Mwito Kutoka Masjidul-Haraam Kwa Wanawake Wote Waislamu Ulimwenguni!

Mwito Kutoka Masjidul-Haraam Kwa Wanawake Wote Waislamu Ulimwenguni!

 

Shaykh 'Abdur-Rahmaan As-Sudaysiy

 

Imefasiriwa na  Ummu 'Aliy

 

 

Sifa zote ni za Allah, Mwingi Wa Rahma Mwenye Kurehemu. Swalah na salaam zimshukie Mtume Muhammad صلى الله عليه وسلم.
 

Dada zangu Waislamu, hamutaweza kufikia ukamilifu munaotaka, hamutaweza kurudisha taadhima ya kale, wala kufikia daraja ya juu kabisa, isipokuwa mukifuata mafundisho ya Kiislamu na musipite mipaka ya shariy'ah. Hii itawafanya nyoyo zenu zipende na kuthamini mitindo mizuri na kuepukana na mitindo mibaya.

 

Kaeni Kwenye Majumba Yenu:

 

Mtasifiwa na Allah, mtaifurahisha jamii yenu na majumba yenu yatakuwa ni yenye furaha.

 وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ الْأُولَى وَأَقِمْنَ الصَّلَاةَ وَآتِينَ الزَّكَاةَ وَأَطِعْنَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ...

33. Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya kijahilia ya kizamani. Na simamisheni Swalaah, na toeni Zakaah, na mtiini Allaah na Mtume Wake … [Al-Ahzaab:  33]

 

Mtakamilisha hijabu zenu, utakaso wenu, na mtakuwa na furaha nyinyi wenyewe, na mtaneemeka.

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاء الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ذَلِكَ أَدْنَى أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا

 

 "Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu". [Al-Ahzab: 59]

 

Uislamu unawakinga dada zangu wa Kiislamu, bila ya Uislamu, mtakuwa kama kitu cha kuchezewa, na mtakuwa kama mali ya kuuzwa, mikononi mwa binaadamu mbwa mwitu, ambao wataangamiza takaso lenu, heshima yenu, na hadhi yenu, kisha wawatupilie mbali na kuwapuuza kama anavyofanya mtu tende na  kokwa yake.

Kwa hivyo, kila mwanamke akitupilia mbali mafundisho ya Kiislamu na kuacha mavazi ya Kiislamu, kuchukulia wepesi mambo ya hijabu kwa kudhihirisha uzuri wake kwa wanaume, kutembea kati yao na kujitia manukato, heshima yake na hadhi yake na nuru yake hupotea. Hadhi yake hudhii na akawa chanzo cha fitna kwa watu na maovu humkumbatia.
 
Ilimradi ewe mwanamke wa Kiislamu, ambae unakamata heshima ya Uislamu na uko radhi nayo, na ewe mwanamke uliye huru, uliyeheshimika, na uliyekingwa, wewe ni mrithi bora wa kizazi cha Waislamu kilichopita, shikamana na Kitabu cha Allah na Sunnah za Mtume Muhammad صلى الله عليه وسلم . 

 

Jitahadharini na mikono ya watu waovu, macho yenye wivu, na watu wenye tabia mbaya na roho chafu, ambao haja yao ni kuwashukisha kutoka kwenye daraja zenu za juu za heshima na makini, wawatoe kwenye raha muliyonayo.

 

Na jitahadharini na uongo na kushindwa katika vita vya hijabu na kuonesha uzuri, na katika takaso na kuwa huru. 
 
Maadui wa Waislamu, wakiwemo Mayahudi na wafuasi wao, wanahangaika na kukosa usingizi kwa sababu mwanamke wa Kiislamu ameheshimika, amemakinika, na amekingwa, kwa hivyo wanamueka kwenye muangaza, wanamtega kwenye nyavu na kumrushia mishale. Juu ya hivyo, ni ajabu kuwa watu wengine ambao ni jamaa zetu, wanawafuata na  kusambaza fikra zao na kunufaisha dhamira zao, hivyo wanazua vita dhidi ya dada zetu Waislamu ambao ndio rutuba ya nyuso zetu kwa kuandika mambo ya uongo na misemo ya udanganyifu hapa na pale.  

 

Vile vile, wanawadanganya na kuwaita wanawake eti wawe huru kwa kuwaambia na kuwalazimisha kimpango watoke majumbani mwao wakafanye kazi. Wanaeneza fununu mbali mbali kuhusu wanawake wa Kiisalmu.
 
Wanataka wanawake wawe huru, lakini, ukweli ni kwamba wanataka kuwaondoa kwenye tabia yao nzuri ya Kiislmau na kuwabambulia kanuni yao ya heshima na staha na kuwalekeza kwenye balaa na ufisadi. Wanataka mwanamke wa Kiislamu awe modeli wa fesheni na kitu cha kuuzwa kwa watu wenye akili duni.

 

Nani ataachiwa maslaha ya majumba, furaha ya familia, kukuza na kuelimisha watoto?
 
Wasichana wangapi wadogo wadogo wanategwa, na athari ngapi zinatokea hijabu ikipuuzwa na jilbabu ikivuliwa? Wanaume waovu wanafaidika kwa kuwaangalia wasichana hao. Hayo ni matokeo ya kuonyesha mapambo na kutangamana kwa wanawake na wanaume makazini, mashuleni, na masokoni.

 

Haitoshi kuwa makumbusho jamii zilizopita, ambazo zilitupilia mbali mafundisho ya Kiislamu, zilitumbukia kwenye uchafu na uhayawani? Baada ya matokeyo hayo, ni lazima turudi nyuma na kutaka wanawake wetu warudi kwenye maboma yao yaliyohifadhiwa; yaani nyumba zao.

 
Yuko mwanamume yeyote, ambae ana chembe ndogo ya staha ambae aneweza kuwa na utulivu wa moyo akijua mke wake amekuwa 'lisho' la macho ya wanaume waovu, na 'mlo juu ya meza'? Hali ya sasa ya baadhi ya jamii, inashuhudia kuwa mwanamke akitoka nyumbani kwake, ni ishara ya uharibifu, hasara, ufisadi, na kuenea kwa shari na uchafu katika jamii.

 

Kwa hivyo, kwa dada zangu wote wa Kiislamu, walioko mashariki na magharibi mwa ulimwengu wa Waislamu, nawaita kutoka kwenye nchi hii iliyo Takatifu na Safi, Makkah, mshikamane na Qur-aan, na mshikamane na Sunnah ya Mtume Muhammad صلى الله عليه وسلم  kwa magego, na mfuate mafundisho ya Kiislamu na nidhamu zake. 

 

Na kwa vyama vya wanawake ulimwenguni, jitahadharini na ujinga na matokeo ya uhalifu wa wanawake kwa kutofuata muongozo wa Kiislamu. Jihadharini kushawishiwa na miito ya kutangaza matangazo yenye sumu, ambayo yanakwenda kinyume na tabia ya mwanamke wa Kiislamu na kanuni yake.

 

Na kwa wale wanaoshirikiana kumhudumia  mtoto wa Kiislamu wa kike, nawaita mumuogope Allah سبحانه وتعالى , na mutimize wajibu wenu kwao (hao watoto wa kike) kwa kumuangalia kwa uzuri na kumchungia heshima yake.

 

Mpaka wa wazi ni  lazima uwekwe dhidi ya uchafu, sinema mbaya, na picha za watu walioko tupu tupu, ambazo zinatokomeza hadhi na uzuri, na zinazokuza  na ufisadi.

 

Na kwa walinzi wa wanawake, baba, waume, na kaka, nawakumbusha jukumu lenu kwa wanawake kulingana na yale Allah سبحانه وتعالى Amesema:   
 

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاء بِمَا فَضَّلَ اللّهُ بَعْضَهُمْ عَلَى بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُواْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللّهُ وَاللاَّتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلاَ تَبْغُواْ عَلَيْهِنَّ سَبِيلاً إِنَّ اللّهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا

 

"Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Allaah baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayoyatoa. Basi wanawake wema ni wale wenye kutii na wanaojilinda hata katika siri kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajilinde. Na ambao mnachelea kutoka katika utiifu wanasihini, muwahame katika malazi na wapigeni. Wakikutiini msiwatafutie njia ya kuwaudhi bure. Hakika Allaah ndiye Aliye juu na Mkuu." (Surah An-Nisaa 4:34)

 

Kwa hivyo ni lazima wamuogope Allah سبحانه وتعالى na wajilinde wao na watoto wao kutokana na Adhabu za Allah سبحانه وتعالى kwa kuwakuza na kuwaelimisha watoto wao kulingana na mafunzo ya Kiislamu. Lazima watahadharishwe na kupuuza mambo haya. 

 

Kwa hivyo, enyi watu wenye busara, chukueni fundisho na mukae chonjo, aliyefuzu ni yule anaefundishika kwa makosa ya watu, na mujue kuwa ummah umefika wakati wa kusikitisha na matatizo yametokea kwa ajili ya kupuuza kuwakuza watoto wa kike kwa njia ya Kiislamu. Na kumbukeni Mtume صلى الله عليه وسلم amesema:

"Sijaacha fitnah kubwa baada yangu kwa wanaume kama wanawake (wakienda kinyume na mafundisho ya Kiislamu)." [Al-Bukhariy na Muslim].

 

Swalah na salaam zimshukie Mtume Muhammad صلى الله عليه وسلم.

 

Share