Tanzania Bara Na Matumizi Ya Shariy'ah Za Kiislamu

Imetayarishwa na:

Naaswir Haamid

 

MUHTASARI

Sifa zote njema ni zake Allaah (Subhanahu wa Taala), Muumbaji wa vilivyo dhahir na vilivyofichikana, Bwana wa Ulimwengu. Rehma na Amani ziwe juu ya kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) ambaye ameletwa kwetu kuwa ni Rehma kwa ulimwengu. Nashuhudia kwamba ameufikisha kwa ulimwengu ujumbe sahihi na muongozo wa haki kutoka kwa Allaah (Subhanahu wa Taala).

 

 

 

 

 

Makala hii imegawika sehemu nne. Sehemu ya kwanza ni utangulizi wa matumizi ya Sheria za Kiislamu

 

 

Tanzania

Bara. Sehemu ya pili inahusika na matumizi ya Sheria za Kiislamu kwenye kipengele pekee cha ndoa za Kiislamu na masharti yake ili kusihi hiyo ndoa. Pia namna ya hiyo ndoa ya Kiislamu inavyohitalifiana na sheria za Tanzania Bara. Sehemu ya tatu inajadili vipengele vyengine vya sheria za Tanzania pamoja na uthibitisho wa kesi zilizowahi kutolewa maamuzi kwenye masuala ya jamii ya Kiislamu. Sehemu ya nne na ya mwisho, inajumuishwa kwa mawazo ya muandishi kuhusiana na namna ya Shariy'ah ya Kiislamu inavyonyongwa na lipi lifanyike ili kuokoa jamii ya Waislamu Tanzania Bara. Sehemu hii inapatikana mwisho kwa jina la hitimisho.

 

 

 

 

 

SEHEMU YA

 

 

KWANZA

 

 

 

 

 

 

 

 

 

UTANGULIZI

 

 

 

 

 

 

 

 

Jamhuri ya Muungano ya

 

 

Tanzania

inajulikana wazi kuwa ni taifa lisilofungamana na dini, ni kwamba dini zote zina hadhi na nguvu sawa ndani ya Jamhuri ya Tanzania. Hivyo, Uislamu ni miongoni mwa dini kadhaa zilizomo Tanzania.

 

 

 

 

 

Tanzania chini ya Katiba yake imetangaza uhuru wa mawazo au dhamiri, itikadi au imani ikijumuisha uhuru wa kubadili dini au itikadi. Uhuru wa mtu kuamini dini au imani atakayo umetawazwa chini ya Kifungu namba 19 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya

 

 

Tanzania

ambacho kinaeleza kama ifuatavyo:

 

 

 

 

 

“(1) Kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, wa imani na wa uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa kubadilisha dini au imani yake.

 

 

 

 

(2) Bila ya kuathiri sheria zinazohusika za Jamhuri ya Muungano, kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kuendeleza dini itakuwa huru na jambo la hiari ya mtu binafsi; na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za Mamlaka ya Nchi.

 

 

 

 

(3) Kila palipotajwa neno “dini” katika kifungu hiki ifahamike maana yake ni pamoja na madhehebu ya dini, na maneno mengineyo yanayofanana au kuambatana na neno

 

hilo nayo yatatafsiriwa kwa maana hiyo.”

 

Matokeo ya Kifungu hicho hapo juu ni kuwa Katiba ya

 

 

Tanzania

inaigawa dini kwenye mafungu mawili ambayo inazifanya dini zote ukiwemo Uislamu kuwa na hadhi tasa (negative status) kwa kueleza kuwa Serikali haina mkono wake katika shughuli za dini. Wajibu wa Serikali ni kuitetea haki hii inapotokezea uvunjwaji wake wa kuabudu. Kwa upande mwengine, dini zote zinatambuliwa kuwa na hadhi sanya (positive status) kutokana na kuwapatia wananchi haki ya kuitangaza na kuimarisha maslahi ya dini ndani ya taifa lisilofungamana na dini kwa kufuata sheria na kanuni za usawa.

 

 

 

 

 

Ingawa Kifungu cha 19 kinaifunga Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kuingilia itikadi za dini, lakini

 

 

Tanzania

hii isofungamana na dini yoyote imetoa ruhusa ya kupitishwa sheria zenye kuathiri imani na matendo ya wanaumini hasa wa Kiislamu. Kwani Uislamu sio tu kuingia msikitini na kuswali; ni mwenendo mzima wa maisha kuanzia kuzaliwa hadi kufa kwake. Uislamu ni mfumo kamili wa kuishi unaozingatia mafundisho ya dini.

 

 

 

 

 

Tunashuhudia Tanzania Bara kurithi baadhi ya sheria za Uingereza, kwa mfano Sheria ya Usimamizi wa Mali zilizo Hafifu, sura ya 30 (The Administration of Small Estate chapter 30) inayompa mzigo mzito maiti kurithiwa kwa Sheria za Kiislamu pale tu atakapotangaza (kabla ya kufa) kwa mazungumzo au maandishi. Ikiwa hakueleza nia ya kurithiwa kwa Sheria za Kiislamu basi atarithiwa kwa sheria za nchi.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Matumizi ya Sheria za Kiislamu Tanzania Bara zimetengwa kwenye mambo ya jamii tu kama ndoa, talaka, mirathi na matunzo ya watoto. Sheria zilizorithiwa kutoka kwa Muingereza ( kwa mfano Judicature of Application of Law Ordinance 1961-JALO na Tanganyika Order in Council) zinaruhusu matumizi ya Sheria za Kiislamu kwenye vipengele vilivyotajwa hapo juu. Pia Mahkama ya Mwanzo (Primary Court) ndizo zenye ruhusa ya kusikiliza madai haya ya Waislamu[1]. Sheria ya Tanzania haijaweka kanuni ya Hakimu katika Mahkama ya Mwanzo shurti ya kuwa Muislamu. Hivyo kwa sheria ya Tanzania madai ya wanandoa wa Kiislamu yanaruhusiwa hata kusikilizwa na Hakimu asiyekuwa Muislamu (Magistrate’s Courts Act of 1984).

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Mpaka hapa tu, utakuwa umetambuwa kuwa Tanzania Bara haina Mahkama maalum ya kusikiliza madai ya Waislam kwa jina la “Mahkama ya Kadhi” ambapo Mahkama hii ipo Kenya, Uganda na Zanzibar. Tanzania Bara wanatumia Mahkama ya Mwanzo ambayo inatumika kusikilizia sio tu madai ya Waislamu bali kwa makabila na itikadi nyengine zote. Pia Mahkama ya Mwanzo ina uwezo wa kusikiliza kesi za madai na jinai kwa sheria za nchi.

 

 

 

 

 

 

 

 

Ni ukweli usiofichika kuwa Mahkama ya mwanzo inawaathiri sana Waislamu kwani haina Mahakimu wa Kiislamu wenye elimu ya Sheria za Kiislamu.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Tunatambuwa pia kuwa Sheria za Kiislamu haitumiki katika nyanja zote za madai na jinai kwa sababu Tanzania imejitawaza kuwa taifa lisilofungamana na dini, hali ya kuwa bado Tanzania inaingilia uhuru wa kuabudu na kuzuia Waislamu kufuata maamrisho ya Sheria za Kiislamu.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Mwaka 1971, matumizi ya Sheria za Kiislamu yalibanwa rasmi kwenye masuala ya ndoa, talaka na mahari. Ili kuwa na nguvu kisheria juu ya masuala hayo, ikapitishwa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 (Law of Marriage Act 1971) ambayo sio mahsusi tu kwa Waislamu bali kwa wananchi wote wa Tanzania bila ya kujali tofauti za dini au imani. Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 (SNM 1971) inazingatia masuala ya ndoa, talaka na mahari kwa muongozo wa taratibu na ushahidi uliokuwa ukitumika zama za Muingereza. SNM 1971 inaweka uwiano wa kisheria kwenye masuala ya ndoa na talaka. Pia sheria hii inatumika sawa sawa kwa Waislamu wote bila ya kujali madhehebu, imani au jinsia.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

SEHEMU YA PILI

 

 

 

 

 

 

 

 

 

KANUNI ZA NDOA YA KIISLAMU

 

 

 

 

 

 

 

 

Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 (SNM 1971) kwa uwazi kabisa inatangaza kuzitambua ndoa za Waislamu na zile za wake zaidi ya mmoja. SNM 1971 haikufafanua taratibu sahihi za Kiislamu za kuikamilisha hiyo ndoa. Mfano mahari, akdi, posa n. k.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kuna mgongano wa umri wa mtu kuoa baina ya SNM 1971 na Shariy'ah ya Kiislamu kwani SNM 1971 inatangaza kuwa umri wa kuoa ni miaka 18 na kuolewa ni miaka 15. Kwa taratibu za Kiislamu, mtoto wa kike/kiume akishafikia balegh tu anaweza kuingia kwenye ndoa. Hii ina maana ya kusema kuwa msichana akianza kutokwa na damu ya hedhi akiwa na umri wa miaka 12 hawezi kuolewa kwa vipengele vya SNM 1971 ingawa kwa Shariy'ah ya Kiislamu anaruhusika.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kitu chengine muhimu kwa ndoa kutambulika chini ya SNM 1971 ni kuwepo cheti cha ndoa kama ni ushahidi wa ndoa. Cheti hicho cha ndoa ni lazima kiwe kimesainiwa na kadhi, wanandoa na mashahidi wawili. Ingawa kwa Shariy'ah ya Kiislamu cheti cha ndoa au hata cha talaka sio lazima mpaka kufikia kiwango cha kutoitambua ndoa kama isemavyo SNM 1971.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

SEHEMU YA TATU.

 

 

 

 

 

 

 

 

Katika sehemu hii, tutajadili namna Shariy'ah ya Kiislamu inavyotumiwa Tanzania Bara kwenye vipengele vifuatavyo:

 

 

 

 

1.    Talaka

 

 

 

 

2.    Matunzo ya watoto

 

 

 

 

3.    Mirathi

 

 

 

 

4.    Kuitanguliza ndoa

 

 

 

 

5.    Kuukana Uislamu (kurtadi)

 

 

 

 

6.    Ugawaji wa mali

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

1-TALAKA

 

 

 

 

Pale ambapo SNM 1971 imetoa maelezo kuhusu ndoa na talaka, Shariy'ah ya Kiislamu haitotumika. Matokeo yake SNM 1971 imeweka sababu maalum za kuitoa talaka na kuifanya ile kauli ya “talaka” kukosa nguvu ya kuivunja ndoa. SNM 1971 inaweka njia mbili za kuivunja ndoa ambazo ni kifo na amri ya Mahkama. Pia ili talaka ipatikane kutoka Mahkama kwa hao wanandoa wa Kiislamu, ni lazima sharti tatu muhimu zitimizwe kabla ya hao wanandoa kuomba hiyo talaka. Kifungu namba 107 (2) cha SNM 1971 kinaeleza:

 

 

 

 

 

 

 

 

1-     Pande zote mbili wawe wamefunga ndoa kwa taratibu za Kiislamu.

 

 

 

 

2-     Wanandoa hao wamefikisha bila ya mafanikio ya kupatikana suluhu kwenye Baraza la kusuluhisha ndoa na baraza hilo liwe limeshindwa kusuluhisha.

 

 

 

 

3-     Pande yoyote iwe imefanya ‘jambo’ au ‘kitu’ kinachoweza kuivunja ndoa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Katika kesi ya Rattansi Vs Rattansi[2] wanandoa walitimiza masharti mawili ya mwanzo, nayo ni (a) wamefunga ndoa kwa mujibu wa Shariy'ah ya Kiislamu na (b) wameshindwa kupata suluhu mbele ya Baraza la kusuluhisha ndoa. Lakini hamna yeyote kati ya wanandoa hawa aliyefanya jambo au kitu kinachoweza kuivunja ndoa. Kwa mujibu wa SNM 1971 inatambua uzinzi, matatizo ya unyumba, maradhi, uwenda wazimu, ukatili, kifungo cha jela kuwa ni mambo yanayoweza kuivunja ndoa. Lakini lile tamko la ‘talaka’ sio shurti na kwa njia yoyote haiwezi kuivunja ndoa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kwenye kesi nyengine ya AbdAllaah Saidi Vs Manamkuu Yussuf[3] ambapo mume alitamka talaka tatu wakati mmoja kabla ya kufika kwenye Baraza la kusuluhisha ndoa. Kaimu Jaji Samatta alieleza kuwa Mahkama ina nguvu ya kutoa talaka pale ambapo inapokubalika kuwa ndoa imevunjika (kama uzinzi, matatizo ya unyumba n. k)

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hivyo, chini ya SNM 1971 ‘talaka’ haitambuliwi kuwa ni ‘kitu’ au ‘jambo’ ki/linachovunja ndoa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Zipo baadhi ya sababu za kuitoa talaka zinazoingiliana chini ya SNM 1971 na Shariy'ah ya Kiislamu. Lakini ushahidi wake unagongana na ule ulioelezwa kwa Shariy'ah ya Kiislamu. “Khula” ni miongoni mwa hizo, ambapo mke anamlipa mume kupatiwa talaka. SNM 1971 haitambui “Khula” kama ilivyohukumiwa kwenye kesi ya Aisha Chambala Vs Muhamadi Nyaseba[4] ambapo mke alifungua kesi ya kuomba talaka kwa hoja ya yeye mke kushindwa kuishi na mumewe kutokana na kukosekana matunzo. Mahkama haikuyapa nguvu yoyote hoja hiyo kwani katika kesi hii hakuna ‘jambo’ au ‘kitu’ kinachoweza kuivunja ndoa hiyo. Kwa mujibu wa Shariy'ah ya Kiislamu, mke anaweza kujiengua katika ndoa ikiwa ni kwa mapenzi ya mke kuomba talaka kwa shurti ya kurejesha mahari aliyopewa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Jambo la kushtuwa kwa Mahkama hizi kuwa hazitumii ushahidi wowote bali kujipweteka kwa kujitosheleza na sababu tatu (Kifungu 107 (2) SNM 1971). Juu ya hivyo, inaonesha wazi kuwa Mahkama hazitaki kufuata matakwa ya Waislamu. Kwani zinapotimizwa shurti hizo, Mahkama hizi hizi hudai kukimbilia ushahidi.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Katika kesi ya Ashura Salim Vs Ali Said[5] ambapo mke alifungua madai ya talaka kutokana na ukatili, lakini Mahkama ya Mwanzo ilikataa kutoa talaka kwa hoja ya kukosekana ushahidi.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kwenye kesi ya Halima Athumani Vs Maulidi Hamisi[6] mkata rufaa (Bi Halima) alifungua madai ya talaka kwa hoja ya ukatili kutoka kwa mumewe. Hoja ya msingi iliyowekwa na Mahkama ni kuwa upo uhalali wa Baraza lisilo la Kiislamu kusuluhisha ndoa na kukataa kuwapatia talaka wanandoa wa Kiislamu? Kwani Mahkama ya Wilaya ilikataa kuwapatia talaka kwa hoja hiyo juu. Uamuzi huu wa Mahkama ya Wilaya ulipingwa na Mahkama Kuu kwani ‘sababu tu’ ya Baraza kutokuwa la Kiislamu haiwezi kulifanya Baraza kuwa batili.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kwa maoni ya Mheshimiwa Jaji kuwa mke anaweza kufungua madai ya talaka kwa njia ya ‘khul’ na mume anaweza akatumia ‘talaqa’ kufungua madai ya talaka. Kwani kwa maelezo ya Mheshimiwa Jaji, Waislamu hawaendi Mahkamani kuomba kupatiwa talaka ila wanaenda kupatiwa maombi ya kusajiliwa hiyo talaka yao. Maoni ya Mheshimiwa Jaji ni sahihi lakini kwa mujibu wa SNM 1971 kifungu 107 (1) na (2) ‘khul’ wala ‘talaqa’ hazina nguvu yoyote.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

2-MATUNZO YA WATOTO.

 

 

 

 

SNM 1971 chini ya kifungu namba 123 inaipa nguvu kwa upande fulani hoja ya Kiislamu kuwa mtoto (wa kiume/kike) aliye chini ya umri wa miaka 7 awe kwa mama. Kwa mujibu wa Shariy'ah ya Kiislamu mtoto wa kiume aliyetimiza umri wa miaka 7 anaweza kuishi kwa baba na mtoto wa kike hana ruhusa ya kuondoka chini ya mikono ya mama hadi aingie balegh.

 

 

 

 

 

 

 

 

Kuna hatua nne zilizoelezwa ndani ya SNM 1971 ambazo lazima ziangaliwe ili kutoa matunzo ya mtoto ama kwa baba au mama:

 

 

 

 

i-                    Usitawi wa mtoto (mfano mali, mazingira, elimu, malezi n. k)

 

 

 

 

ii-                  Maelezo ya wazee.

 

 

 

 

iii-                 Maelezo ya mtoto yataangaliwa ikiwa anaweza kujieleza.

 

 

 

 

iv-                Sheria za mila na utamaduni.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hivyo, usitawi wa mtoto unapewa kipaumbele kama ilivyotolewa hukumu kwenye kesi ya Zainab Pothoo[7] ambapo iliamuliwa kuwa hamna mtu yeyote mwenye haki zozote dhidi ya mtoto. Kinachoangaliwa zaidi ni usitawi wa mtoto na wala sio Shariy'ah ya Kiislamu. Kwa mujibu wa hukumu hii, ikiwa Mahakama zote zitaangalia tu usitawi wa mtoto basi upo uwezekano wa mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa kukosa malezi ya mama mzazi au mtoto kupatiwa matunzo na mzee (baba/mama) aliyekuwa si muislamu. Ilimuradi tu kuna maslahi ya fedha kwa mmoja wa hao wazee, haingaliwi dini wala Shariy'ah ya Kiislamu. Pia inaweza kumfanya baba mzazi kutengwa na mwanawe halali na kupatiwa mama wa kambo. Matokeo yake kwenye kesi ya Asya Amir Vs Ahmed David[8] mtoto alizaliwa nje ya ndoa baadaye wazee wakafunga ndoa. Mahkama Kuu ikajilazimisha kumtambua mtoto amezaliwa ndani ya ndoa na hivyo ni mtoto halali. Akapatiwa mume matunzo ya mtoto ambapo kwa mujibu wa Shariy'ah ya Kiislamu ni kosa kwani ni mama pekee mwenye matunzo ya mwana aliye haramu.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Katika kesi nyengine ya Saada Muyoyo Vs Hussein Ally[9] baba mtu alikuwa sio baba halisi wa mtoto Khamisa lakini akafungua madai ya matunzo ya wote kwa mtoto Khamisa na mtoto Pili. Mahkama ya Mwanzo ilimpa matunzo kwa Pili na Khamisa. Lakini Mahkama Kuu ikaeleza kuwa kwa vile ustawi wa mtoto unaangaliwa zaidi, na kwa vile watoto hao wa kike wapo kwenye umri wa utoto ni bora wawe kwa mama hadi kufikia umri wa kwenda shule. Kosa lililopo kwenye uamuzi huu (ingawa baba mzazi aliomba hilo, lakini ombi lililokuwa batili haliwezi kukubaliwa) ni baba kutozwa nguvu kutoa malipo kwa ajili ya matunzo ya watoto wote wawili, hata kwa Khamisa ambaye si mwanawe halisi.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

3. 1  MIRATHI

 

 

 

 

Sheria za Tanzania Bara hazielezi ni sheria gani itumike pale ambapo aliyefariki alifuata mila pamoja na Shariy'ah ya Kiislamu. Lakini nguvu zaidi inapelekwa kutumika sheria za kikabila kuliko Shariy'ah ya Kiislamu.

 

 

 

 

 

 

 

 

Sheria ya Usimamizi wa Mali zilizo Hafifu (The Administration of Small Estate Ordinance) inaamrisha kuwa masuala ya mirathi kwa pande zote mbili ambazo ni waislamu, itumike Shariy'ah ya Kiislamu. Lakini Sheria ya Usimamizi wa Mali zilizo Hafifu haielezi namna ya kuigawanya hiyo mali ya mirathi. Kwa mujibu wa Uislamu, kuna sheria maalum ya mirathi inayotoka moja kwa moja kwa Allaah (Qurani)[10] ambayo ndio msingi mkuu wa Shariy'ah ya Kiislamu. Hivyo sheria na kanuni za mirathi kwa waislamu zipo na hatuna haja wala hapana uwezo kwa yeyote kuwatengenezea Waislamu sheria zilizokuwa nje ya maamrisho ya Muumba.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Chini ya Uislamu, mirathi inakwenda moja kwa moja kwa warithi chini ya utaratibu uliopangwa. Haijapewa nguvu Mahkama isokuwa ya Kiislamu kugawanya mali hiyo. Sheria ya Usimamizi ya Mali zilizo Hafifu (The Administration of Small Estate Ordinance) inatambuwa kuigawanya mali kwa njia za Kiislamu pale tu ambapo Aliyefariki ameeleza kwa maneno au maandishi kurithiwa kwa taratibu za Kiislamu. Shariy'ah ya Kiislamu zinaeleza kuwa ni thuluthi 1/3 tu ya mali anayoweza kuiandikia wasia[11]. Hivyo, 2/3 inatakiwa iwe kwa warithi, mgao au zawadi ya mali kwa yeyote nje ya sheria ya mirathi isizidi thuluthi.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Masuala ya jamii ya Waislamu nchini Tanzania yamefanywa kuwa na uhusiano wa sheria za nchi na sio Quran au Sunnah. Vivyo hivyo kwa Mahkama kufuata sheria za nchi tu. Matokeo yake, hata wasia ukitolewa mbele ya Mahkama, utahukumiwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.  Ikumbukwe kwamba Katiba hiyo hiyo inakaa kuingilia masuala ya dini.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Wakati huo huo, Shariy'ah ya Kiislamu zinakataa kuandikia wasia kwa mtu yeyote. Mfano wasia kwa asokuwa Muislamu au kwa atayakayemrithi n. k. Anaweza kwa mapenzi yake Aliyefariki kutoa mali yake kama zawadi lakini kwa kiwango kisichozidi thuluthi (1/3) ya mali yake. Matumizi ya Shariy'ah ya Kiislamu kwenye Mahkama za Tanzania unaonesha wazi kuingilia kanuni za Shariy'ah ya Kiislamu. Kwenye kesi ya Anwar Z. Mohammed Vs Saidi Selemani Masuka[12] ambapo Mahkama ya Rufaa ilitumia Ijtihad[13]. Hata wakili wa Mkataa Rufaa Muheshimiwa Korosso alishauri Mahkama kutoitambua Shariy'ah ya Kiislamu kwani inakwenda kinyume na Katiba inayoeleza kuwa mtu yeyote ana haki ya kumiliki na kugawa mali (wasia zaidi ya thuluthi) kwa namna apendavyo.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Katika kesi hiyo ya Anwar dhidi ya Saidi, aliyefariki alikuwa ni mwanamke aliyeolewa na Bw. Saidi. Aliyefariki aliandika wasia wa mali yake yote kwa mumewe Bw. Saidi akimwacha mwanawe wa kumzaa ndugu Anwar bila ya urithi wowote.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Ndugu Anwar alikuwa mtoto wa Aliyefariki lakini kwa mume mwengine. Tutambue kuwa, wasia zaidi ya thuluthi ndani ya Uislamu ni fasikh.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kutokana na wasia huo, Anwar hakuweza kumrithi mama yake kinyume na mafundisho ya Shariy'ah ya Kiislamu kwani Anwar anaweza kumrithi mama yake hata bila ya wasia. Mahkama za chini zote zilimkatalia Anwar haki ya kurithi. Mwishowe, Mahkama ya Rufaa kupitia kwa Mheshimiwa Ramadhani, J. A ikatengua uamuzi wa Mahkama Kuu na kumruhusu Anwar kurithi. Hivyo matumizi ya sheria za Tanzania na matumizi ya haki za lazima ‘fundamental rights’ bado yanahitaji kufafanuliwa barabara katika kutunga sheria zisizofungamana na dini.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

3. 2 MIRATHI KWA WASOKUWA WAISLAMU.

 

 

 

 

Kabla ya kuchambua kipengele hichi, ieleweke kuwa Uislamu umeweka vizingiti na kuruhusu yenye manufaa kwa binaadamu wenyewe. Shariy'ah ya Kiislamu haina lengo la kumnufaisha jasho, damu, nguvu n. k. ya Muislamu istarehewe na kudhalilishwa mbele ya wasokuwa waislamu. Hivyo Shariy'ah ya Kiislamu imeweka kizuizi kwa asokuwa Muislamu kumrithi Muislamu ili kuupa nguvu Uislamu kwa kuiachia mali iendelee kwa kizazi kilicho cha Kiislamu. Shariy'ah ya Kiislamu inaeleza kuwa itakapotokezea mrithi kuwa si Muislamu hataruhusika kumrithi Aliyefariki hata akiwa ni ndugu wa karibu. Lengo kuu la kuweka kizuizi hichi ni kuimarisha dola/jamii ya Kiislamu.

 

 

 

 

 

 

 

 

Uamuzi wa Mahkama za Tanzania unaonesha kuwa mahusiano baina ya warithi na aliyefariki yanaangaliwa zaidi kwenye ndoa na uzazi. Hivyo, sifa ya mrithi kuwa ni Muislamu iliondolewa kama ilivyohukumiwa katika kesi ya Shambaa Juma na wengine Vs Rashid Juma[14] Maelezo ya kesi hii ni kwamba ikiwa dini itatumika kuwa ni kigezo cha mirathi, hata asohusika (alimuradi ni Muislamu tu) anaweza kudai mirathi kwa hoja ya dini. Kwa ufafanuzi ni kuwa Uislamu unatambua kuwa waumini wote ni ndugu, lakini udugu unaozungumzwa hapa sio ule wa kurithi. Kwa hivyo sio hoja ya dini pekee kuruhusu Muislamu kumrithi Muislamu mwenziwe. Bali ni lazima uwepo pia uhusiano wa damu au ndoa. Ni wazi kuwa Uislamu umekataza mirathi ya Muislamu ambaye amebadili dini au yule alokuwa na uwezo wa kumrithi (kwa mfano mke, ndugu, baba n. k) lakini akawa nje ya Uislamu. Hawa ndio makusudio ya Shariy'ah ya Kiislamu. Hivyo, hukumu hiyo ni mbaya kwa Waislamu kwani kigezo cha dini kwa Uislamu kinaangaliwa sawa sawa na kigezo kuhusu chanzo cha uzazi na ndoa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Msingi wa haki ya mirathi haukumalizia hapo kwenye kesi hiyo bali hata kwenye kesi ya Re Salum Omar Mkeremi[15] ambapo mjane asokuwa Muislamu aliruhusiwa kumrithi mumewe alimuradi tu ilikuwapo ndoa. Kwa Shariy'ah ya Kiislamu, ndoa baina ya mke wa Kiislamu na mume asokuwa Muislamu haikubaliki. Pia mhusika asokuwa Muislamu hawezi kumrithi Muislamu kwa namna yoyote itakayokuwa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kwenye kesi nyengine ya Jumanne Selemani Vs Catherine Sindano[16] mjane asokuwa Muislamu na asokuwa na mtoto alipewa nusu ya mirathi wakati Shariy'ah ya Kiislamu inaeleza kuwa mjane asokuwa na mtoto anarithi ¼ ya mirathi haikutumika. Kwa mujibu wa Sheria za Kiislamu, bi Catherine si Muislamu na hivyo haruhusiki kumrithi Muislamu kwa namna yoyote. Ni kusema kuwa Mahkama za Tanzania zinafuata matakwa ya kuibeza Shariy'ah ya Kiislamu sio kuisimamisha.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

3. 3 HAKI ZA WAJANE WA KIISLAMU KATIKA MIRATHI.

 

 

 

 

Nguzo ya haki na usawa kwenye jinsia imedhaminiwa ndani ya Katiba kifungu namba 12 inayozungumza kama ifuatavyo:

 

 

 

 

 

 

 

 

“(1) Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wo wote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.

 

 

 

 

(2) Hakuna sheria itakayokuwa na kifungu chochote ambacho ni cha ubaguzi wa moja kwa moja au kwa taathira yake.

 

 

 

 

(3) Haki za raia, wajibu wa maslahi ya kila mtu yatalindwa na kuamuliwa na mahakama pamoja na vyombo vya nchi na vinginevyo vilivyowekwa na sheria.”

 

 

 

 

 

Dunia imejikubalisha kuelewa kuwa Qurani inamnyima mwanamke mirathi sawa ya ile ya mwanamume na hivyo kuonekana kuwa Qurani ina ubaguzi (AstaghfiruAllaah). Ni wazi kabisa kifungu hichi cha Katiba kinateka nyara Sheria za Muislamu wa kike kurithi nusu ya kile anachorithi ndugu yake wa kiume. Sheria za Kiislamu pia zinabezwa kwa kumpa mjane asokuwa na mtoto ¼ ya urithi wa mume na 1/8 akiwa na watoto.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kidogo tu nichambue hapa kuwa mwanamke ndani ya Uislamu hajazuiliwa kupatiwa zawadi ya mali ila ameshurutishwa mwanamme kumpatia makazi, kivazi, chakula kwa mujibu wa sheria. Mahari anatoa mume kumpa mke hata iwe ni dola milioni moja na bado vyote hivi vinakuwa kwa mke mali yake isogawanywa na mume. Ingawa mume cha kwake ni nusu bin nusu kwa mke.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Dunia inangalia kipengele cha mirathi tu ndani ya Uislamu kuwa na ubaguzi! Wanawake mpaka wa Kiislamu waliokosa elimu na ufahamu sahihi wanafuata mdundiko wa Magharibi bila ya kutafuta ukweli. Kama wanawake ni wenye akili wadai wanaume kufuata hiyo Shariy'ah ya Kiislamu. Kwani Uislamu unamuamrisha mume kukaa na mke sio kumtelekeza, kumpa mahari sio kumlaghai, kumpa matunzo sio kumuuza. WAllaahi naapa kwa Yule Anayemiliki nafsi yangu, hamna matunzo bora na ya ufakhari kwa mwanamke zaidi ya Sheria za Kiislamu. Kama hazifuatwi hizo Sheria, ni wajibu mwanamke kuzipigania na sio kuzipinga. Aidha kama dola zinataka haki basi siteo nguvu kutekeleza Shariy'ah ya Kiislamu, angalau hizi za familia na mirathi.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Juu ya hayo, Mahkama ya Tanzania Bara zinatumia mila na Shariy'ah ya Kiislamu kutambua haki za mirathi. Kwa upande mwengine wa kesi ya ReSalum, hoja kuu kwenye kesi hii ni sheria gani itumike baina ya Shariy'ah ya Kiislamu au sheria za kikabila za Wahehe.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Mwisho, Shariy'ah ya Kiislamu ikachukua mkondo wake kwa aliyefariki kurithiwa kwa mujibu wa Shariy'ah ya Kiislamu. Lakini tuelewe kuwa ilikuwa ni hatua ya upendeleo kwani kwa Kabila la Wahehe, mjane angeweza kuzuiwa haki ya kurithi mali. Kwa maana hiyo Uislamu ndiyo wenye kutoa haki kwa wanawake.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hivyo, daima Mahkama zinaangalia manufaa na sio kusimamisha Shariy'ah ya Kiislamu kama Quran na Sunnah inavyofafanua. Panapoonekana kufuatwa hiyo Shariy'ah ya Kiislamu basi kuna uwezekano mkubwa wa kumpendelea mwanamke au inatumika pale kwa maslahi ya fulani tu.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kwa wakati tulio nao sasa, Mahkama ziweweka alama za kuangalia kwa kesi ambazo zina mgongano wa sheria. Nazo ni; ikitokezea kuwa na mzozo wa madai juu ya mirathi ya Muislamu ambaye pia akifuata mila za kabila analotokea. Katika hili Mahakama inaweza kufuata alama zifuatazo:

 

 

 

 

1-     Desturi ya maisha: Inaangalia namna aliyefariki alivyokuwa akiishi ndani ya  jamii ambayo inafuata kanuni za kabila husika.

 

 

 

 

2-     Nia ya aliyefariki: Mazungumzo na wasia unatazamwa ili kuonesha azma yake kutumika kanuni za Shariy'ah ya Kiislamu au kabila.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

4-KUITANGULIZA NDOA

 

 

 

 

 

 

 

 

Hii ni aina ya ndoa zinazobarikiwa ndani ya Tanzania. Watu wanaoishi kinyumba na kupata watoto bila ya kufunga ndoa rasmi wakiwa wamedumu katika maingiliano hayo kwa muda wa zaidi ya miaka miwili basi hutafsiriwa ni ndoa. Kifungu namba 160 SNM 1971 kinatangaza kuwa mwanamke anayekaa kinyumba na mwanamme kwa muda wa zaidi ya miaka miwili wanatambuliwa kuwa na hadhi ya ndoa, pia watoto waliozaliwa au   watakaozaliwa watatambuliwa kuwa ni wa ndani ya ndoa na hivyo ni halali.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Ndoa zina nguvu na shurti maalum ndani ya Uislamu. Ikiwa wahusika watakaa kinyumba na kuishi pamoja na kupata watoto bila ya kufunga ndoa ya Kisheria za Kiislamu kwa miaka yoyote watakayokaa kinyumba ni kwenda kinyume na maamrisho ya dini, hiyo ni haramu na wanatenda dhambi kubwa yenye hukumu iliyosawa na uzinifu.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Ni kosa kubwa kuitafsiri kwa uwongo Shariy'ah ya Kiislamu kutoka kwa Majaji kadhaa wa Tanzania Bara na kutangaza kuwa madhehebu takriban yote ya Uislamu yanaikubali dhana ya kuitanguliza ndoa. Waislamu wanafuata mwendo huu batili hawana hoja ya Kiislam, hawa ni waasi. Wanachofanya ni kuingiza sheria za mila ndani ya Uislamu. Sheria za Kiislamu hazihitaji nyongeza kutoka kwetu.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hukumu hii imetolewa kwenye kesi ya Habibu Rahman Chowdhury[17] Mheshimiwa Bw. Peter alieleza kuwa Uislamu unaruhusu kuidhinisha na kuikubali ndoa kuwa halali katika mazingira ambayo hakukuwepo sherehe ya arusi lakini ushahidi kuonesha kuwa wahusika walikusudia kufunga ndoa na kuishi katika ndoa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hivyo, kwa maoni ya Jaji Peter, hakuna haja ya kuitangaza/kuisherehekea arusi bali nia ndio inayoangaliwa. Kinyume na mafundisho ya Uislamu ambapo nia tu kwenye ndoa haikubaliki bali itangazwe na kushuhudiwa kwa mujibu wa shurti za dini ya Kiislamu.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Katika kesi nyengine ya Pazi Vs Khamis[18] Jaji mhusika alitumia baraka za kesi ya Chowdhury. Hivyo maisha ya kinyumba pekee yalikubalika kuwa ni ndoa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Suala la kujiuliza, ni nani alijua nia ya hao watu kama kuoana? Kwanini mtu aingie kwenye gharibu wakati jambo la dhahiri lipo? Ndoa ina sheria zake, maadam hazikusimama kuifunga ndoa, basi hapo hapana ndoa. Ndoa ni aina ya mkataba ambao umewekewa sheria maalum. Bila ya kufunga huo mkataba na kufuata taratibu za sheria basi hamna ndoa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

5- KUUKANA UISLAMU (kurtadi)

 

 

 

 

Kwenye sehemu hii, hatutazungumzia tu kuhusu kubadili dini ya Uislamu kwa kuingia dini nyengine (kurtadi), bali tutajadili athari ya kurtadi katika kipengele cha kuhodhi (kumiliki) mali.

 

 

 

 

 

 

 

 

Uislamu una msimamo kuwa imani yake ya dini ndio sahihi na imani ilokuwa nje ya mwenendo wa Uislamu kwa maamrisho ya Quran na Sunnah sio sahihi na haukubaliki kwa maisha ya mwanaadamu yoyote.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hivyo, Muislamu yeyote atakayebadili mwenendo sahihi na kuanza kuupiga vita Uislamu na Waislamu kwa kejeli, dharau na propaganda n. k (Mfano mzuri rudia kadhia ya Salman Rushdi) basi huyo amefanya kosa la jinai na adhabu itakuwa juu yake kwani ataleta chuki na fitna kubwa katika jamii ya Uislamu.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kwa sheria za Tanzania, mtu akitoka kwenye ukafiri na kuingia katika Uislamu, Sheria za Kiislamu hazitumiki juu yake.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Katika kesi ya Mtoro bin Mwamba Vs A. G [19] iliamuliwa kuwa Mkabila atakayebadili kuingia kwenye Uislamu hana haki ya kuhukumiwa kwa kutumia Sheria za Kiislamu.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Miongoni mwa sababu za kutoa talaka ndani ya Shariy'ah ya Kiislamu ni kurtadi, vivyo hivyo kwa SNM 1971. Ajabu kuwa kipengele hichi cha kurtadi hakitumiki kuzuia mirathi.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

6- UGAWAJI WA MALI

 

 

 

 

Mali za ndoa tunazojadili hapa ni zile baada ya kutolewa talaka. SNM 1971 inaeleza njia mbili muhimu zitumike kwa Mahakama kuigawa mali hiyo. Nazo ni:

 

 

 

i)                    Mali iwe ni nguvu sawa ya wanandoa (wote wawili).

 

 

 

 

ii)                   Mahakama iigawe sawa kwa wanandoa.

 

 

 

 

Hivyo, Mahakama itaangalia nguvu za mke na mume kwa kuigawanya mali sawa sawa. Utata mkubwa uliokuwapo hapa ni kuhusiana na nini kinachojumuisha kusemwa ‘nguvu sawa’ ambapo yalitafsiriwa katika kesi maarufu ya Bi Hawa Mohammed Vs Ally Sefu[20] uamuzi katika kesi hii ni kuwa kazi za ndani ya nyumba anazofanya mke zinamnasabu wa ‘nguvu sawa’ na zinachangia katika mali ya ndoa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kabla ya kuendelea mbele, kuna sababu za kutoigawa mali sawa sawa. SNM 1971 inaeleza:

 

 

 

 

(a)    Mila za wahusika zinaizuia Mahakama kuigawa mali kwa mujibu wa sheria za nchi. AU

 

 

 

 

(b)   Ikiwa mali ya ndoa haikupatikana kwa nguvu sawa baina ya wahusika. AU

 

 

 

 

(c)    Ikiwa baina ya mhusika anamdai mwenziwe fedha au mali yoyote yenye thamani. AU

 

 

 

 

(d)   Ustawi wa watoto pia utaangalia na ikiwa upo uwezekano wa kutoigawa mali sawa sawa baina ya mama au baba mzazi wa mtoto.

 

 

 

 

Kesi ya Bi Hawa inaangukia kizuizi (a) kwani kwa sheria ya Tanzania, Uislamu unaangukia hapa na kupewa hadhi sawa ya sheria za makabila. Shariy'ah ya Kiislamu inazuia mjane wa talaka kugaiwa mali ya ndoa aliyochuma mume. Hivyo, haiwezi Mahakama kuamua kuigawa mali ya ndoa sawa sawa kwa kigezo cha kazi afanyazo mke ndani ya nyumba. Jee haitoshi mume kupewa mzigo juu ya mke wa kumlisha, kumpa makaazi, kumvisha, kumpa matibabu na sio mke tu. Jukumu hili linakuwa juu ya baba hata kwa watoto wake. Mahakama inaweza isione hili, inaangalia mke na mali tu. Mali zake mke daima zitabakia kuwa za mke na mume hatakiwi kuzigusa kwa Shariy'ah ya Kiislamu. Katika sheria za Kiislamu akichumacho mke kinabaki ndani ya mikono yake wala hamna ruhusa ya kuigawa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Cha kushangaza SNM 1971 imeshurutisha mke mwenye uwezo kumtumikia mume kwa mavazi, chakula n. k pale ambapo mume hana uwezo. Sasa kuna waume walokimbilia Mahakamani kuidai haki hii? Ipo pambo tu kwa sababu achilia mbali jamii ya Waislamu, Jamii zote zaelewa jukumu la kuitumikia maisha ya ndoa ni juu ya mume.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Ni ukweli usiofichika, Shariy'ah ya Kiislamu inapigwa vita hata kwa vipengele vidogo tena vilivyo sawa kwa imani nyengine. Waislamu wana wajibu wa kuusimaimisha Uislamu kuanzia sheria ndogo mpaka kubwa. Kwani Qurani unaamrisha Muislamu aingie kwenye Uislamu mzima mzima. Sio nusu anafata, mengine kuyaacha. Mfano tu wa hijabu, Uislamu umeshurtisha wanawake wote sio kwa WachaMungu wa kike tu kama wafanyavyo imani nyengine za dini. Uislamu haumnufaishi mmoja na kumuacha mwengine.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hoja ya talaka kuathiri mali za ndoa inajadiliwa vizuri katika kesi ya Bibie Maulidi Vs Mohamed Ibrahim[21] ambapo wahusika walioana kwa Shariy'ah ya Kiislamu na kuachana kwa tamko la ‘talaka’ na kubarikiwa (kuruhusiwa) talaka hii mbele ya uamuzi wa Mahakama ya Mwanzo. Lakini kuhusu ugawaji wa mali ya ndoa, ikahitaji kuangalia ushahidi wa ubia (mchango) baina ya mume na mke. Hoja ya msingi katika kesi hii ilikuwa, jee upo uwezekano wa kazi za ndani ya nyumba kuwa ni ubia? Mahkama ilijikubalisha kuwa mke amefanya mchango katika mali ya ndoa na kutoa uamuzi wa kuigawanya sawa sawa. Katika rufaa ya Mahkama Kuu ilitupilia mbali hoja ya kazi za nyumbani kuwa ni mchango sawa kwani mke alipatiwa nyumba aliyojengewa kama ni zawadi kutoka kwa mumewe yenye thamani ya Tsh 40,000/-

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Uhakika ni kuwa uamuzi huo wa Mahkama ya Mwanzo ulikwenda kinyume na taratibu za Kiislamu ambapo Uislamu unatambuwa mali ya kila mhusika na zawadi baada ya kuachana.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Pia, mume alijenga nyumba hiyo kama ni zawadi na sio kwa lengo jengine. Ni kusema kuwa Mahkama Kuu haikuigawa mali hiyo kwa hoja ya ‘nguvu sawa’ na kuridhika Mahkama kwa nyumba aliyozawadiwa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

SEHEMU YA NNE

 

 

 

 

 

 

 

 

 

HITIMISHO

 

 

 

 

 

Kama tulivyopitia mawazo tofauti ya Majaji na Sheria za Tanzania, tumetambua kuwa Shariy'ah ya Kiislamu inawekwa pamoja na Sheria za Makabila. Kawaida ya makabila zina sheria kutokana na urithi na imani au itikadi. Tofauti na Uislamu kutumia Qurani ambayo inazaidi ya miaka 1400 kuwa ndio Katiba yao. Sasa Tanzania na Dunia kwa ujumla ituoneshe sheria yoyote inayotumika hadi leo yenye zaidi ya miaka mia moja tu ambayo haikuwahi kufanyiwa marekebisho yoyote. Ukweli kuwa hamna.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Uislamu unasheria zake maalum, kuziweka sheria hizi pamoja na zile za makabila ni kumfanya Allaah na Kitabu Chake kuwa na hadhi ya miungu ya kikabila.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Sababu hii ya kuichanganya Quran na Sunnah (Shariah) pamoja na makabila ndio chanzo cha kufanya Mahkama kujaribu (bila ya mafanikio) kuikosoa Shariy'ah ya Kiislamu. Yareti kama Tanzania Bara ingeliachia Waislamu kuhukumiana kwa sheria zao. Mahkama za Tanzania zisingefikia hatua ya kuikosoa Shariy'ah ya Kiislamu kama tulivyoona katika kesi tulizojadili.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Juu ya tofauti kubwa baina ya Shariy'ah ya Kiislamu na zile za makabila (baynal maghrib wal mashrik na bayna ssamaa’ wal ardh), bado zinajumuishwa pamoja kwa sheria za Tanzania kama SNM 1971, Sheria ya Usimamizi wa Mali Hafifu na Katiba yenyewe. Pia sheria za kurithi kutoka utawala wa Muingereza zimeathiri matumizi ya Shariy'ah ya Kiislamu nchini Tanzania.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Ni utambuzi wa wazi kuwa SNM 1971 inaitikia ule wimbo wa ‘Beijing’ kumpendelea mwanamke kwa madai ya haki na usawa kuimarisha na kukuza haki za wanawake kuliko kutoa uamuzi kwa haki. Kama tunavyoona SNM 1971 inaweka usawa wa talaka baina ya mume na mke wakati Uislamu umempa usimamizi wa talaka mwanamme. Hili ni jukumu kwa wanaume sio upendeleo. Ndani ya Uislamu hakuna kigezo cha kusema Imamu (aliye juu) kuwa ni bora kuliko maamuma. Wote ni sawa, ila kwenye jahazi lazima awepo kiongozi kwani nahodha wawili hawakai pamoja. Ndivyo kwa Uislamu kumteua mwanamme kuwa msimamizi wa masuala ya ndoa na ndio akapewa majukumu chungunzima kuanzia kutoa mahari, kugharamia makazi na mengineyo. Jee hatuoni huu mzigo alioubeba mume? Kama wa kusimama kutetea jinsia ndani ya Uislamu ni wanaume lakini katu hawatasimama kutetea dhulma kwani wamekubali jukumu hili kuwa lao.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Inaelekea lengo la kupitisha sheria kama ya SNM 1971 ni kumpa nguvu mwanamke iliyokuwa nje ya uwezo wake. Kwani kwa Tanzania kuiwekea sheria Uislamu ni kuitoa kasoro dini hii. Hii ni dini kamili na ndio maana haieleweki kwa wale wanaofuata dini au itikadi zenye kasoro chungu nzima. Hao hawaelewi falsafa ya Uislamu hadi pale watakapoondoa taka taka nyoyoni mwao. Nyoyo zilizojaa taka taka haziwezi kuiona haki.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Tumeshuhudia baadhi ya wanasheria wa Tanzania[22] kueleza kuwa miongoni mwa malengo ya kupitisha SNM 1971 ni kuwawezesha wanawake (haswa wa Kiislamu) kupatiwa talaka bila ya kutilia maanani vizingiti vya Shariy'ah ya Kiislamu.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Kama tunavyotambua kuwa Mahkama za Kadhi zipo Afrika ya Mashariki yote Kenya, Uganda na Zanzibar. Lakini bado mjadala wa Tanzania Bara kuwa na Mahkama yake ya Kadhi haujatatuliwa, ijapokuwa Kadhi sio tamko lililotakatifu kutoka Qurani Tukufu. Historia inaonesha kuwa ‘Kadhi’ ilianza kipindi cha utawala wa Ufalme wa Umayyad (Umayyad Dynasty) na kazi zake zilikuwa ni kusimamisha haki na kutoa ufafanuzi kwenye vipengele vya Shariy'ah ya Kiislamu. Kadhi waliwajibika kutumia Quran na Sunnah.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Ingawa sasa zipo jitihada zinazoonekana kufanyika kuanzisha Mahkama ya Kadhi Tanzania Bara, lakini huenda ikawa Mahkama ya Kadhi kuwa ni jina zuri nje lakini isiyo na maslahi kwa Waislamu kama ilivyo ofisi ya Mufti kwa Zanzibar. Hivyo, taratibu zifuatwe kuhakikisha Mahkama ya Kadhi itafanya uadilifu na lengo kuu liwe kuwawezesha Waislamu kufuata muongozo wao sahihi wa Quran na Sunnah kwa njia ya kusimamisha haki na kutoa ufafunuzi kwenye vipengele vya Shariy'ah ya Kiislamu.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Ieleweke na itambulike kuwa Waislamu wa Tanzania kutia nguvu kuanzishwa Mahkama ya Kadhi hauna lengo la kurudisha utawala wa Kiislam Tanzania Bara kwa kuanzisha dola ya Kiislamu. Waislamu wanadhamiria kuzikuza imani zilizokuwa hafifu na zinazokaribia kupotea kwa kuanzisha Mahkama maalum kwa Waislamu ambayo itasimamia masuala ya jamii ya Waislamu akili na waangalie mwenendo wa Mahakama ya Kadhi nchini Kenya, Uganda na Zanzibar. Mahakama hizo hazijaleta mitafaruku wala kulaumiwa kutotenda haki. Makosa ya kibinadamu hutokea, nayo hushughulikiwa kama taratibu za kisheria zilivyo

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

MAREJEO:

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

KATIBA YA JAMHURI YA TANZANIA 1984.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

SHERIA YA NDOA YA MWAKA 1971

 

 

 

 

 

 

 

 

 

ESSAYS ON LAW AND SOCIETY by Legal Aid Committee, Faculty of Law, University of Dar-es-Salaam. MWAKA

 

 

 

 

 

 

 

 

 

WOMAN IN ISLAM, B. Aisha Lemu and Fatima Heern, Islamic Council of Europe 1978.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

THE SECULAR STATE AND THE STATE OF ISLAMIC LAW IN TANZANIA presented by Makaramba on 21st to 23rd of July 2000 at The Islamic Law in Africa Project (ILAP), University of Cape Town – South Africa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

THE STATUS AND APPLICATION OF ISLAMIC LAW IN TANZANIA by Robert V. Makaramba.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

CUTOMARY LAW OF TANZANIA, James, R. W and Fimbo, G. M

 

 

 

 

Website:

 

 

 

 

www.law.emory.edu/IF4region/eastcentralafrica.html

 

 

 

 

 

 

 


[1] Kifungu cha 18 (1) cha Sheria za Mahkama za Hakimu (The Magistrate Courts Act of 1984)

[2] (1971) TLR no. 55

[3] (1978) LRT no. 43

[4] Rudia makala ya Makaramba

[5] DSM H. C (P. C) matr. Civ App No. 39 of 1973 (unreported)

[6] H. C (1991) TLR pg. 79

[7] (1959) EA pg. 917

[8] (1968) HCD namba 206

[9] (1971) HCD namba 9

[10] Suratun-Nnisaa: 11

[11] Sayyidna Umar (RadhiyAllaahuAnhu) alitaka kuitowa ardhi yake yote kuwa waqfu, lakini Mtume (SwallAllaahuAlayhi Wasalaam) alimzuia.

[12] Rudia makala ya Makaramba

[13] Ijtihad ni maelezo binafsi ambayo yanafungamana kutoka Quran na Sunnah. Ijtihaad inatumika na Ulamaa maalum wa Kiislamu anayeitwa Mujtahid. Ijtihad imezuiwa kutumika karne ya 10 Hijriya. Hivyo, matumizi ya Ijtihad hayakubaliki kwa Waislamu seuze kwa wasokuwa Waislamu

[14] (1966) C. A. D/80/1966 reported in James, R. W and fimbo, G. M CUSTOMARY LAW OF TANZANIA, E. A. L. A, 1973 pg 174-175.

[15] (1978) LRT namba 18

[16] Rudia makala ya Makaramba

[17] (1921) LR 481 A 11 4

[18] (1968) HCD no. 18

[19] (1953) TLR

[20] CA no. 9 of 1983

[21] HCT (1989) TLR pg. 162

[22] Mheshimiwa Katiti (Justice Katiti) “bunge halikukusudia kupitisha sheria hii mpya (SNM 1971) iwe ni ngumu kwa Waislamu wanawake kuomba talaka, kama vile ilivyokuwa kwa sheria za zamani.”

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Share