Zingatio: Pepo Ni Tupu

 

Naaswir Haamid

 

Sasa umefika wakati, huyo kiumbe anasimamishwa mbele ya Muumba kwa ajili ya kuhisabiwa. Ah! Ndio kauli yake ya juu anayoweza kuitamka kuipa matumaini nafsi yake. Ilhali hakuna msamaha isipokuwa wa Mola wake. Mali zake hazina nafasi siku hiyo. Ni amali ndio inahesabiwa. Mwisho wake, anamalizia ndani ya Moto wa Jahannam. Allaah Tuepushe na adhabu hiyo ya moto wa Jahannam.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekwisha tubainishia halali na haramu, na kutuweka wazi kwamba mwenye kumtii yeye basi ataingia Peponi na mwenye kumuasi basi ataingia Motoni. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika khutbah yake mwisho kwenye Hijjatul-widaa' alisema:  ((Enyi watu, hakuna jambo lolote ambalo litakukurubisheni na Pepo na kukuepusheni na moto ila nimekuamrisheni nalo. Na hakuna jambo lolote litakalokukurubisheni na moto au kukuepusheni na Pepo ila nimekukatazeni nalo))   [Al-Bukhaariy]

Leo Waislamu tunamuasi Mola wetu kwa makusudi kabisa bila ya aibu wala haya yoyote. Hali ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekwishatuhakikishia kwamba sote tutaingia Peponi, isipokuwa tu kwa yule anayekataa. Ni kusema kuingia kwetu Motoni ni kwa kujitakia. Kwani yote ameshayaeleza, ufunuo ulio wazi upo mbele yetu kuufuata. Ni kipindi kifupi tu cha maisha kinatubabaisha hadi kumuasi Mola. Tumeshughulishwa na mihangaiko ya dunia, tukiipa mgongo Siku ya Mwisho.

 

Ikumbuke Siku ambayo Jahannam itaulizwa kama imejaa. Na itasema iletewe zaidi. {{“Siku Tutakayoiambia Jahannamu: “Je! Umejaa?” Nayo itasema: “Je! Kuna ziada (zaidi Naije tu!).”}} [Suratu-Qaaf: 30]

 

Basi na tujitayarishe kwa vitendo vyema ili tusije kuwa miongoni mwa wenye kutupwa ndani ya Jahannam hiyo. Kwani Pepo siku hiyo itaumbiwa viumbe wa ziada ili ipate kujazwa, ilhali Moto utanadi kutosheka na kusema basi.

 

Imetokana na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu). Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Zitajadiliana Moto na Pepo. Utasema Moto: Mimi ninawaathiri wenye kuleta jeuri na majabari, na Pepo itasema: Na kwangu haingii ila mtu aliye dhaifu, aliye chini na aliye dhalili. Basi Atasema Allaah kwa Pepo: “Hakika wewe ni Rahma Zangu, Ninamrehemu yeyote nimtakaye miongoni mwa waja wangu” – Na Atasema kwa Moto: “Hakika wewe ni adhabu Zangu, Ninamuadhibu yeyote nimtakaye miongoni mwa waja wangu. Na kila mmoja wenu nitakujazeni.” Ama kwa Moto haitojaa, mpaka Atakapoweka Mguu wake juu yake na kusema: Basi! Basi! Ama huko utajaa na watakusanyika baadhi ya wengine juu ya baadhi. Na wala Allaah Hamdhulumu Yeyote miongoni mwa waja Wake. Ama Pepo, basi hakika Allaah Ataumba viumbe wengine kwa ajili yake. Imepokewa na al-Bukhaariy na Muslim.

 

Bila ya shaka yoyote, anayehitaji Pepo, yabidi kujidhalilisha na kujifanya dhaifu mbele ya Subhaanah. Na katu tusifikirie kujitakabari, kwani Kibri ni Chake Mkubwa wa Wakubwa na malipo ya kuwa na kibri ni Moto tu. Hivyo, tujitayarishe kwa kujipinda ili nasi tupate kuwa miongoni mwa hao wachache watakaoingia Peponi In Shaa Allaah

 

 

Share