Skip navigation.
Home kabah

Inafaa Kutokuvaa Hijaab Kwa Khofu Ya Wazazi Wake Kujua Kama Kasilimu?

 

SWALI:

Shukrani zote zinamstahikia M/Mungu, kuna mwanafunzi mwenye asili ya kihindi anayeendlea na masomo yake nchini urusi amesilimu na hataki wazazi wake wajue ili kukamilisha azma hiyo ameamua kutojitofautisha kama alivyo kuwa mwanzo ikwa pamoja na kutovaa hijaab, je inajuzu kufanya hivyo?

 

JIBU:

 

 

 


 

 

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu kwa swali lako. Mas-ala ya Dini ya hasa ya kuvaa Hijaab kwa mwanamke wa Kiislamu si mas-ala ya hiyari bali ni wajibu kwake akiwa ni Muislamu au amesilimu kutekeleza wajibu huo. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

 

 

((وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا))       

((Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Allaah na Mtume Wake wanapokata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Allaah na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi))   [Al-Ahzaab: 36]

 

Naye ikiwa amejisalimisha katika kukubali dini ya haki basi inampasa asiogope mtu yeyote ila Muumba wake pekee. Hivyo ni lazima athibitishe Uislamu wake na atambue kuwa ni kawaida ya wengi wanaosilimu bila ya wazazi wao kupatwa na mitihani kama hiyo. Kuvumilia na kuwa imara katika dini yake ya haki ni jambo linalompasa. Wazazi wake hawana majukumu naye tena katika mas-ala ya dini, bali ni yeye mwenyewe ajiamulie yanayompasa kutekeleza amri za Mola. Wazazi wanabakia kuwapa heshima yao na kuwafanyia ihsaan (wema) kama kawaida.

 

Ingawa wazazi wanayo haki kwako ya kuwatii amri zao, lakini haipasi kuwatii katika maasi au amri zozote za Mola Muumba. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

((وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَى وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ)) 

(( وَإِن جَاهَدَاكَ عَلى أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا وَاتَّبِعْ سَبِيلَ مَنْ أَنَابَ إِلَيَّ))

((Na Tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni Kwangu Mimi ndiyo marudio))  

((Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwatii. Lakini kaa nao kwa wema duniani, nawe ishike njia ya anayeelekea Kwangu)) [Luqmaan:14- 15]

 

Maswahaba wa mwanzo kuingia katika Uislamu walipatwa na mitihani mikubwa zaidi ya mateso kutoka kwa Makafiri na wengine kutoka kwa wazazi wao lakini hawakurudi katika ukafiri bali walithibitika katika Uislamu na kupokea hiyo mitihani ambayo ni kama majaribio ya kuhakisha Uislamu wa mtu:

 

  ((أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لَا يُفْتَنُونَ)) ((وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ))

 

((Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe?))   ((Hakika Tuliwajaribu waliokuwa kabla yao, na kwa yakini Allaah Atawatambulisha walio wa kweli na Atawatambulisha walio waongo)) [Al-'Ankabuut: 2-3]  

 

Ama kuhusu Hijaab Allaah Anatubainishia wazi kabisa pale Aliposema:

 

((يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاء الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ذَلِكَ أَدْنَى أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا)

"Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu "[Al-Ahzaab: 59].

Jambo muhimu la sisi kujiuliza je, Hijaab ya Kiislamu inafaa iwe vipi? Au masharti ya kivazi cha Kiislamu ni yepi? Masharti ni kama yafuatayo:

·         Vazi kuwa pana.

·         Kutoonyesha maumbile wala vilivyo ndani.

·         Kusitiri uchi.

·         Kutokuwa na mapambo aina yoyote.

·         Kutofanana na vazi la kikafiri.

·         Kutokuwa vazi la kujionyesha.

·         Liwe halifanani na vazi la mwanamme.

Ushauri wetu utakuwa ni yeye awe ni mwenye kuvaa vazi hilo pamoja na mtandio na aache na sare ambayo inayoonyesha tumbo.

Tunamuombea dada yetu kila la kheri aweze kuvuka mtihani huo kwa salama kabisa. 

Na Allaah Anajua zaidi