Amefariki Hana Wazazi Wala Mke Wala Watoto Anao Ndugu

SWALI:

 

ASSALAAM ALAYKUM

 

AMEFARIKI HANA WAZAZI WALA MKE WALA WATOTO  A-WALIO CHANGIA NA ALIYEFARIKI BABA NA MAMA NI WANAWAKE WATATU TU  B-WALIO CHANGIA BABA TU NA ALIYEFARIKI NI MWANAUME MMOJA NA WANAWAKE WATATU.

 

JAZAAKUMULLAAH KHAIR - WABILLAAH TAWFIQ

 

Assalaam alaykum,

 
Nashukuru sana kwa kulitilia hima suala langu. Ningependa kujua jinsi ya kuigawa mali ya aliyefariki kwa wanandugu wanaostahiki kisheria kurithi mali ya kaka yao. Ikiwa ni fedha taslim pamoja na nyumba. Kama nilivyoelezea kuwa aliyefariki AMEACHA NDUGU WALIOCHANGIA MAMA NA BABA WATATU AMBAO NI WANAWAKE TU. Na amewacha NDUGU WA BABA MMOJA WANNE, KATI YAO MMOJA NI MWANAUME NA WATATU NI WANAWAKE. Natumai swali langu liko wazi.

 
Jazaakumullah khair wabillaah tawfiq


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Mirathi iliyoachwa na kaka aliyeaga dunia. Na hili swali tayari tutumelijibu hapo mbeleni na sijui kama jibu halikueleweka au vipi lakini naona ni kama vile awali isipokuwa limefafanua kuwa aliyefariki hana wazazi, mke wala watoto. Swali lako ni kuwa jamaa wa aliyaefariki waliobaki ni kama wafuatao:

 

1.     Dada watatu shaqiqi (kwa baba na mama).

2.     Dada watatu kwa baba, na

3.     Kaka kwa baba tu.

 

Urithi wa jamaa wa aliyefariki ni kama katika jadwali ifuatayo:

 

 

Namba

Uhusiano na Aliyefariki

Mgao

1

Dada Shaqiqi 1

2/9 (22.222)

2

Dada Shaqiqi 2

2/9 (22.222)

3

Dada Shaqiqi 3

2/9 (22.222)

4

Dada kwa Baba 1

1/15 (6.667)

5

Dada kwa Baba 2

1/15 (6.667)

6

Dada kwa Baba 3

1/15 (6.667)

7

Kaka kwa Baba

2/15 (13.333)

 

JUMLA

1 (100)

 

Kwa vitu vilivyobaki vya kurithiwa ni nyumba na fedha taslimu alizoacha aliyefariki. Fedha taslimu zitagawanywa kulingana na mgao ulio hapo juu, ama nyumba itategemea wanavyoona warithi. Inaweza kuajirishwa, na ijara inayopatikana igawa kwa mgao kila mmoja haki yake, au inaweza kuuzwa na pesa kupatiwa kila mmoja anachostahiki au mwenye uwezo akainunua miongoni mwa ndugu kisha hizo fedha zilizopatikana kwa njia hiyo kuweza kugawiwa kila mmoja.

 

Ikiwa ni nyumba kubwa ambayo inaweza kugawiwa kila mmoja bila matatizo na kila mmoja akapata haki yake anayostahiki kutakuwa hakuna matatizo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share