Hatari Ya Kueneza Hadiyth Dhaifu Na Visa Vya Uongo

 Imekusanywa na: Ummu Iyyaad

Ndugu Waislamu, tunachukua fursa hii ya kutekeleza amri ya Allaah سبحانه وتعالى na Mtume Wake صلى الله عليه وآله وسلم katika Hadiyth Sahiyh ifuatayo: 

  عَنْ تَمِيمٍ الدَّارِيِّ أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ :((الدِّينُ النَّصِيحَةُ قُلْنَا لِمَنْ قَالَ لِلَّهِ وَلِكِتَابِهِ وَلِرَسُولِهِ وَلِأَئِمَّةِ الْمُسْلِمِينَ وَعَامَّتِهِمْ)) مسلم

 Kutoka kwa Tamiym Ad-Daariyyi kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema:

((Dini ni Nasiha, tukasema kwa nani? Akasema: kwa Allaah سبحانه وتعالى na kitabu Chake na Mtume wake, na kwa Viongozi wa Kiislam na watu wa kawaida)) [Muslim]

Waislamu tunatakiwa daima tuwe katika kupeana nasiha na kuepushana na kila aina ya shari. Na kufanya hivi ndio kudhihirisha mapenzi baina yetu. Na kunasihiana katika jambo kama hili la kusambaza Hadiyth dhaifu bila shaka ni muhimu zaidi  kwani kuna hatari kubwa ndani yake kama tuonavyo maonyo yaliyomo katika Hadiyth za Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  

Nasaha hizi zinafuatia makala, hadiyth, au ujumbe mbalimbali unaoenezwa kwenye mtandao au simu za mkono (mobile phones)  na kusukumwa na kupeperushwa kwa mamia ya Waislam, kama ile 'HADIYTH YA ADHABU KUMI NA TANO ZA MWENYE KUACHA SWALAH', au zile hadiyth za 'SIKU KUMI BORA MWEZI WA MFUNGO TATU' au ile 'BARUA KUTOKA KWA SHEIKH AHMAD WA MADINA', 'MALAIKA MKUBWA NA MDOGO', 'FADHILA ZA MAJINA 99 YA ALLAH', 'MALAIKA WATANO WAKATI MTU ANAKUFA' na mfano wa hizo nyingi zikija kwa lugha mbalimbali.

Jambo muhimu kabisa ni kuwa Muislamu inapomfikia Hadiyth ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم basi imeshakuwa WAJIB kwake ahakikishe usahihi wa Hadiyth hiyo. Kama ni Sahihi anaweza kuwatumia wenzake ili apate fadhila za kupata thawabu za wale watakaofuata mafundisho hayo. Na kama ni dhaifu basi haimpasi kusambaza ili asije kubeba dhambi na dhambi za watakaotenda mafunzo hayo ya upotofu.

Hadiyth zifuatazo zinaonyesha manufaa na madhara za mafunzo ya uongo na upotofu:

Hadiyth ya kwanza:

عن أبي مسعود الأنصاري رضي الله عنه يقول النبي صلى الله عليه وسلم : (( من دل على خير فله مثل أجر فاعله)) خرجهما مسلم في صحيحه .

((Mwenye kuongoza katika kheri atapata thawabu kama za mwenye kufanya)) [Muslim katika Sahihi yake]

Hadiyth ya pili:

 عن أبي هريرة رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم أنه قال : ( من دعا إلى هدى كان له من الأجر من أجور من تبعه لا ينقص من أجورهم شيئاً ومن دعا إلى ضلالة كان عليه من الإثم مثل آثام من تبعه لا ينقص ذلك من آثامهم شيئاً)  رواه مسلم  

Kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kasema

((Atakayelingania kwenye uongofu atapata thawabu (ujira) wa yule atakayemfuata bila ya kupungukiwa chochote katika thawabu zao. Na atakayeelekeza katika upotofu atapata dhambi mfano wa dhambi za yule atakayefuata bila ya kupungukiwa chochote katika dhambi zao)) [Muslim]

Hadiyth ya tatu:

((من سن في الإسلام سنة حسنة كان له أجرها وأجر من عمل بها من بعده لا ينقص ذلك من أجورهم شيئاً ومن سن في الإسلام سنة سيئة كان عليه وزرها ووزر من عمل بها من بعده لا ينقص من أوزارهم شيئاً)) خرجه مسلم في صحيحه

((Atakayefanya kitendo chema  katika Uislam atapata ujira wake na ujira wa yule atakayekitenda baada yake  bila ya kupungukiwa  thawabu zao. Na atakayetenda kitendo kibaya katika Uislam atabeba (mzigo wa) dhambi zake na dhambi za yule atakayetenda wala hapungukiwi kitu katika (mzigo wa) dhambi hizo)) [Muslim]

Kusambaza Hadiyth bila ya kuhakisha kama ni Sahihi kutasababisha hatari na madhara yafuatayo

KWANZA:  HATARI YA KUJIANDALIA MAKAZI YA MOTO

Ataangukia katika miongoni mwa mwenye kumuongopea Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kama ilivyo katika Hadiyth:

((من كذب علي متعمدا فليتبوأ مقعده من النار)) متفق عليه

((Atakayeniongopea makusudi basi ajitayarishie makazi yake motoni))  [Al-Bukhaariy Na Muslim]

Na kama tunavyoona kwamba hatari yake ni kujitayarishia makazi motoni (tunamuomba Allaah Atuepushe na hilo). Hivyo pia tutakuwa tumewaingiza na wenzetu ambao nao wataendelea kuzisambaza hizo Hadiyth na itaendelea hivyo hivyo kuwaingiza ndugu zetu wengi katika hatari kama hii. Na hatari zaidi ni kwamba kila watu wanapozidi kuzisambaza, basi dhambi huzidi kuongezeka kwa waliotuma wote nyuma yao na haswa zaidi kwa aliyeanzisha, (maana kwamba, wingi wa dhambi unazidi kuongezeka na wa mwanzo kabisa ndiye mwenye kubeba dhambi za watu wote)  

PILI: KUPOTEZA WAKATI KWA AMALI ZISIZOKUBALIWA

Hadiyth hizo zitazidi kusambaa na wengi wasioweza kupambanua baina ya Hadiyth Sahihi na Hadiyth Dhaifu watakuwa wanaona ni sawa kwao na watakuwa wanapoteza wakati wao kufanya ibada zinazotajwa fadhila zake katika Hadiyth hizo dhaifu na wasipate thawabu yoyote, wakati wangeliweza kuutumia wakati wao na nguvu zao kwa ibada zilizokuwa na uhakika zilizothibiti kwa ushahidi sahihi na wakapata ujira.

Allaah سبحانه وتعالى Anasema:

((وَقَدِمْنَا إِلَى مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاء مَّنثُورًا))

((Na Tutayaendea yale waliyoyatenda katika vitendo vyao, Tuvifanye kama mavumbi yaliyo tawanyika)) [Al-Furqaan:23]

Na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم anasema:

(( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa  na mafunzo ya dini yetu basi kitarudishwa.)) [Al Bukhariy] 

 

JAMBO MUHIMU KUZINGATIA

Ibada zetu zote ikiwa ni kwa vitendo au kauli LAZIMA zutimize sharti mbili muhimu kabisa  nazo ni:

1-Ikhlaas – Iwe kwa kutaka Ridhaa ya Allaah سبحانه وتعالى  na sio yenye Riyaa au sio yenye kutendeka kwa ajili ya       maslahi ya kidunia.

2-Iwe inatokana na mafundisho ya Qur'aan na Sunnah. (kufanyika kwa mujibu wa mafunzo ya Qur'aan na Sunna sahihi).

 

 

TATU: KUPOTEZA MAFUNZO SAHIYH NA KUENEZA MAFUNZO YA UZUSHI (BID'AH)

Dhara jingine la  jambo hili ni kwamba, kila zinapoendelea kusambaa hadiyth hizo dhaifu, ndipo hadiyth sahihi nazo zinaachwa kutumika na kujulikana, na mwishowe ni kuenea mafunzo yasiyo sahihi ya uzushi (Bid'ah) na kupotea yale yaliyo sahihi.

Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم    

(( وأياكم ومحدثات الأمور فإن كل محدثة بدعة وكل بدعة ضلالة))

((Jihadharini na mambo ya uzushi kwani kila uzushi ni Bid'ah na kila Bid'ah ni upotofu))

 

NNE: UKOSEFU WA MAPENZI YA MTUME صلى الله عليه وآله وسلم

Tutambue kuwa kuhakikisha kwamba Hadiyth Sahihi za Mtume صلى الله عليه وآله وسلم zinabakishwa na Hadiyth dhaifu zinafutwa ni ishara ya mapenzi makubwa kwa anayempenda Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kwa dhati kwani hakuna mtu apendaye kumzulia mpenzi wake maneno asiyoyasema. Na kinyume chake ni kudhihirisha ukosefu wa mapenzi ya kipenzi chetu Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم.

Nani basi katika sisi mwenye kumpenda khaswa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ? Yule mwenye kumsambazia tu uzushi bila ya kuwa na hadhari au yule mwenye kujali na khofu ya kumsambazia uzushi?  

TANBIHI:

 

Ukipokea jambo lolote lenye mashaka na utata kuhusiana na Dini, tafadhali tuma maswali@alhidaaya.com lifanyiwe utafiti kabla ya kuwatumia wengine na kuenezwa, na utajibiwa haraka InshaAllaah.

 

Tunamuomba Allaah سبحانه وتعالى Atujaalie nuru ya elimu Yake na Atuonyeshe yaliyo ya haki tuyafuate na yaliyo ya batili tuepukane nayo.

 

 

 

 

Share