Ukimbizi - Watoto Wanashangazwa Baba Kubadilisha Jina Nifanyeje?

 

SWALI: 

 

Natumae swala kama hili limeshaulizwa, lakini ningeomba ufafanuzi zaidi Inshallah. Mimi nimekuja ulaya kwa ukimbizi kwa kusema urongo kama tunavyosema kwa sababu ya maisha mazuri, ikanibidi ni badilishe jina langu lote baada ya kupawa fikra hiyo. Leo niko na mke na watoto na jina ninalo tumea siyo langu kwa kizazi, athari ninayo iyona ni kwa watoto kuitwa jina la baba ambalo wanajuwa kuwa siolake na wao wanajuwa jina asili langu,wanakuwa na utata ndani yake jee nifanye nini kutatua hali hino kwa njia ya Kiislam?


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muulizaji swali. Hali kama hiyo inajitokeza pindi mtu akikiuka agizo la Allaah Aliyetukuka na baada ya hapo inakuwa ni majuto na kutoweza kujirudi. Kwa hali hiyo ndiyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akapiga vita sana uongo kwani unakuweka mahali pabaya sana hapa duniani na kesho Akhera. Miongoni mwa muongozo wake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kuwa Muislamu hawezi kusema uongo kabisa. Kwa jinsi hiyo ndiyo Allaah Aliyetukuka Akatutaka tuseme ukweli na tuwe pamoja na wakweli. Anasema Aliyetukuka: “Enyi mlioamini! Mcheni Allaah, na kuweni pamoja na wakweli” (9: 119).

 

Kwa jinsi hiyo ndio kusema ukweli ukawa na ujira mkubwa sana mbele ya Allaah kwa kiasi kuwa malipo yake ni Pepo. Anasema Aliyetukuka: “Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume na Waumini wanawake, na watiifu wanaume na watiifu wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanaosubiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao sadaka wanaume na wanawake, na wanaofunga wanaume na wanawake, na wanaojihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanaomdhukuru Allaah kwa wingi wanaume na wanawake, Allaah Amewaandalia msamaha na ujira mkubwa” (33: 35).

 

Maafa ya kusema uongo ni kama hayo yaliyokupata na kwa kupatwa na hilo hata watoto inakuwa ni vigumu kukuelewa na huenda hilo likawaathiri nao wakaingia katika kosa hilo la uongo. Ikiwa inawezekana kurekebisha kosa hilo katika ngazi za kiserikali bila wewe kupata madhara yoyote itakuwa sawa. Lau ikiwa kufanya hivyo kutakuletea madhara basi itabidi uwaeleweshe watoto wao uhakika wa yale yaliyotokea na kuwa haikuwa kupenda kwako.

 

Baada ya kufanya hivyo, itabidi urudi kwa Allaah Aliyetukuka kwa kuomba toba ya kikweli na uhakika, ujute kwa ulilolifanya na uweke azma ya kutorudia tena kosa hilo maishani mwako. Fanya mema kwa wingi ili madhambi na makosa yako yawe ni yenye kufutwa na Allaah Aliyetukuka kwani Yeye Anatueleza:

Hakika mema huondoa maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanaokumbuka” (11: 114). 

 

Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia:

Mche Allaah popote pale ulipo. Na ufuatilize jambo baya kwa zuri, litafuta hilo baya” (at-Tirmidhiy kutoka kwa Abu Dharr na Mu‘aadh bin Jabal [Radhiya Allaahu ‘anhuma]). 

 

Tunakutakia kila la kheri na fanaka katika yote yatakayokupeleka katika mema na kupata msamaha kutoka kwa Allaah Aliyetukuka pamoja na kurekebisha hayo makosa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share