Mume Na Mke Kuishi Mbali Kwa Muda Mrefu

 

 

SWALI:

 

Assalaam aleikum warah.... 

Nini inakuwa juu ya mtu na mume wake kuishi sehemu tofauti ingawa ni  kwa maridhiano kwa mda mrefu, na hasa inapokuwa hakuna uwezekano wa mmoja kumfuata mwenzake mfano anapokuwa kifungoni ama machimboni ama popote inapokuwa ngumu kutoka kwa hiari yake na kwa miaka kadhaa imepita?

wabilah taufiq


 

JIBU:  

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Mume na mke kuishi mbali kwa maridhiano hakuna neno, ila mushkila ni kuishi mbali mbali kwa muda mrefu. Kutengana huku huenda kukasababisha mmoja wao au wote kutokuweza kustahmili au kujizuia kumtamani mwenziwe hivyo huenda ikampeleka mtu kufanya yasiyompasa. Hasa kwa mwanamume ambaye Allah (Subhaana wa Ta'aala)  Amemtambua kuwa ni dhaifu kwa mambo hayo na ndio maana Akawaruhusu wanaume waweze kuoa wake mpaka wanne.

 

Kwa hakika kunapotokea hilo huwa ugumu zaidi uko kwa mwanamke kwa sababu yeye hawezi kuolewa na mtu mwengine ilhali mwanamme anaweza akaoa kule alipo isipokuwa anapokuwa jela. Katika wakati wa Ukhalifa wa ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) wakati ambapo Jihadi zilipamba moto na Waislamu wengi wakawa wako nje katika uwanja wa vita kulitokea yafuatayo. Wakati wa doria zake za usiku, ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipita kwa nyumba na kumsikia mwanamke akiimba:

 

"Lau ingekuwa si kumcha Allah,    Basi hiki kitanda kingetikisika".

 

Asubuhi ‘Umar (Radhiya Allaau ‘anhu) alimwendea bintiye, Mama wa Waumini, Hafswa (Radhiya Allaahu ‘anha) na kumuuliza mwanamke anaweza kukaa muda gani bila kuwa na mumewe. Hafswa (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa anaona haya kidogo lakini baba yake akamwambia Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Haoni haya katika ukweli. Hapo akamwambia miezi 4 au miezi 4 na siku 10. Amiri wa Waumini, ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alitoa agizo kwa majemadari jeshi na magavana wasiwaweke mujahidina zaidi ya muda huo. Kabla ya muda huo kumalizika wanatakiwa waje waangalie familia zao kisha ndio warudi tena vitani.

 

Na ndio ikiwa mume hajulikani alipo au muda ni mwingi na mke hawezi kujizuilia, mke anaweza kutaka talaka ili akipata mume aolewe na ajiepushe na zinaa.

 

Na Allah Anajua zaidi

 

Share