Kusomea Maji Surah Za Ruqyah Kisha Kumwagia Kwenye Ukuta

 

SWALI:

 

Assalamu Aleykum, namshuku ALLAAH alie wapa fahamu ndugu zetu wa alhidaaya kutuelimisha. pia salamu nyingi zimfikie mtume wetu (s.a.w.) pia nawashukuru sana ndugu zangu kwa iman alhidaaya naomba mutuvumilie na malipo yenu kwa ALLAAH na ALLAAH AWAZIDISHIE ELMU zaidi na zaidi na sasa namshukuru ALLAAH elmu yangu naipata kwa alhidaaya na ninawaamini sana.

 

 

Bismillah swali yangu.

Kuna mwalimu m1 aliniambia nisome Surat anam kwenye maji alafu ni mwagie katika ukuta bala itatoka kwa uwezo wa ALLAAH nikamuuliza sio vibaya? Akasema kama qu an inatundikwa na kumwagia itakuwa sio vibaya. Sijafanya ndio nawauliza nyie, nakusomea tiba ya ruqya katika maji ukamwagia katika ukuta pia itakua vibaya? na kitabu ya fadhila ya suratul fatiha ukiifata nivibaya na kitabu ya fadhila ya ikhlas ni nzuri kuisoma na kufuata. Samahani kwa usumbufu ya maswali yangu m.mungu atawazidishia kila la kher na mafanikio mema AMIN.

 JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Alaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Ruqyah na kukubalika kwake kishari’ah.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu.

 

Mwanzo tungependa kukufahamisha kuwa Suratul An‘aam si miongoni mwa Surah au Aayah za Ruqyah. Pia ifahamike Qur-aan haijateremshwa ili itundikwe ukutani bali lengo lake kubwa ni kubadili waliyonayo watu katika tabia, maadili, mas-ala ya kijamii, kiuchumi, kisiasa, kwani huo ni mfumo kamili wa maisha. Qur-aan imeteremshwa kuwaongoza watu katika njia ya sawa. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

 

Hiki ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake, ni uongozi wa wamchao Mwenyezi Mungu” (2: 2).

Pia, “Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa Qur-aan ili iwe ni uongozi kwa watu, na hoja zilizo wazi wa uongozi na upambanuzi” (2: 185).

 

Vile vile kuhusu kumwagwa kwa maji yaliyosomewa Aayah zozote au Surah zozote za Qur-aan ni jambo ambalo halina ushahidi kutoka mafunzo ya Quraan wala ya Sunnah, hivyo ni vizuri kuepukana nalo. Hatujui sababu gani au nia ya kutaka kufanya hivyo. Kama ni kwa ajili ya kuikinga nyumba, basi tayari tunayo mafunzo yenye dalili ya kinga za nyumba. Nazo utazipata katika Swali lifautalo ambalo limeelezewa kwa kirefu aina zote za kinga za nyumba:

 

Unapohamia Katika Nyumba, Unatakiwa Usome Au Kufanya Chochote

 

Ama kuhusu kitabu cha fadhila cha Suratul Faatihah hatufahamu ni kipi. Lakini fadhila za Surah hiyo zinafahamika kupitia kwa Qur-aan na Hadiyth sahihi. Qur-aan inasema:

Na hakika Tumekupa Aayah saba tukufu zisomwazo mara kwa mara na Tumekupa Qur-aan nzima iliyo tukufu” (15: 87).

 

 

 

Pia kupona kwa kiongozi wa kabila moja la Kiarabu ambaye kabila lake lilikataa kuwapatia ugeni Maswahaba (Radhiya Allaahu‘anhum). Kiongozi huyo aliumwa na nge akakosa dawa ya kupunguza machungu, hivyo kuwafanya watu wake waende tena kwa Maswahaba kuona kama wana usaidizi wowote. Mmoja kati ya Maswahaba alimsomea Surah hii naye (kongozi) huyo akawa ni mwenye kupona (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Swalah pia haisihi bila kuisoma Surah hii. Hivyo, kusoma fadhila zilizonukuliwa kutoka kwa Hadiyth sahihi hapana tatizo bali ni jambo lililohimizwa lakini ikiwa ni za kubuniwa itakuwa haifai.

 

Ama Suratul Ikhlaasw ina fadhila kubwa sana. Surah hiyo ni sawa na thuluthi ya Qur-aan. Inafaa tuisome asubuhi na jioni mara tatu tatu na pia wakati wa kulala na baada ya Swalah. Surah hii pamoja na Mu‘awidhatayn ina kinga dhidi ya shetani.

 

Hakika ni kuwa sisi huwa hatupati usumbufu wowote kwa nyinyi kutuuliza mas-ala ili tuweze kuielewa Dini yetu. Tuzidi kuombeana ili tuweze kukidhi haja za watu kwa kujibu maswali yao. Na Allaah Aliyetukuka Atuzidishie mema hapa duniani na kesho Akhera inshaAllaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share