Mirathi - Kaka Amefariki Ameacha Mama Mke Ndugu

SWALI:

 

Naomba kuuliza kuwa kaka yangu amefariki ameacha mke na mtoto mmoja na aiyefariki ameacha gari aina ya pickup tani 3 ila mpaka sasa gari yake ilianguka baada ya kifo chake kwa wiki 1, ndo tuko katika mipango ya kuitengeneza na likishatengenezwa tutaliuza kama milioni 4 ili tuanzae mipango ya kugawa urithi, swali langu ni hili katika kugawa urithi nani ambaye anaestahiki kupata ulithi zaidi, je na mke wake atagawia urithi? je na mama yetu pia anapata kiasi gani? nashukuru kama mtanijibu.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu mirathi. Mama mzazi anarithi sudusi (1/6) ya mali iliyoachwa na aliyefariki kwa mujibu wa Qur-aan:

Na wazazi wake wawili, kila mmoja wao apate sudusi ya alichokiacha, ikiwa anaye mtoto” (4: 11).

 

Mke aliyefiliwa na mumewe anapata thumuni (1/8) kwa mujibu wa mgao wa Qur-aan:

 

 

Na wake zenu watapata robo mlichokiacha, ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumuni ya mlichokiacha” (4: 12).

 

 

Ndugu wa aliyefariki hawatakuwa ni wenye kurithi chochote kwa kuwepo kwa mtoto wa aliyefariki. Hivyo, kitachobakia atapatiwa mtoto.

 

Tufahamu kuwa mgao huu ni baada ya kulipiwa madeni aliyokuwa nayo aliyefariki, kutoa pesa za mazishi na kama ameacha wasiya. Ikiwa hilo gari umesema linatengenezwa, gharama hiyo itatolewa kutoka kwa pesa hizo lakini ikiwa mtasaidia itakuwa ni kheri na thawabu kutoka kwenu.

 

 

Tunawaomba muwe na subira na uvumilivu kwa kuondokewa na kipenzi chenu na alipwe mema nanyi pia.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

 

 

Share