Mwanamke Aliyekwishaolewa Kabla - Anahitaji Walii? Na Ndoa Ya Pili Inaruhusiwa Kuwa Ya Siri

 

SWALI:

Mwanamke kaolewa na kashaachwa kakaa miaka 10 sasa anataka kuolewa na anataka kuolewa siri jee inatosha yeye mwenyewe kutoa idhini na kuwaita mashahidi pamoja na shekhe kwa ajili ya ndoa nb mwanamke huyo babayake yuko hai lakini huyu mume kampa masharti kuwa ni lazima iwe siri jee ndoa itafaa au haifai

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Hakika ni kuwa kila jambo katika Uislamu lina masharti kusihi kwake. Lau masharti kama hayo hayatatimia basi jambo au ‘amali hiyo inayofanywa haitakubaliwa. Kama ilivyo Swalah, Zakaah, Swawm na Hijjah, ndoa nayo ina masharti yake.

Miongoni mwa mojawapo ya masharti ya ndoa ni kupatikana kwa walii wa mwanamke, akiwa ni bikira au thayyib (aliyeolewa hapo mbeleni). Na haingii akilini haswa kwa Muislamu iwe ndoa itafanywa waalikwe mashahidi wawili na pia wamualike Shaykh wa kuozesha lakini baba asialikwe. Baba ni mtu muhimu na ndiye anayetakiwa atoe ridhaa katika jambo hilo na pia ndiye anayefungisha ndoa au ndiye anayemwakilisha Shaykh au mtu mwengine afungishe hiyo ndoa, na ndiye mshauri mkuu wa binti yake katika suala hilo muhimu la maisha yake.

Na katika sharti ya ndoa ni lazima kuweko walii kama Alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa Abu Muusa Al-Ash'ariyy (Radhiya Allaahu ‘anhu):

((Hakuna Nikaah ila kwa Walii)) [Abu Daawuud, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na ameisahihisha Shaykh Al-Albaaniy katika Sahihi ya At-Tirmidhiy]

Vile vile Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Mwanamke yeyote akiolewa bila ya Walii wake basi Nikaah yake ni baatil, Nikaah yake ni baatil, Nikaah yake ni baatil)) [Ahmad, Abu Daawuud, At-Tirmidhiy na kaisahihisha Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyhul-Jaami'i]

Kufanywa ndoa katika hali hiyo ni kuwa mwanamke anaficha kitu muhimu. Tuelewe ndoa kama hiyo haitakubaliwa katika sheria ya Kiislamu. Labda tukiuliza, kwa nini baba afichwe katika jambo muhimu kama ndoa?

Hivyo, nasaha kwetu kwa ndoa anayetaka kuolewa ni amfahamishe baba mzazi kabla ya shughuli hiyo.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share