Sadaka Inafaa Kumtolea Mama Yangu Aliyefariki?

 

SWALI:

 

Jirani yangu aliniuliza kuhusu mama yangu aliye fariki kama nimemtolea sadaka baada ya kufa mimi nikamjibu sikutoa sadaka yoyote, isipokua mimi nijuavyo kama ana deni inabidi nimlipie ikiwa deni hilo ni kwa binaadamu au kwa Mwenyezi Mungu na kama aliweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu ya kufunga inabidi pia nimlipie kwa kufunga. Na zaidi na muombea dua yeye akanijibu haifai mtu akifiwa na mama yake inabidi amtolee sadaka ampelekee majuzuu na misahafu madrasa au msikitini sasa sijui uthibitisho wa hili.

 


 

 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwako kwa swali lako hilo. Swali mfano wa hilo tuliwahi kulijibu lakini hakuna tatizo kulijibu kwa mara nyingine tena.

 

Maiti ananufaika kwa yote yaliyopitishwa na sheria ya Kiislamu ima katika Kitabu cha Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na kwa uongofu wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Imepokewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Anapokufa mwanaadamu basi amali zake zote hukatika isipokuwa kwa mambo matatu: Sadaka ya kuendelea, au elimu yenye manufaa au mtoto mwema anayemuombea” (Muslim).

 

Ukitazama kwa hakika mambo yote hayo ni katika juhudi alizofanya maiti kabla ya kufa kwake. Hivyo, ujira wake unamwendea akiwa kaburini mwake.

 

Pia maiti ananufaika kwa yafuatayo kama alivyotuashiria Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakika kwa yanayomfuata Muumini kwa matendo na mambo mema baada ya mauti yake: Elimu aliyofundisha na kuieneza, mtoto mwema aliyemuacha, msahafu aliourithisha au Msikiti aliojenga, au nyumba kwa wapita njia aliyojenga, au sadaka aliyoitoa kutoka katika mali yake katika hali yake ya afya na uhai wake. Zote hizo zinamfuata baada ya umauti wake” (Ibn Maajah na Ibn Khuzaymah, na Isnadi yake ni Hasan). Hizi Hadiyth mbili zinatuonyesha mambo yanayomnufaisha Muislamu anapokufa kwa mambo aliyoyafanya akiwa hai.

 

Lakini zipo Hadiyth zinazotueleza kuwa mtoto anapomtolea mzazi wake aliyefariki sadaka basi thawabu zinamfikia. Miongoni mwazo ni: Yupo mtu aliyemuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakika mamangu ameaga dunia, je itamfaa nikimtolea sadaka?” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ndio” (al-Bukhaariy).

Imepokewa kuwa Sa‘ad bin ‘Ubaadah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema: “Ewe Mtume wa Allaah! Hakika mamake Sa‘ad amekufa, je ni sadaka ipi iliyo bora?” Akasema: “Maji”. Hivyo akachimba kisima akasema: “Cha mamake Sa‘ad” (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah).

 

Na katika Hadiyth nyingine, alikuja mtu kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: “Baba yangu amefariki na ameacha mali ambayo hakuusia chochote, je, nikitoa sadaka mali hiyo atapata malipo kwayo?Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu: “Ndio” (Muslim).

 

Hivyo yako mambo mengi ambayo yanamfaa maiti mojawapo ikiwa ni kumtolea sadaka na pia kumuombea duaa.

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kwa faida zaidi:  

 

‘Amali Za Kuwatendea Wazazi Waliofariki Waendelee Kupokea Thawabu

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share