Daku: Wakati Wa Mwisho Wa Kula Daku

 

 

Wakati Wa Mwisho Kula Daku

www.alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Ndugu zangu waislam,  Ningependa kujua saa za kula daku ni mwisho saa ngapi

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Daku unaweza kula saa yote hadi inapoingia Alfajiri. Hii ni kutoka na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

   ((..وَكُلُواْ وَاشْرَبُواْ حَتَّى يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ثُمَّ أَتِمُّواْ الصِّيَامَ إِلَى الَّليْلِ...))

((…Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Swawm mpaka usiku…)) [Al-Baqarah: 187]

Hivyo, unaruhusiwa kula daku hadi Alfajiri ndipo unapoanza kufunga. Na hata Muadhini akiadhini na kama una tonge au fundo la maji mdomoni usiliteme, kamilisha kulimeza kisha ndio uanze kufunga. Haya yamethibiti katika Sunnah kama inavyoonyesha Hadiyth ifuatayo:

 

 عن ابن عمر رضي الله عنهما قال: كان لرسول الله صلى الله عليه وسلم مؤذنان: بلال وابن أم مكتوم .فقال رسول الله صلى الله عليه وسلم ((إن بلال يؤذن بليل فكلوا واشربوا حتى يؤذن ابن أم مكتوم))  متق عليه

Kutoka kwa Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhuma) ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na waadhini wawili; Bilaal na Ibn Ummi Maktuum. Akasema: ((Hakika Bilaal anaadhini usiku (adhana ya mwanzo), basi kuleni na mnywe hadi aadhini Ibn Ummi Maktuum)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share