Ameniapia Kuwa Hakuoa Mke Mwingine Nami Nimesikia Kuwa Kaoa Kisiri Sasa Inafika Miaka Miwili – Nishike Yepi?

SWALI:

 

kuolewa siri na kufichwa mke aliekuwepo ndani ya ndoa mpaka yule mke apate habari na watu wengine ni sheria? kwani mume wangu ameoa na mimi hajaniambia lakini nimepata habari sio za kubuni bali ni za uhakika. Lakini mpaka hii leo hajanambia na sasa inakaribia miaka 2 na huyo mwenzangu tunaishi vizuri bila matatizo. kwa kuwa mwenzangu tunaishi vizuri hajaniambia cha kushangaza mimi nilimuuliza kwa kuwa tayari tupo pamoja miaka 50 nilipomuuliza amenambia hajaowa ila alitaka kuowa kwa shinikizo la ndugu zake na amaapa kwa Mnyezi MUNGU kuwa hajaowa je sasa mimi nishike yepi kwani nakosa raha na ndoa yangu.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ndoa ya siri na uke wenza. Hakika ni kuwa katika Uislamu hakuna ndoa ya siri kwa maana ya mume na mke mtarajawa wakubaliane kisha imalizike hivyo. Bali ndoa kama Ibadah nyingine ina masharti yake. Miongoni mwa masharti ni:

 

  1. Kuwepo kwa walii wa msichana.

  2. Kuwepo mashahidi wawili waadilifu.

  3. Kukubali kwa mume na kumpatia mahari mke.

  4. Kukubali kwa mke mwenye kuolewa.

 

Kwa jinsi hiyo hakutakuwa na siri yoyote. Ila hii ndoa ya siri inavyoeleweka huku Afrika Mashariki na haswa Kenya upande wa Pwani ni kuwa mume anakwenda kuoa bila kualika wala kumuambia mkewe anatimiza masharti kwa kiwango cha chini. Ndoa kama haina tatizo bali ni vyema kwa ndoa kualikwa kama alivyotushauri Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam). Na katika mume kuoa mke wa pili si lazima amtake shauri, au amwambie mke wake wa kwanza, yeye anaweza kuoa bila ya kufanya hayo lakini ni katika wema na ihsani kumwambia mwenziwe haswa ikiwa mumeishi kwa muda mrefu kama mlivyo nyinyi.

 

Jambo la wewe kuamini ni kuwa ikiwa mume amekuambia kuwa hajaoa muamini yeye wala usipeleleze  kwani kufanya hivyo kutakuingiza wewe katika haramu. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Enyi mlioamini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi” (al-Hujuraat [49]: 12). Sahau kamwe kama uliwahi kumtajia mumeo kuhusu kuoa kwake mke wapili.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share