kila sehemu upendayo) bali ni mbele tu. [Musnad ya Imaam Ahmad] 

Nasaha zetu kwa dada yetu ni kama zifuatazo:-

1.     Endelea kumcha Allaah سبحانه وتعالى bila kuyumba yumba.

2.     Kuwa na istiqaamah na usimkubalie mumeo kukuingiza katika tendo hilo la haramu.

3.     Mfanyie Da‘wah mumeo kwa hekima na mawaidha mazuri huenda akabadilika kutokana na tabia hiyo yake mbovu na mjulishe kuhusu Aayah yenye makatazo hayo katika Qur-aan na Hadiyth  

4.     Ikiwa imeshindikana kumrekebisha basi itisha kikao baina ya wazazi wako na wazazi wa mume. Na ikishindikana kabisa, bora udai talaka yako uepukane na haraam hiyo.

 

Tanbihi:

       Mume kumuingilia mke kwa nyuma haina maana kwamba mke ameachika (Talaka) moja kwa moja kama wanavyofahamu wengi, bali ana haki mke kudai talaka lakini hakuna dalili kwamba hukumu ya talaka iwe imepita katika kitendo hiki.                   

Tunakuombea kwa Allaah  Akupatie moyo wa kukataa maovu na Akupatie uimara katika kudumu na mazuri. Tunamuomba Allah Amuepushe mumeo na tabia mbaya hiyo na Amrudishe katika njia ya haki.  Tunakuombea muafaka katika kutatua tatizo hilo.

Na Allah Anajua zaidi.

 

 

Share