Ukombozi Wa Mwanamke

 

Ukombozi Wa Mwanamke

 

Imekusanywa na: Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amempa heshima mwanamke kwa kumpandisha cheo kutoka Kwake na sio kutoka kwa mwanamme. Lakini hiyo sio hali ya mwanamke wa Kimagharibi, kwani Allaah anafutwa kabisa na hakuna ulinganisho unaofanywa ila kwa mwanamume tu. Matokeo yake mwanamke wa Kimagharibi analazimika kutafuta cheo chake kwa kujilinganisha na mwanamme. Na kwa kufanya hivyo, amejikubalisha kufuata njia isiyo sahihi. Amekubali kuwa mwanamme ndio kigezo chake, na hatoweza kuwa binadamu kamili mpaka awe sawa na mwanamme.

 

Na ni wanawake wangapi tunawaona wakiiga nyendo za kiume? Mwanamme anapokata nywele zake, na yeye hutaka kuzipunguza. Anapojiunga na jeshi, mwanamke pia hutaka kujiunga na jeshi, mwanamme akiwa konda wa daladala na yeye pia anataka kuwa konda wa kike na mengineyo zaidi. Anataka vitu hivi bila ya sababu nyengine ila ni "usawa".

 

Kawaida ya mwanamke wa Kimagharibi ni kuwa, anamsahau Allaah na hayupo kwenye imani iliyo sahihi. Haya ndiyo yanayofanyika hata kwa wanawake wa Kiislamu, kujidai kumsahau Allaah na kutoka kwenye imani iliyo sahihi. Pia wanawake wa Kiislamu wamekuwa wakifuata kwa upofu mwenendo usio sahihi na kiitikio cha dhana ya kuwa mwanamke ni sawa na mwanamme kwa kila kitu. Muislamu wa kike anasahau kutambua kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) amempa heshima mwanamme na mwanamke kutokana na tofauti zao na sio kutokana na usawa. Hakika sio maadili ya Uislamu kufuata kila akifanyacho mwengine hata kikiwa sio sahihi. Hili ndilo linalofanyika kwa wanawake, kwa kuwa mwanamme anakifanya na wanawake watake kuiga. Kwa mfano mwanamme kuongoza swala ya jamaa wakiwemo hata wanawake ndani yake kumewashughulisha sana wanawake mpaka kufikia kutaka kuswalisha hata wanaume. Na kuongoza sala sio bora kwa kuwa ni jambo la uongozi tu. Yule anayeongoza sala hana kwa njia yeyote hadhi ya imani na dini. Kama kweli ingekuwa nafasi ya mwanamke kupata utukufu, cheo na utashi wa dini, kwanini Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ashindwe kumuomba Bibi Khadiyjah (Radhwiya Allaahu ‘Anha) au Bibi Ayshah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa) ambao ni bora wa bora kwa viongozi hawa wa kike kuongoza swala? Wanawake hawa waliahidiwa pepo kwa imani zao na wala sio kwa uongozi wao.

 

Wanawake wa leo wanamuangalia mwanamme na kuanza kufikiria kuwa “hiyo sio haki”. Kila kukicha wanamuangalia mwanamme alifanya nini jana na anaendelea kwa kuvumbua nini ili naye mwanamke apate kuwa sawa na huyo mwanamme. Wanawake wanafikiri hayo, ijapokuwa kwa upande mwengine Allaah hakutoa utukufu wowote kwa mwanamme katika mambo ya mirathi wala kuongoza swala. Isipokuwa kikubwa walichonacho wanaume ni mzigo wa majukumu ya kuwatumikia hao wanawake kila siku. Wanachoshindwa wanaume, ni kusimamisha huo wajibu wao, na ndio maana wanawake hawapati haki zao. Yareti kama wanaume watamhifadhi mwanamke na kumtumikia namna ambavyo Uislamu umeamrisha, mwanamke leo hatowaacha watoto wake kwenda kutafuta kazi zisizokuwa za msingi. Ni juu yao wanawake kupigania haki zao na sio kuzibeza tu kila kukicha.

 

Ni wakati wa wanawake kukaa kupitia daarisa zinazomgusa mwanamke na kuona neema alizofadhilishwa kwa dini yake na sio kwa jinsia yake. Na Allaah amempa heshima pekee mama. Mtume ametufundisha kuwa pepo ipo chini ya nyayo za mama. Lakini vyovyote atakavyofanya mwanamme, hawezi kuwa sawa na mwanamme. Kwa jambo hili mbona hakuna usawa? Kwanini mama amepewa heshima pekee kuliko mwanamme? Lilipotolewa suala nani anayefaa kupewa heshima zaidi baina ya mama na baba, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijibu "mama" mara tatu kabla ya kusema "baba" mara moja tu. Je kwa hili wanaume hawahitaji ukombozi? Sasa tuigeuze shilingi upande wa pili kwa kuuangalia wajibu wa mwanamme kumtumikia mwanamke katika malazi, mavazi mpaka viazi (chakula). Pia tunamuona mwanamme akifaradhishwa kuswali msikitini hali ya kuwa mwanamke amestiriwa kutekeleza ibada hii adhimu ndani ya nyumba yake. Jee kwa hili kuna usawa? Hamna wanaume watakaopenda na wao waruhusiwe kuanzia sasa kuswali vyumbani mwao bila ya udhuru wowote? Mbona hapa wanaume wanahitaji ukombozi? Na kwanini asisimame mwanamme kutetea ukombozi wa kijinga kama huu kwa ile dhana ya "jinsia sawa"? Hii yote kwa sababu mwanamme si mtu wa kuchezewa kifikra mara moja. Anaelewa umuhimu wake ndani ya jamii na nafasi yake kwa mwanamke. Kilichoshindikana hapa ni utekelezaji tu wa mwanamme juu ya majukumu yake. Na ndio maana hatokaa mwanamme kuanza kunadi "ukombozi wa mwanamme" Na itakuwa kioja cha karne wanaume kudai usawa katika mambo hayo. Tunarudia kusema vyovyote afanyavyo, mwanamme (baba) hawezi kuwa sawa na hadhi iliyo sawa na mama.

 

Na katika mambo ambayo Allaah amempa heshima kwa upekee wake mwanamke, atajifanya kuwa na kazi ya kutafuta nafasi na heshima yake kwa kigezo cha mwanamme, iwe ni kwasababu ya cheo au hata kuwa kuonekana tu. Kwa hivyo upekee wake mwanamke uwe wa aina yoyote, kulingana na desturi za Uislamu ni kujishusha hadhi kwa kujilinganisha kwake na mwanamme. Kwa hisia hizo ni aibu, kwani hata cheo kile tukufu cha mama kimesahaulika. Kwenye mapambano baina ya vita vya hisia na uwezo wa kufikiri, ni kawaida sasa uwezo wa kufikiri unaingiliwa zaidi na cheo. Na ndio maana mwanamke amekuwa akikimbilia cheo bila ya kuhisi au kufikiria taathira mbaya kwa jamii nzima.

 

Muda atakapoanza mwanamke kukubali kuwa kila afanyacho mwanamme ni bora, vyote vitakavyofuata ni kujibeza na kujiona kuwa hayupo sawa. "Kama mwanamme anacho na sisi tunakitaka" Kama mwanamme amekuwa akifanya kazi, wanahisi kuwa hilo ni bora na hivyo kutaka kuwa mbele katika kazi hata zisizoshabihiana na maumbile yake mwanamke au hata kuingia katika biashara haramu. Hukaa hadi kufikiria kuwa kama wanaume wanasalisha, basi Imam (mwanamme) yupo karibu na Allaah.

 

Kwa njia hizi, wanawake wamejikubalisha na hisia ya kwamba uongozi hapa duniani ni bora kuliko kuwa na cheo chao pekee mbele ya Allaah. Muislamu wa kike hahitaji kujidhalilisha, lazima atambuwe kuwa anaye Allaah kama mfano wake. Anaye Allaah wa kumpa cheo chake, hapa hahitaji mwanamme.

 

Kwa kweli, vita hivi vya kumfuata mwanamme, wanawake hawajakaa kuangalia kuwa walivyonavyo ni bora kwao. Na katika kadhia nyengine, mwanamke amekubali hata kuutupa utukufu wake kwa sababu tu ya kuwa sawa na mwanamme. Yule konda wa kike akibakwa na kukashifiwa atamlaumu nani? Mbona hatusikii konda wa kiume kubakwa?

 

Miaka hamsini iliyopita, mwanamme alionekana kuondoka nyumbani kwenda viwandani. Na mwanamke wakati huo akiwa nyumbani kama mama. Na wakati huo huo mwanamke alijua fika kuwa mwanamme anakwenda viwandani kwa ajili yake yeye, akaona kana kwamba ni ukombozi wa mwanamke kuacha kumsimamia kiumbe chengine (mtoto) ili tu kufanya kazi viwandani. Amekubali kuwa kufanya kazi ni lazima, na cheo ni bora kwani tu inanyanyua upande mdogo wa msingi wa jamii. Hii yote ni kwasababu mwanamme anafanya na mwanamke anataka kuiga.

 

Jamii inashindwa kuelewa taathira ya kazi hiyo, kwani bado mwanamke anatarajia kuwa kiumbe aliye bora, mama bora, mke bora, mfanyakazi mzuri wa nyumbani na mfanyakazi bora wa kike. Yote haya anatarajia yeye kiumbe mmoja mwanamke. Ingawa kwa kweli hamna kosa lolote, kwa maana ya mwanamke kuwa na kazi, lakini baadaye mwanamke anakuja kutambua kuwa amejitoa sadaka kwa upofu wake wa kumfuata mwanamme.

 

Tunaangalia tukiwaona watoto wakikulia kuwa na tabia za maajabu, na baadaye tunatambua ni namna gani watoto wetu wangekulia kama mama angemsimamia vilivyo mtoto wake. Kwa mnasaba wa utandawazi, Jamii inaanza kuangusha lawama kwa kuporomoka maadili. Na kwa vile utandawazi ni wa jinsia zote, lawama ni za wote. Na kwa vile utandawazi haushughulishwi na uchaguzi wa kazi kwa jinsia, lawama zaanzwa kushushwa kwa wanaume pia, wakae ndani kupika na kulea watoto kama wafanyavyo wanawake.

 

Namna hoja zitakavyotolewa, ni kweli kuwa mwanaume ana wajibu wa kuchangia malezi kwa kuwa karibu na mtoto wake. Mtoto halelewi na mzazi mmoja tu, ni mashirikiano ya baba na mama, wote wawili kwa wakati mmoja. Lakini kati ya mwanamke na mwanamme, ni nani mwenye nafsi na maumbile ya kulea mtoto akakulia kuwa ni mtoto wa kweli? Ni baba au mama? Ukweli ni kuwa mama. Au Allaah alikosea kumpatia maumbile ya kumnyonyesha mtoto kupitia kwa mwanamke? Kwa wanavyojidai kupigania "jinsia sawa" ilibidi mwanamme na mwanamke wote wawe na maumbile ya kumnyonyesha mtoto.

 

Ni wanawake wangapi wanaomba kubaki nyumbani na watoto wao, lakini wanalazimika kuwa kazini kutokana na "umuhimu wa fedha". Mwanamke wa leo ameshughulishwa kufanya kazi sio tu kwa ajili ya familia yake, bali ni kukua kwa matumizi yasiyo na msingi. Ni fedha ngapi yaenda kwa saluni? Ni fedha ngapi zaenda kwenye sherehe zisizo na maana katika misingi ya Uislamu? Mwanamke amefunguliwa saluni, duka la nguo za mitindo ya Magharibi na mengineyo zaidi. Akili ya mwanamke imeelekezwa huko bila ya kuifikiria jamii kwenye matatizo ya mayatima na maeneo ya kusomea. Yareti kama mwanamke atakuwa na maisha ya wastani, atatumia muda wake mwingi kumtumikia mtoto na sio kazi. Mwanamke mjinga ni yule afanyaye kazi kutwa, na kumaliza muda na pesa zake kwenye saloon, parties na trips akimwacha mtoto wake kulelewa na nyanya.  Umuhimu huu unalazimishwa zaidi na hisa za "jinsia sawa" kutoka Magharibi ambao umemuondoshea mwanamke wa Kiislamu dhana ya cheo cha mwanamke kwa kigezo cha "tofauti za jinsia" na sio "jinsia sawa".

 

Imewachukua karibu karne moja wanawake wa Kimagharibi kutambua cheo cha mwanamke. Ambapo ndani ya Uislamu, mwanamke ana cheo chake takriban miaka zaidi ya 1,400 iliyopita. Mwanamke atakuwa dhalili pale atakapohitaji kuwa na cheo kilicho sawa na mwanamme. Na kusema ukweli, hahitaji kuwa sawa na mwanamme. Kwani, mwanamke wa kweli, hatofikia ukombozi halisi wa mwanamke hadi pale atakapoacha kujilinganisha na mwanamme kwenye mambo yasiyo na msingi. Hii ni kwa sababu, mwanamke ana cheo na utukufu wake kutokana na tofauti yake na mwanamme. Cheo kilichotunukiwa kutoka kwa Mola.

 

Kwa yule mwenye akili, daima atachagua uadilifu dhidi ya uhuru. Hali kadhalika, baina ya uongozi wa dunia na pepo chini ya nyayo, atachagua pepo.

 

Namna utakavyoenda Mashariki, ndivyo utakavyoipa mgongo Magharibi. Namna utakavyokuwa na shughuli za kuitumikia Dunia ndivyo utakavyokuwa mbali na Aakhirah. Na ndio maana kila mwanamke akitumikia kazi anakuwa mbali na mtoto. Kipi muhimu zaidi baina ya nafsi ya mtoto na fedha za ziada? Daima nafsi ya mtoto itakuwa juu. Kumbuka kuwa mwanamke ana cheo kikubwa kwa ulezi wake uliojaa huruma, uadilifu, subira na hekima. Hakuna utajiri kuliko kukinai. Mwanamke aparamie ngazi moja baada ya nyengine, afanye kazi mithili ya punda kwa ajili ya pato la dunia. Lakini daima akumbuke kwamba, mtoto ndio kigezo chake kwa jamii anayoishi. Akimharibu, amejiharibia, akimchunga, amejichunga.

 

Share