Kukata Undugu Na Dada Anayefanya Ushirikina Na Kupenda Starehe Za Dunia Inajuzu?

SWALI:

 

 

 

Inafaa kutosemezana na dada yako kama hataki kukutendea haki kwa mfano yeye anataka kukutibu kishirikina na wewe kutaki halafu anapenda starehe za dunia kama nyimbo na mengineyo je inafaa kumnunia? Wabillahi Taufiq

 

Ahsante


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kukata uhusiano na dada yako kwa sababu maalumu.

 

 

Kumsusia ndugu katika mas-ala kama hayo ya shirki, ni jambo ambalo lipo katika sheria. Hata hivyo, inabidi upite kipindi cha kumnasihi kwa muda kabla ya kutekeleza hilo. Mwanzo inatakiwa utumie njia zote za kuweza kumnasihi ili aachane na mambo hayo mabaya kwa njia na mawaidha mazuri. Inatakiwa uzungumze naye kuhusu ubaya wa ushirikina na kuwa anayemshirikisha Allaah Aliyetukuka basi ‘amali yake hupomoka na kutosamehewa (Suratun Nisaa’ [4]]: 48, 116), ushirikina ni dhuluma kubwa sana (Luqmaan [31]: 13). Ikiwa hukufanikiwa watumie marafiki zake walio wema, mpe vitabu vinavyozungumzia kuhusu uovu wa shirki, kanda na kaseti na makala pamoja na njia nyingine zitakazoweza kumfahamisha madhara hayo.

 

Ikiwa umetumia njia zote unazoziona ni sawa lakini dada yako amekataa basi unaweza kumkata na kumsusa dada yako kwa maasiya anayoyafanya. Hii tunaweza kupata funzo kutokana na kususiwa Maswahaba watatu (Radhiya Allaahu ‘anhum) kama ilivyo katika kitabu cha Hadiyth cha Imaam an-Nawawiy, Riyaadhw asw-Swaalihiyn, namba 21.

 

Utakaloweza kufanya ni kumchapishia makala asome katika kiungo kifuataco. Kufanya hivyo na pindi akiongoka, thawabu zitakurudia wewe Inshaa-Allaah.

 

 Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!- إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Ampatie hidaaya dada yako na arudi vyema katika maagizo ya Dini, Amiyn.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share