Mwanamke Katika Eda Kuzungumza Na Asiye Mahram Wake – Mchanganyiko Wa Wanawake Na Jamaa Wasio Maaharim Wao

SWALI:

 

assalam alaikum warahmatu llahi wabarakatu,kwanza ningependa kuwapapongezi kwa jitihada zenu.jazakumu llahu kheir. ama swali langu,nilikua nauliza kama mwanamke ambaye yuko amefiliwa namumewe nayeyumo kwenye eda,akipigiwa simu kutoka londo na causin yake mwanamume ambaye anamke nawatoto,kumpapole nabaada yakila wiki au mwezi akamjulia tena haliyake,mwenye eda akamwambia huyu causin yake kuwa ameambiwa hafai kuzungumza na mtu yoyote ambaye aweza kumuowa,sasa nauliza kama hivi nisawa au sisawa?kama nisawa vipi kuhusu

watu kutembeleana majumbani kama mtu kuwatembelea cousin zake ambao

wameolewa au marafikizake wanaume  wakakaa pamoja kula au kuzungumza familia zote nao wamejistiri?

 assalaam aleikum


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Mwanamke katika Eda anatakiwa afuate sheria za Eda kama Alizozihukumu Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Hakuna tofauti katika kutekeleza sheria hizo hata ikiwa ni jamaa wa karibu kama ulivyouliza kuhusu mtoto wa ‘ami, au mjomba, au shangazi (cousin) au hata jamaa yeyote mwengine ambaye anaweza kumuoa. Watu ambao hawawezi kumuoa ni wale waliotajwa katika Aayah ifuatayo:

 

((وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَى جُيُوبِهِنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاء بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاء بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُوْلِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَى عَوْرَاتِ النِّسَاء وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ وَتُوبُوا إِلَى اللَّهِ جَمِيعًا أَيُّهَا الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ))

 

((Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au wafuasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyokhusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa)) [An-Nuur: 31]

Kwa hiyo haifai kabisa mwanamke kuzungumza na asiye Mahram wake ila kwa dharura tu. Ama kusema cousin wake ampigie kumuuliza hali kila wiki, hiyo sio dharura na hivyo ni jambo linalopaswa kujiepusha nalo.

 

Soma makala ifuatayo ambayo imeelezea yote yanayopasa na yasiyopasa katika EDA.

 

EDA - Hikma Yake, Hukmu Zake, Yanayopasa Na Yasiyopasa

 

Na kuhusu kutembeleana majumbani baina ya jamaa wasio Mahaarim (wanaume ambao wanaweza kukuoa), ni kwamba hakuna ubaya ikiwa watakapokuja patakuwepo na Mahaarim zako vilevile pamoja na wewe na si kuwepo wewe peke yako. Kadhalika wewe kwenda kuwatembelea jamaa zako ambao si Mahaarim zako panahitajika pawepo Mahaarim zako hapo ili kuzuilika aina yoyote ile ya fitna. Na haipasi kuchanganyika wanawake na wanaume hata kama ni jamaa ikiwa ni cousins, au shemeji n.k. Hivyo basi linalopasa ni kujitenga nao, wanawake wawe katika chumba peke yao na wanaume peke yao. Kufanya hivyo itakuwa ni kufuata sheria za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na pia kuwafunza ndugu, jamaa na wengineo sheria hiyo ambayo wengi ima hawana elimu nayo, au hawaifuati. Pia itakuwa ni mafunzo na mazoea kwa vizazi vyenu nao wataendeleza mafunzo hayo na thawabu zote zitamfikia mwenye kuanza kutekeleza na kufunza wenziwe.

 

Ingia katika makala muhimu upate maelezo zaidi.

 

Ikhtilaatw (Kuchanganyika Wanaume Na Wanawake)

 

Na Allaah Anajua zaidi  

 

 

Share