Hijaab Inasababisha Kutoka Nywele? Nini Hukmu Yake?

 

Hukmu Ya Hijaab - Je, Inasababisha Kutoka Nywele?

 

Alhidaaya.com 

 

 

SWALI:

 

Assalaamu Alaykum Ndugu Zangu, Naomba Kuwa Uliza Nipate Kujua.

 

Mwanamke Ni Lazima Kufunika Kichwa Mbele Za Muhreem. Ryt Lakini Mbele Za Watu Wake Wa Nyumbani Na Muhreem Wake Akae Kichwa Wazi-----ryt Tumesisitizwa Tufanye Dhikrullah Saa Zote    Na Jina La Allaah Huwezi  Au 

 

Una Weza Kutaja   Kichwa Wazi ??? Sasa Mwanamke   Wakati Gani Ata Vua Hijaab?

 

Mimi Nime Nyonyoka Nywele Na Nimeambiwa Sababu Ni Hijaab. Inawezekana Allah Atuwekee   Sharia Ya   Kutudhuru???? Plz Help.   

 

Jazaakallaahu Kheir Fiamaanillah

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Mwanamke akiwa nyumbani na mumewe au maharimu zake (wanaume wasioweza kumuoa) Shariy’ah imempa ruhusa kutokuwa katika vazi la hijaab. Isipokuwa kuweko na mipaka ya kuonyesha mwili wake  asjiweke wazi sana hadi akaonyesha zaidi kwao sehemu ya mwili wake, au kuvaa nguo iliyobana au inayoonyesha mwili wake wa ndani n.k.   Ni muhimu kuweko stara baina yao japokuwa ni maharimu wake.

 

 

Na ikiwa upo na mume wako chumbani basi unaruhusiwa kupunguza mavazi yako kadiri unavyopenda na kadiri mumeo atakavyotaka. Hilo halina shaka.

 

 

Kuhusu kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla), inaruhusiwa kumdhukuru bila ya kujifunika kichwa.  

 

 

Ama kuhusu kunyonyoka nywele haina uhusiano wowote na uvaaji wa hijaab. Lau ingekuwa kuwa hivyo hawangepiga marufuku jambo hilo katika nchi za Magharibi Wangewaacha Waislam wawe na uhuru wao katika kuvaa kama walivyoamrishwa na Rabb wao, ili wanyonyoke nywele kwani ingelikuwa ndio furaha yao.  

 

 

Mwaka 2005 katika gazeti moja Kenya lilitaja utafiti uliofanywa nchi ya Uzunguni kuwa kuvaa Hijaab kunaleta ugonjwa wa baridi yabisi. Kama hilo lingekuwa kweli, basi leo hii wanawake wote wangekuwa wapo nyumbani hawawezi kutembea! Lakini hizo ni propaganda maarufu zinazoongozwa na nchi za kimagharibi.  

 

 

Ugonjwa wa kupuputika (kunyonyoka) nywele ni kawaida kwa wanawake na wanaume ikiwa watakosa protini katika vyakula. Ugonjwa kama huu huweza kutibika kwa kutumia aina fulani ya mafuta ambayo inazipatia nguvu   Hivyo jambo hilo si la kumshitua wala kumtia taharuki mtu yeyote yule.

 

 

Kuliweko na Swahaabiyyah katika enzi za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyepata tatizo hilo.  Asmaa (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: Mwanamke mmoja alimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ee Rasuli wa Allaah! Binti yangu alipatikana na shurua zikatoka nywele zake, nami sasa ninamuoza, je, niziunge nywele zake [kwa kuziunganisha na nywele zingine]?)) Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu: ((Allaah Amemlaani muunga nywele na muungwaji)) [Al-Bukhaariy].

 

 

Bila shaka inafahamika kuwa Allaah ('Azza wa Jalla) Ndiye Muumba wetu, hivyo, Anajua yale mambo yanayotudhuru na yanayotunufaisha katika maisha yetu. Hatuamuru kufanya kitu ila kina faida kemkemu kwetu japokuwa huenda tusilifahamu hilo na jambo lolote Analotukataza basi lina madhara makubwa kwetu.

 

 

Kunyonyokwa na nywele ni magonjwa ambayo yanaweza kumpata mmoja miongoni mwetu, na kila ugonjwa una dawa yake kama alivyotueleza hayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):  

  

 عن أبي الدرداء رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : ((إن الله تعالى أنزل الداء والدواء وجعل لكل داء دواء فتداووا ولا تداووا بالحرام))

Imetoka kwa Abuu Ad-Dardaa (Radhwiya Allahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Ameteremsha maradhi na dawa zake. Kwa kila maradhi kuna dawa yake, basi jitibuni wala msijitibu kwa yaliyo haraamu)) [Al-Bukhaariy na Abu Daawuwd]

 

Na pia:

 

عن عبدالله بن مسعود :قال رسول الله صلى الله عليه وآله وسلم  (( ما أنزلَ اللَّهُ داءً إلَّا أنزلَ لَه شفاءً فعليكُم بألبانِ البقرِ فإنَّها تَرُمُّ من كلِّ الشَّجرِ))

Imetoka kwa 'Abdullah bin Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu): Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Hakuteremsha maradhi ila Ameteremsha dawa zake, basi juu yenu (kunyweni) maziwa ya ng'ombe kwani yanatokana na kila aina ya miti)) [Hadiyth Swahiyh au hasan, ameisahihisha Al-Albaaniy katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (4/208), Swahiyh Al-Jaami’ (1808)]  

 

 

Hivyo, Kwa kuwa hakika ni hiyo basi suluhisho ni kutafuta tiba endapo tunakuwa wagonjwa.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share