Wazazi Wanamkataa Aliyekuja Kumposa Kwa Sababu Ya Umasikini, Je, Nini Hukmu Yake

SWALI:

 

Assalam aleykum..

 

Napenda kuuliza swali langu hili, mimi ni msichana na naishi marecani pamoja na wazazi, nimepata mtu ninae taka kufunga ndoa nae kwa uwezo wa allah lakini mtu huyu anaishi africa na hana uwezo wa kuja hapa ninapoishi, na mimi bado sijawa na uwezo kwa kumsaidia kusafiri nilipo. Kwa kua mimi ni msichana nimeona ni uraisi kumuelezea mama yangu lakini kanikatalia amesema siwezi kufunga ndoa na mtu aliye kua maskini, mwenzangu ashawajuulisha wazazi wake sasa wanataka waje kwa wazazi wangu lakini mimi nasema bado kwa sababu naogopa watakataliwa. Najua wazazi wanahaki ya kuchagua nani akuowe, na wanatizama mambo mingi katika mchumba huyu je umasikini umo katika mambo yanayo tizamwa na ni haki hii maskini kukataliwa kuoa mtu mwenye uwezo.

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuolewa na mwanamme aliye masikini.

Labda kabla ya kuingia katika kukataliwa na wazazi kuhusu kuolewa na mwanamme huyo, tungependa kukuuliza unamjua vipi kijana huyo ilhali wewe upo Marekani? Je, unamjua kwa kuwa umemsikia kutoka kwa marafiki zako au mmekutana ndio ukampenda? Je, umempenda kwa sababu ya uzuri wake au umempenda kwa sababu ipi?

 

Mara nyingi hushindwa sisi kuchagua mume aliyependekezewa katika shari’ah kisha huja tukajuta baadaye. Ni vyema kabla ya kuendelea mbele mwanzo utazame sifa zifuatazo kwa huyo kijana kama anazo:

 

1.     Awe ameshika Dini ya Kiislamu vilivyo.

2.     Awe na maadili mema na tabia nzuri.

3.     Awe ameepukana na maasiya ya aina yote. 

 

Ama katika ndoa ya Kiislamu, mali haiaizamwi kama sifa inayohitajika kwa kijana kupata mke, japokuwa kwetu ndio tumeweka kama kigezo muhimu sana. Kama mali ndio kigezo basi Swahaba ‘Abdullaah bin Mas‘uud, Julaybib, Zayd bin al-Haarithah na wengineo (Radhiya Allaahu ‘anhum) hawangepata wake. Hasa Swahaba Julaybib (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa hajulikani baba yake wala nasaba yake, hajulikani alikotoka lakini akamuoa msichana wa Ki-Answaar mwenye nasaba na utajiri.

 

Na pia wazazi hawana haki ya kumchagulia mume msichana wake japokuwa wana haki ya kumpatia nasaha ili asiwe ni mwenye kudhulimika katika ndoa hiyo. Na tufahamu kuwa masikini huweza kutajirika na tajiri kufukarika. Hilo tunatakiwa tulifahamu vyema.

 

Hata hivyo ni bora kuwatii wazee kwani ndoa kama hiyo huwa haina raha japokuwa kisheria mnaweza kuoana na fungamano lenu likawa halali kabisa. Hata hivyo, utakuwaje wewe uwe unaishi na mumeo ambaye hawezi kwenda kwenu wala kuwa na mahusiano mazuri na wazazi wako.

 

Njia ambayo unaweza kuitumia ili kufikia lengo hilo ulitakalo ni kuwatumia mashaykh ambao wanaweza kwenda kuwaeleza wazazi wako kuhusu ndoa ya Kiislamu inavyotakiwa iwe na pia uchaguzi wa msichana anayeolewa. Au pia unaweza kuwatumia jamaa zako ambao wanakubaliana na ndoa hiyo ili waweze kwenda na kuwakinaisha wazazi wako kuhusu uchaguzi wako.

 

Tunakuombea kila la kheri na tawfiki katika yaliyo na kheri nawe hapa duniani na Kesho Akhera.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share