Anaweza Kufunga Ndoa Bila Ya Kumshauri Mama Yake Asiye Muislamu?

 

SWALI:

Nimezaliwa nje ya ndoa na mama yangu alikuwa muislamu, ila kwa sasa si muislamu, nimejitahidi sana kumrejesha lakini sikufanikiwa hadi imefikia kuwa mimi na yeye huwa hatupendani kama mtu na mama yake, swali ni kwamba hivi majuzi nilimtambulisha kwa mchumba wangu ila yeye hakuonesha ushiriano hata kidogo hata kuwapa taarifa ndugu zake hakutaka, kiasi kwamba nilishindwa kutekeleza ibada hiyo muhimu ya ndoa, sasa nataka kujipanga tena upya ili niondokane na 'uwendawazimu huu' je naweza kufunga ndoa bila ya kuwapa taarifa upande wa familia yangu? kwani wananiaona kinyume pindi ninapowatamkia suala la ndoa.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo kuhusu uhusiano mbaya baina yako na mamako mzazi na pia ndoa.

Ama kuhusu mahusiano yako na mamako jaribu kiasi unachoweza mbali na kwamba yeye hataki uhusiano nawe.

Suala lako hilo ni zito lakini usife moyo kabisa kwani kwa juhudi zako na tawfiki ya Allaah Aliyetukuka siku moja atabadilika nami nina hakika na hilo. Yeye kuwa ni mbaya kwako nawe usifanye makosa hayo kabisa kwa uovu haulipwi na uovu bali endelea kumtendea wema. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

 

Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu. Lakini hawapewi wema huu ila wanao subiri, wala hawapewi ila wenye bahati kubwa” (41: 34 – 35).

Endelea kumtendea wema mamako hata kama amekukata nawe utapata thawabu nyingi kabisa mbele ya Allaah Aliyetukuka na usikose kumuombea du’aa aongoke hapa hajafariki.

Ama kuhusu ndoa hakika ni kuwa mwanamme hahitaji idhini kutoka kwa wazazi si kama msichana. Jambo linalotakiwa kwako kufanya ni kuonyesha utu na Uislamu kwa kuwaeleza jamaa zako upande wa mama ikiwa wamekupuuza basi unaweza kuendelea kuoa kwani ndoa haicheleweshwi kabisa. Fadhila na ubora wa kuoa ni mkubwa hivyo usichelewe ukiwa umejiona uko tayari kutekeleza ibadah hiyo.

Tunakuombea kwa Allaah Aliyetukuka Akufanyie sahali, wepesi na uweze kutekeleza hilo bila taabu wala shida.

Na Allaah Anajua zaidi

Share