Mwanamke Anataka Kuolewa Ndoa Ya Pili, Je, Anahitaji Idhini Ya Walii?

SWALI:

Ndugu waislam, shukurani kubwa zimwendee Allaah subhanahu wataala na mtume wetu muhammad S.A.W pamoja na wale wote walioanzisha websait hii . Suala langu         

 

Mimi niliolewa na kuachika nikabahatika kuposwa na mchumba mwengine    

ambae hatujuanikwa hiyo hakuna shaka kwenye ndoa kwa hilo, lakini kinachonikosesha raha ya maisha ni ile siku ya harusi hakuna aliyechukua

idhini kwa wazee wangu niliwaambia kama naolewa na tulikubalia na wazee wa huyu mchumba walikwenda kujuana na familia yangu.lakini siku ya harusi ilipofika niliambiwa kama madhali niliolewa na kuachwa basi haina haja kuchukuliwa idhin jee ndoa yangu mimi ipo kwenye fungu gani? Na kama haijasihi nifanye nini? Naomba jawabu lenu haraka iwezekanavyo. Ahsanteni.    

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri dada yetu. Ieleweke wazi kuwa ndoa yoyote ile ni lazima kuwe na walii wa mwanamke iwe ni ndoa yake ya kwanza (akiwa bikira) au ya pili (akiwa ameachwa au ni mjane). Walii kumuoza bintiye ni katika sharti la kusihi Nikaah. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

Hapana Nikaah ila kuwepo kwa walii …” (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah kutoka kwa Abu Muusa [Radhiya Allaahu ‘anhu]).

Hivyo, mwanamke akijiozesha mwenyewe bila walii, Nikaah yake ni batili. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Amewataka mawalii kuwaozesha wajane wao:

Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu” 924: 32).

Akasema tena (Subhaanahu wa Ta‘ala): “Basi msiwazuie kuolewa na waume zao endapo baina yao wamepatana kwa wema” (2: 232).

Hii Aayah ya pili wanaambiwa mawalii wasiwe ni wenye kuwazuia wawili wapendao baada ya kuwa eda imemalizika kurudiana bali wanataka watoe idhini ikiwa kuna wema ndani ya kurudiana kwao.

Walii wa mwanamke ni babake, kisha aliyeusiwa naye, kisha babu mzaa baba, kisha watoto wake mwanamke, kisha watoto wao hata wakishuka chini vipi, kisha nduguze shaqiqi, kisha nduguze kwa baba, kisha watoto wao, kisha ‘ami shaqiqi, kisha ‘ami kwa baba tu, kisha watoto wao. Kisha jamaa zake wa karibu na kisha hakimu ikiwa hana jamaa kabisa.

Kama tulivyosema hapo juu idhini ya walii ni lazima katika ndoa yoyote. Kwa vile wazazi wa mume walikwenda kwa wazazi wako na kulingana na maelezo yako ni kuwa ndoa hiyo ilikubalika. Kwa maelezo yako kuwa wazee wa mume walionana na wazee wako kabla ya harusi na kukubaliana, hiyo inaonyesha kuwa walii wako alitoa idhini japo ilikuwa si siku ile ile ya harusi hilo si tatizo, muhimu ni kuwa alilikubalia jambo hilo. Na kwa hali hiyo, inavyoonyesha ni kuwa ndoa yako ilipata idhini ya walii wako.

Tunakutakia kila la kheri na fanaka katika ndoa yako.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share