Talaka Tatu Pamoja Inakubalika? Mume Hatimizi Zamu Kisha Ametoa Talaka Mara Tatu Kwa Pamoja

SWALI:

natumai munaendelea vizuri na kufahamisha waislamu kama kawaida Naomba niulize suala jengine lakinisa siri ndani ya
nafsi yangu kuhusu ndoa.
Kama nilivyouliza hapo nyuma kuwa mume wangu ana mke mwengine ambae alitoa masharti kwamba mume wangu asijezamu kwangu. yaliyotokea ni kama ifuatavyo alikaa miezi 3 hajaja kwangu kubwa anamuhudumia mtoto wake kama kawaida lakini alipokuja nilikasirika

sana na mwisho ananiambia nimekuacha mara 3. Hivyo sheikh wakati wa hasira talaka inasihi? Naomba majibu haraka iwezekanavyo ahsante muislam mwezenu.


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'Alayhi Wa Aalihi Wasallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'Anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Mwanzo ni makosa kwa mume kuoa mke wa pili kisha akawa hamtimizii mahitajio yake hasa kumgawia siku. Na mke mkuu hafai kuweka sharti ambalo linakwenda kinyume na sheria ya Allah na mume naye akafuata, kwani hii ni dhulma kwa mke na dhulma ni jambo ambalo halifai katika Dini. Allah (Subhaana Wa Ta'aalah)  Anasema:

((وَإِن جَاهَدَاكَ عَلى أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا))

((Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwatii)) (31: 15).

Hapa Allah Ametutajia kuhusu shirki lakini pia inaingia dhambi lolote ambalo Muislamu haifai kumtii kiumbe anapotakwa kufanya hayo. Na Mtume  (Swalla Allahu 'Alayhi Wa Aalihi Wasallam) anatuweka wazi kabisa pale aliposema: “Hapana utiifu kwa kiumbe ikiwa utiifu huo utakwenda kinyume na aliyoamrisha Muumba”.

Talaka inapita kwa wanazuoni wengi pindi mume mwenye kuitoa akiwa na akili timamu, kwa hiari yake na amebaleghe, lakini akiwa ni mwenda wazimu, mtoto au amelazimishwa basi talaka haipiti. Sasa tukija kwa talaka ya aliyekasirika (mwenye ghadhabu) lakini yule ambaye hajui kabisa anachosema wala hatambui kinachotoka, talaka huwa haipiti.

Amepokea Ahmad, Abu Dawud, Ibn Maajah na al-Haakim, ambaye ameisahihisha kutoka kwa ‘Aishah (Radhiya Allahu 'Anha) kuwa Mtume (Swalla Allahu 'Alayhi Wa Aalihi Wasallam)  amesema: “Hakuna talaka wala kuacha huru (mtumwa) katika Aghlaaq”.

Na Aghlaaq imefasiriwa kuwa ni ghadhabu, na pia kutendesha nguvu, na pia imefasiriwa kama uenda wazimu. Na Ibn Taymiyah amesema kama ilivyonukuliwa katika Zaad al-Ma‘aad: “Hakika ya al-Ighlaaq ni mtu kufunga moyo wake na wala asiwe ni mwenye kukusudia maneno au pia asiwe ni mwenye kujua kama kwamba imefungwa kwake lengo lake na uamuzi wake. Na inaingia katika hilo talaka ya aliye lazimishwa, na mwenda wazimu, na aliyepoteza akili yake kwa sababu ya vileo (mlevi) au ghadhabu (hasira) na kila ambacho hukukusudia wala huna maarifa nacho kwa ulichosema”. Na wanachuoni wameigawanya ghadhabu sehemu tatu:

1. Kuwa ile ghadhabu ni mwanzoni wa jambo lake, haibadilishi akili ya mwenye hasira kwa kuwa anakusudia kwa anayosema na anayajua. Na bila shaka kuwa talaka kwa maana hii ya ghadhabu inapita kwa kukubaliwa na wanachuoni wote.

2. Ni ile ambayo ghadhabu inakuwa mwisho na inaharibu akili yake na kumfanya kama mwenda wazimu ambaye hakusudii anayoyasema wala hayajui. Ghadhabu kwa maana hii haipiti kwani yeye na mwenye wazimu ni sawa.

3. Hii ni ghadhabu ambayo ipo katika hali hizo mbili za juu. Anakuwa mkali na anatoka katika ada na ukawaida wake lakini hawi kama mwenda wazimu, ambaye hakusudii anacho sema wala hajui. Na rai ya Jamhuur ni kuwa talaka hii inapita (Abdur-Rahmaan al-Juzayriy, Kitaabul Fiqhi ‘Alal Madhaahib al-Arba‘ah, Mj. 4, uk. 294).

Baada ya kusema haya inatakiwa ifahamike kuwa talaka si kitu cha mchezo na kinatakiwa kitolewe katika hali ya utulivu wa roho na mwili. Na ndio Mtume (Swalla Allahu 'Alayhi Wa Aalihi Wasallam) akatuusia kuwa tusighadhike, na akalikariri hilo mara kadhaa (Al-Bukhaariy kutoka kwa Abu Hurayrah [Radhiya Allahu 'Anhu]). Na pia ikiwa tutakasirika nasi tumesimama, basi tukae. Ikiwa itaondoka sawa lau haitaondoka basi jilazeni (Abu Daawuud kutoka kwa Abu Dharr [Radhiya Allahu 'Anhu ])

Hivyo, ni nasaha kwa waume wasiwe ni wenye kutoa haraka talaka kwa wake zao kisha wakawa ni wenye kujuta, kwani hakuna mchezo na talaka. Na lau talaka hii itapita kwa sababu hatujui hali ya mume wako katika ghadhabu yake itahesabiwa kuwa ni talaka moja na wala sio tatu, hivyo mna uwezo ikiwa mnataka kuishi pamoja kurudiana kabla ya kupita eda bila kufungwa nikaha nyengine. Ikiwa eda itapita basi itabidi mume ikiwa anamtaka kumrudia mkewe, afuate njia kama ya awali kwa kumposa na kumpatia mahari, kwani hii inakuwa ni ndoa mpya.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share