Mume Kutamka 'Kila Mtu Ajue Maisha Yake' Ina Maana Ni Talaka?

 

SWALI:

Napenda kutuma fursa hii katika huu mtandao kuweza kuuliza wali ili na mimi niweze kupata ufafanuzi zaidi na kuelewa hususan kuhusiana na ndoa.

Je kama mume na mke wamekaa tofauti kwa muda wa mwaka na zaidi (nchi tofauti) na palikuwa na mgogoro kati ya hao watu wawili na ikatokea ya kwamba mmoja wapo akamuandikia mwenzake barua pepe kwa kusema "kila mtu ajue maisha yake" na kutokea wakati huo watu hawa hawana masiliano takriban mwaka mzima. Watu hawa ni bado wanandoa???

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali la ndugu yetu. Hakika ni kuwa swali lako halipo wazi kwani umesema: ‘mmoja wapo akamuandikia mwenzake’. Sasa huyu aliyeandika ni mume au mke. Ikiwa ni mke basi barua yake hiyo haitakuwa na maana yoyote wala haitakuwa ni talaka kwani talaka ni haki ya mume. Ikiwa ni hivyo mume atabeba dhambi ya kutomtazama na kumtimizia haki za mkewe.

Kutokuwa na mawasiliano haimanishi kuwa talaka imetuka baina yao lakini ikiwa alyeandika ni mume ibara hiyo: ‘kila mtu ajue maisha yake’ itategemea na niya yake kwani maneno hayo hayapo wazi. Talaka kupita na kuhesabiwa ni lazima yawe kwa maneno yaliyo wazi kama nimekutaliki, wewe si mke wangu na mfano wake. Ni lazima mke amuandikie mumewe kuhusu hilo au ampigie simu na apate ufafanuzi wa kihakika. Akipata ufafanuzi ndio mke atapata uhakika kama yeye bado ni mke au si mke wa mtu. Lau itakuwa ni talaka basi mke ana haki ya kupatiwa na mume masurufu ya chakula, matibabu, malazi wakati wa eda yake.

Talaka haiwi imepita mkikaa mbali mbali kwa muda hata ikiwa ni miaka miwili au mitatu mpaka talaka itolewe.

 

Twawatakia kila la kheri na fanaka na mrudiane kwa masikilizano au muachane kwa wema.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share