Kuwaosha Watoto Wachanga Kwa Majimbo Kwa Ajili Ya Siha Na Kuwakinga Maovu Inafaa?

 

SWALI:

Shukran kwa kutujibia masuali yetu na Inshallah Allah atakulipeni mema na muzidi kutusaidia ndugu zenu katika Imani.

Suali langu ni, katika jamii zetu hususan huku Tanzania tangu miaka ya nyuma, wazee wetu wakijifungua huwa watoto wao wanawakosha majimbo ili mtoto akue na achangamke uzuri na aingie mwili akazane. Pia hilo jimbo linamsaidia kumuepusha mtoto na mambo mabaya kama Sihri n.k. Na hadi hii leo watoto wakizaliwa wazee wanashikilia lazima watoto wakoshwe jimbo, na ukikataa inakua ugomvi.

Je hii ni sahihi? Na kama sio sahihi naomba munifafanulie.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa muulizaji swali kuhusu suala la ‘majimbo’. Kulingana na muulizaji inaonyesha kama haya yanayoitwa majimbo yanachukuliwa kuwa ndio yenye kuwahifadhi watoto na kuwapatia siha nzuri.

Kwa hivyo, suala ambalo tutaliangazia ni kuhusu njia gani tunafaa tuwakinge watoto pamoja na kujikinga sisi wenyewe. Kinga ni zile tulizopatiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kinyume na hivyo hatutakuwa ni wenye kufaulu wala kupata kinga ya uhakika na mara nyingi tutakuwa tunanyonywa. Kwa kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) peke Yake ndio tunapata kinga na hakuna madhara yanayoweza kutufika.

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatueleza:

Sema: Halitusibu ila Alilotuandikia Allaah. Yeye ndiye Mola wetu Mlinzi. Na Waumini wamtegemee Allaah tu!” (9: 51).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuusia Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) na hivyo kutuusia sisi:

Jua kwamba hakika lau watu wakusanyike ili wakunufaishe wewe kwa jambo lolote, hawawezi kukunufaisha ila kwa jambo Alilokuandikia Allaah; na wakikusanyika ili kukudhuru kwa jambo lolote, hawawezi kukudhuru ila kwa jambo Alilokuandikia Allaah(at-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh).

Kinga anazopata mtoto zinaanza kuanzia wakati baba anapomchagulia mama. Dini ni kinga kubwa kwa wanandoa na vizazi vyao vitakavyopatikana. Kinga yenyewe inaanza pale mwanamme kabla ya kuposa anaposimama kuswali rakaa mbili ili kumtaka ushauri Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na mwanamke naye afanye vivyo hivyo. Hii ni Swalah ya Istikhaarah ambayo Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhuma) anatuelezea kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwafundisha Swalah hiyo kama alivyokuwa akiwafundisha Surah katika Qur-aan (al-Bukhaariy).

Baada ya posa na wanandoa kuungana katika Nikaah, ni Sunnah kwa mume kusema anapoingia kwa mkewe siku ya mwanzo du’aa ifuatayo:

“Allahumma inniy as-aluka khayrahaa wa khayra maa jabaltahaa ‘alayhi wa a’udhu bika min sharrihaa wa sharri maa jabaltahaa ‘alayhi – Ee Allaah! Nakuomba kheri yake na kheri aliyokuja nayo na uniepushe na shari yake na shari aliyokuja nayo” (Abu Daawuud na Ibn Maajah).

Usiku huo wa mwanzo baina ya mume na mke si usiku wa starehe tu bali ni lazima watekeleze amri za Dini, na katika hayo ni Swalah. Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

Atakapooa mmoja wenu na ikawa ni siku ya mjengo na aswali rakaa mbili na amuamuru mkewe aswali nyuma yake kwani Allaah Atajaalia katika nyumba hiyo kheri” (al-Bazzaar).

Kinga ya mtoto pia inapatikana kwa mume kuomba du’aa aliyotufundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati mtu anajamiiana na mkewe kwa kusema:

Bismillaahi Allaahumma jannibnash Shaytwaan wa jannibish Shaytwaana maa razaqtanaa – Kwa jina la Allaah, Ee Allaah! Tuepushe na Shetani na Umuepushe kwa kile utakachoturuzuku”. Akizaliwa mtoto Shetani hataweza kumdhuru (al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Ibn ‘Abbaas [Radhiya Allaahu ‘anhuma]). 

Mtoto pia anakingwa hasa na magonjwa kwa kupatiwa lishe bora na katika siku za mwanzo kunyonyeshwa. Maziwa ya mama hasa kwa wiki za mwanzo yana kinga kubwa sana kwani yanamuepusha na maradhi mengi na kumfanya kuwa na siha nzuri. Kwa hiyo, ndio Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatuambia:

Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili kwa anayetaka kutimiza kunyonyesha. Na juu ya baba yake chakula cha kina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada” (2: 233).

Mama kupata lishe bora ni njia moja ya kuwakinga watoto kutokana na maradhi. Na pindi mtoto anapokuwa mgonjwa basi mtoto anafaa kupelekwa na wazazi wake hospitali ili atibiwe. Hilo la kutibiwa ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesema:

Hakika kila ugonjwa una dawa, ikisibu dawa ugonjwa anapona kwa idhini ya Allaah Aliyetukuka” (Muslim na Ahmad).

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) ndiye Mwenye kuponyesha kama Alivyotueleza:

Na ninapougua ni Yeye ndiye Anayeniponesha” (26: 80).

Ama kinga nyingine, ni kusoma Aayah kumi za Suratul-Baqarah ambazo zinaleta natija kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kuiepusha nyumba hiyo na kuingiliwa na mashetani. Ayah zenyewe ni kama zifuatazo 1 hadi 4, 255 hadi 257 na 284 hadi 286. Pia kuwakinga watoto ndani ya nyumba pindi kunapoingia kiza. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesema:

Ikifika jioni wazuilieni watoto wenu kutoka toka kwani mashetani wanatawanyika nyakati hizo … fungeni milango na mtajeni Allaah mnapoifunga kwani Shetani hafungui mlango uliofungwa” (al-Bukhaariy na Muslim).

Kinga nyingine kubwa ya watoto ni vile alivyokuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwafanyia wajukuu zake, al-Hasan na al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kwa kuwasomea: “U‘idhukumaa bikalimatiLlaahi at-Tammaati min kulli Shaytwaaniw wa haammah wa min kulli ‘aynil laamah – Nawakinga kwa maneno ya Allaah yaliyotimia, Awakinge kutokana na kila Shetani, na uvamizi na kila jicho lenye kudhuru” (al-Bukhaariy).

Ama kinga hiyo wanayofanyiwa watoto wa sehemu uliyopo haina faida yoyote na haijapokewa katika machimbuko ya Kiislamu ya kisheria. Inawezekana kuwa hayo ‘majimbo’ kama mnavyoita yanawafanya kweli watoto wawe wachangamfu lakini huo ni mtihani kwani Shetani huwa akiwapambia wanaadamu mambo yao mpaka wakayakinisha kuwa yanafanya kazi. Huo ni mtihani kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kwenu kutazamwa kama mtaweza kushika yale Yake au mtategemea vingine mbali na Yeye. Bila shaka, utumiaji wa ‘majimbo’ kwa ajili kumuepusha mtoto na mambo mabaya na sihri ni dalili tosha kuwa kunatumika sihri pia au mfano wake. Utumiaji wa sihri ni shirki na haramu katika Dini yetu tukufu. 

Tunakuombea kila la kheri katika kuondosha munkari kama huo wa ‘majimbo’.

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 



 

Share