Kufunga Na Kusherehekea Siku Inayosemekana Ni Ya Israa na Mi'iraaj

SWALI:

 

Naomba mtujulishe kama kufunga tarehe 27 ya mwezi huu wa rajab na kusherehekea kama ni sahihi?

 

ahsanteni

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Swali lako ni zuri na muhimu na lahitaji kufafanuliwa kwa kuwa ni jambo limekita kwa wengi miongoni mwa Waislam na kuamini kuwa kufanya hivyo ni sahihi na kuna ujira mwingi.

Tukio la Israa na Mi’iraaj ni tukio adhimu na ni miongoni mwa miujiza aliyopangiwa Mtume wetu karimu na Mola wake Mtukufu. Anasema Allaah kuhusiana na tukio hilo:

   بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ  

 

((سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَى بِعَبْدِهِ لَيْلاً مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ البَصِيرُ))

 

Kwa Jina La Allaah Mwingi Wa Rahmah Mwenye Kurehemu

 

((Subhaanah!  (Utakasifu ni wa) Ambaye Amemchukua mja Wake (sehemu ya) usiku kutoka Al-Masjid Al-Haraam mpaka Al-Masjid Al-Aqswaa ambao Tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake (amechukuliwa) ili Tumuonyeshe baadhi ya Aayaat (miujiza, ishara, dalili) Zetu. Hakika Yeye (Allaah) ni As-Samiy’ul-Baswiyr (Mwenye kusikia yote daima - Mwenye kuona yote daima).)) [Al-Israa: 1]

 

Hapana shaka kwamba safari ya Israa na Mi'iraaj, (safari ya usiku mmoja kupanda Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika mbingu saba na kurudi siku hiyo hiyo kwamba ni jambo tukufu alilojaaliwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na limethibitika ukweli wake. Hali kadhalika ni jambo kuu la ajabu katika maajabu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kuonyesha uwezo na daraja Yake juu ya Viumbe Vyake.

 

Usahihi wa tukio hili liko katika dalili kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alichukuliwa kupelekewa mbinguni na milango ilifunguliwa kwa ajili yake akapita kila mbingu na kuonana na Mitume walioko katika kila mbingu hadi kufika mbingu ya saba ambako Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Alimuamrisha Swalah tano. Idadi ya Swalah hizo kwanza ilikuwa ni khamsini lakini Mtume wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alirudi kwa Mola Wake kwa kuomba hadi zikapunguzwa kuwa ni Swalah tano ambazo Muislamu atakapozitimiza atapata thawabu za Swalah khamsini kwa vile kila kitendo chema kinalipwa mara kumi. Na Ndipo ibada ya Swalah ikawa na daraja ya juu, nzito na muhimu kuliko ibada zote.  

 

Ama kuhusu usiku wenyewe wa tukio hili la Israa na Mi'iraaj hakuna Hadiyth Swahiyh inayoelezea kuwa ilikuwa katika mwezi wa Rajab au tarehe 27 ya mwezi huu wa Rajab kama wengi wanavyodhania. Usimulizi wowote unaotaja mwezi au tarehe ya tukio hili umekosa dalili Swahiyh kama wasemavyo Maulaama wa Hadiyth. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa hikma Yake Amewafanya watu wasahau siku hii. Hata kama ingelikuwa hiyo siku imetajwa katika dalili basi isingeliruhusiwa Muislamu kuipwekesha kwa kufanya ibada fulani au kusherehekea. Hii kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala Maswahaba zake hawakufanya hivyo. Na ingelikuwa kuipwekesha ni amri iliyo katika Dini yetu basi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) angelitoa mafunzo kwa Ummah wake kwa kauli au vitendo. Na ingelikuwa imefanyika zama zake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) basi bila shaka ingelijulikana na usimulizi ungelitufikia kwa isnaad Swahiyh kama tulivyopata mafunzo mengineyo ya uhakika.

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika khutbah yake mwisho kwenye Hijjatul-widaa' alisema: 

 ((يا أيها الناس،  ما من شيء يقربكم إلى الجنة ويباعدكم من النار إلا وقد أمرتكم به، وما من شيء يقربكم من النار ويباعدكم من الجنة إلا وقد نهيتكم عنه))

((Enyi watu, hakuna jambo lolote ambalo litakukurubisheni na Pepo na kukuepusheni na moto ila nimekuamrisheni nalo. Na hakuna jambo lolote litakalokukurubisheni na moto au kukuepusheni na Pepo ila nimekukatazeni nalo)).

 

Na ni amri kutoka kwa Mola wetu Mtukufu kufuata yote aliyotufunza Mjumbe Wake:

 ((وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا))

((Na lolote (lile) analokupeni Rasuli (Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) basi lichukueni, na (lolote lile) analokukatazeni, basi acheni.)) [Al-Hashr: 7]

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa Mkweli Muaminifu aliyetimiza ujumbe aliopewa kwa ukamilifu na ndipo dini yetu ilipokamilika Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

  ((الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الإِسْلاَمَ دِينً))

((Leo Nimekukamilishieni Dini (yenu), na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe (ndio) Dini yenu.)) [Al-Maaidah: 3]

 

Hivyo mwenye kufanya kitendo ambacho hakimo katika Dini yetu itakuwa ni kupoteza muda wake kwa ibada isiyo na thamani kama tulivyoonywa:

 (( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika dini yetu) basi kitarudishwa)) [Al-Bukhaariy]

  

 

Mambo ya bid'ah yafanywayo siku ya tarehe 27 Rajab:

 

  •       Kufunga siku hiyo ya tarehe 27 Rajab:

 

عن  خرشة بن قال:  رأيت  عمر بن الخطاب يضرب أكف الرجال في صوم رجب حتى يضعونها في الطعام ويقول رجب وما رجب إنما رجب شهر كان يعظمه أهل الجاهلية فلما جاء الإسلام ترك مجمع الزوائد : 3/194

“Nilimuona Umar akiichapa mikono ya wale waliyokuwa wamefunga mwezi wa Rajab mpaka walipofungulia, na alikuwa akisema huu ni mwezi uliyokuwa ukiheshimiwa sana wakati wa jahiliya. (kabla ya Uislamu) Na ulipokuja Uislam Ukaachwa. (Majma'u az-Zawaaid Mj. 3 Uk. 194)

  

 
  •         Du’aa maalum ambazo husomwa hasa wakati wa mwezi huu wa Rajabu zote ni za kuzua ni Bid’aa.
 
 
  •        Kuzuru makaburi hasa kwenye mwezi huu wa Rajab ni Bid’aa kwa sababu makaburi yanapaswa kufanyiwa ziara muda na wakati wowote ule wa mwaka.
 
 
  •         Swalaatur-Raghaaib (Swalah Ya ar-Raghaaib). Swalah hii huswaliwa mwanzo mwanzo mwa mwezi wa Rajab. Hakukujulikana Swalah ya aina hii katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala Maswahaba zake watukufu wala kwa Watangu Wema (Salafus-Swaaalih), bali ilikuja kuzushwa na kuwa maarufu katika zama hizo bora kupita. Wanachoni wengi wakubwa wameikemea. Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyah (Rahimahu Allaahu) amesema: Swalaat ar-Raghaaib ni bid’ah kwa mujibu wa maafikiano (Ijmaa’) ya wanazuoni wa Dini. Kama Imaam, Maalik, Imaam ash-Shaafi’iy, Imaam Abu Haniyfah (Allaah Awarehemu wote) anasema kuwa Hadiyth iliyosimuliwa kuhusiana nayo ni Hadiyth mbovu na ya kuzushwa kwa mujibu wa kongamano la wanachuoni mabingwa wa Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo ni bora Waislam wakae nayo mbali na wakemee aina za bid’ah kama hizo zinazoenea katika jamii ya Kiislam
 
 
  •         Swalaat Ummu Dawuud kwenye nusu ya Rajab.
 
 
  •         Kuna madai baatil kwamba matukio makubwa yametokea kwenye mwezi huu wa Rajab. Lakini hakuna mapokezi yoyote katika hayo yaliyokuwa ni sahihi. Inadaiwa kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizaliwa kwenye usiku wa mwanzo wa mwezi wa Rajab! Na kwamba alishushiwa Wahyi kwa mara ya kwanza kabisa kwenye tarehe 27 au tarehe 25 ya mwezi huu wa Rajab. Hakuna ushahidi wowote sahihi juu ya haya, na wala hakuna riwaya iliyothibiti kuhusiana nayo. Pia imepokewa katika Isnaad ambayo si sahihi kutoka kwa al-Qaasim bin Muhammad kwamba safari ya mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya Israa na Mi’iraaj ilifanyika kwenye tarehe 27 ya mwezi wa Rajab. Madai kama hayo yamepingwa vikali na wanachuoni wengi.
 
 
  •         Miongoni mwa bid’ah kubwa kubwa zinazofanyika kwenye mwezi huu ni usomaji wa Kisa cha Mi’iraaj na kusherehekea na kuadhimisha tukio hilo kwenye tarehe 27 ya mwezi huu wa Rajab, au kuutenga usiku huu kwa aina fulani fulani za ‘Ibaadah au kufanya ‘Ibaadah za ziada kama vile Qiyaam al-Layl au kufunga kwenye mchana wake. Vilevile kufanya sherehe kusherehekea. Baadhi ya sherehe huambatana na mambo ya haramu kama vile kuchanganyikana wanaume na wanawake kuimba na kucheza miziki, mambo haya yote hayaruhusiwi hata kwenye zile sherehe kuu mbili za ‘Iyd (‘Iyd al-Fitwr na ‘Iyd al-Adhwhaa) ambazo ndizo zinazotambuliwa kisheria katika Uislamu na ambazo tumewekewa sheria nazo na Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sembuse ya sherehe hizi za kuzushwa ambazo hazina mashiko sahihi katika Uislamu. Mbali ya hilo hakuna Ushahidi wowote kwamba Israa na Miraji ilifanyika kwenye Mwezi Ishirini na saba ya Mwezi huu wa Rajab! Hata kama itathibitishwa basi hakuna sababu iliyo wazi ya kuandaa sherehe kwenye siku hii kwa sababu hakuna mapokezi yoyote yaliyopokewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au kutoka kwa Maswahaba wake watukufu (Radhiya Allaahu ‘anhum) au kutoka kwa Watangu Wema (Salafus Swaalih) wa Ummah huu. Kama hilo lingekuwa ni jambo zuri basi bila shaka wangalilifanya wao mwanzo kabla yetu sisi.
 
 
Kwa nini Muislamu ajitakie mashaka zaidi ya kufanya ‘Ibaadah isiyokuwa na dalili? Kwa nini kwanza asitimize hizo ambazo tayari dalili zake ziko wazi? Kama Muislamu anapenda sana ‘Ibaadah ya kufunga basi afunge Swawm ya Daawuud lakini wangapi wanaoweza kufanya ‘Ibaadah hiyo?
Juu ya hivyo kufuata bid'ah (uzushi) ni upotofu na kujitakia mtu mwenyewe kuwa na makazi mabaya siku ya Qiyaamah:
 
(( إن خير الكلام كلام الله وخير الهدي هدي محمدصلى الله علي وسلم  وشر الأمور محدثاتها وكل محدثة بدعة وكل بدعة ضلالة وكلضلالة في النار)) أخرجه مسلم في صحيحه 

 

((Maneno bora  ni kitabu cha Allaah (Qur-aan) na uongofu mbora kabisa ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na jambo la shari kabisa ni uzushi, na kila jambo jipya (katika Dini) ni bid'ah (uzushi)  na kila bid'ah ni motoni))[Muslim katika Swahiyh yake]

 

 
Tukinaike na yaliyo Swahiyh na tushukuru kuwa muongozo tulioletewa kwetu kutoka kwa Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) umekamilika na hatuja haja ya kujipa mashaka zaidi ya kufanya ‘Ibaadah za bid'ah wakati tunashindwa kutimiza zile tulizofaridhishiwa ambazo zimethibiti.
 
 
Tunatumai kwa maelezo hayo tuliyonukuu yatamtosheleza mwenye kutaka kufuata haki kwamba kuipwekesha siku ya tarehe 27 Rajab kwa ‘Ibaadah yoyote au kusherehekea kwa aina yoyote kwamba sio katika mafunzo ya dini, hiyo ni bid'ah ipasayo kuepukana nayo. Muislamu akipenda kufunga apate thawabu za uhakika afunge Jumatatu na Alkhamiys, au siku za Ayyaamul-biydhw (Masiku meupe nayo ni tarehe 13, 14 na 15 katika kila mwezi), na Swawm ya Nabii Daawuud yaani siku afunge na siku aache. Na pia mwezi wa Sha'abaan unakaribia ambao anaweza kufunga siku zozote atakazo bila ya kuipwekeshe siku Fulani maalum wala kuupa umuhimu wa nusu ya Sha'abaan kwa kufunga na kuswali sana usiku. kama tunavyoona katika makala ifuatayo:
 
 
 
 

 

Allaah Atujaalie kuwa ni katika wale wenye kuheshimu mambo yaliyowekwa na shariy'ah na Kushikamana barabara na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa nje na ndani. Na mwisho wa maombi yetu ni kwamba Kila sifa njema ni za Allaah Mola wa ulimwengu wote.
 
Na Allaah Anajua zaidi

 

 


Share