Yupi Yatima Zaidi? Aliyefiwa Na Mama Au Baba?

   

 

SWALI:

ndugu zangu waislam, Nina maswali mawili ambayo ningewashkuru sana nikijuwa majawabu yake, jee yatima, ni alofiwa na mamake, au baba au wazazi wote wawili? Yupi wafaa kumtizama zaidi?

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa muulizaji swali kuhusu mas-ala ya uyatima. Hakika ni kuwa binaadamu yatima ni yule aliyefiliwa na baba kabla ya yeye kubaleghe. Kijana au msichana akisha baleghe huwa haitwi tena yatima.

Yatima wote wanaofiwa na wazazi wake wawili au baba au mama wote ni yatima na wanahitaji kuangaliwa ipasavyo ili kupata fadhila zake ambazo fadhila hizo ni sawa tu mbele ya Allaah, ikiwa ni kumlea aliyefiwa na wazazi wawili au mmoja.

Hata hivyo kutokana na Swali lako, bila shaka yule ambaye amekosa baba na mama anakuwa ni yatima kamili na anahitaji kuangaliwa na kwa huruma zaidi kwa ajili ya kukosa wazazi wote na pia atakuwa zaidi ni mwenye kuhitaji kuangaliwa kwa matumizi ya malezi yake.     

Kisha anafuatia yule aliyefiwa na baba kwani baba kawaida ndiye mwenye kuleta masarufu nyumbani. Kwa hiyo uangalizi wa kumhudumia kwa ajili ya kulelewa kwake unahitajika zaidi kuliko yule anayefiwa na mama.

Lakini tunarudia kumalizia tena kuwa wote hayo ni Yatima na kuwalea na kuwahurumia ni wajib wetu na fadhila zake ni kubwa mno kama tulivyopata mafunzo katika Qur-aan na Sunnah:

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatuelezea kuhusu kuwatazama mayatima kwa pale Aliposema:

Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa” (76: 8).

Kutomtazama yatima ni jambo ambalo si zuri katika Uislamu kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

Huyo ndiye anayemsukuma yatima” (107: 2).

Na zipo fadhila kubwa zilizowekwa na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa wenye kuwatazama mayatima. Anasimulia Sahl bin Sa‘d (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Mimi na amtazamaye yatima tutakuwa hivi Peponi”, akaonyesha kidole chake cha kati na cha shahada na kuvipambanua (al-Bukhaariy).

Amesema Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Yeyote anayemtazama yatima akiwa ni jamaa yake au si jamaa yake, mimi na yeye tutakuwa pamoja Peponi kama hivi, na Maalik (akaelezea) kwa kuashiria kwa kidole chake cha shahada na cha kati zikiwa karibu (Muslim).

Ulaji wa mali ya mayatima ni miongoni mwa madhambi makubwa ambayo mtu anatakiwa ajiepushe kabisa.

Amesema Allah Aliyetukuka:

Hakika wanaokula mali ya mayatima kwa dhulma, hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao moto, na wataingia Motoni” (4: 10).

Na Amesema Aliyetukuka:

Wala msiyakaribie mali ya yatima ila kwa njia ya wema kabisa” (6: 152).

Na Amesema Aliyetukuka: 

 

Na wanakuuliza juu ya mayatima. Sema: Kuwatengenezea ndio kheri. Na mkichanganyika nao basi ni ndugu zenu; na Allaah Anamjua mharibifu na mtengenezaji” (2: 220).

Na imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Jiepusheni na madhambi saba yanayoangamiza”. Watu wakauliza: “Ewe Mtume wa Allah ni yapo hayo?” Akasema: “Kumshirikisha Allaah, na uchawi, na kuua nafsi ambayo Allaah Ameiharamisha isipokuwa kwa haki, na kula riba, kula mali ya yatima, kukimbia siku ya vita na kuwatuhumu kwa zinaa wanawake waliohifadhiwa na Allaah, Waumini wasiyo na habari ya zinaa” (Al-Bukhaariy na Muslim).

Hivyo ni vyema kuwatazama mayatima kwa kadiri ya uwezo wako na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Atakubariki hapa duniani na Kesho Akhera kukuweka mahali pema.

Ingia katika kiungo kifuatacho pia upate pia maelezo zaidi kuhusu kulea yatima:

Jukumu La Kulea Yatima

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share