Mume Anaweza Kuoa Kwa Siri Mke Wa Pili

SWALI:

 

Assalam aleykum warahmatullahi wabarakatu…..........

Swali langu ni hili kwamba baba yangu aliowa mke wa pili ila kisiri hakutuambia sisi wanae wala mama yetu ila aliwaambia ndugu zake tumekuja kujuwa baada ya kama mwaka hivi sasa swali langu linauliza ya kwamba je mume anafaa kidini kuoa kisiri bila ya kumwambia mke wake na kama haifai nini hukumu ya mwanaume anaeoa kisiri?


 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ndoa ya siri.

Hakika ni kuwa hili suala limekithiri kuulizwa katika tovuti hii ya alhidaya na pia katika darsa na mawaidha tofauti.

 

Ifahamike kuwa kidini mume halazimiki kumwambia mkewe wa kwanza, watoto wake na wengineo anapotaka kuoa mke wa pili au watatu. Ndoa kama ‘Ibaadah nyingine ina masharti yake lau yatatimia basi ndoa inakuwa ni sawa na mke wa pili halali ya mume huyo. Hata hivyo, ni katika utu na ubinaadamu kwa mume kumueleza mkewe wa awali kuhusu hilo.

 

Pia tufahamu kuwa katika Uislamu hakuna ndoa ya siri kwa maana ya mume na mke kuchukuana na kukaa pamoja. Ama ikiwa siri hii ni ya kumficha mke wa awali na hali masharti ya ndoa yamekamilika basi haitosababisha ndoa ile kuwa haraam. Lakini tujue pia kutangaza ndoa ni Sunnah na Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasisitizia kwenye Hadiyth. Lau katika ndoa kutapatikana masharti yafuatayo basi ndoa hiyo ni sawa kabisa kidini:

 

  1. Kuridhia mume kumuoa mwanamke huyo.

  2. Kukubali kwa mwanamke kuolewa na mume huyo.

  3. Kuwepo na walii wa mwanamke kama baba yake, babu yake kuumeni, kakake na mfano wao.

  4. Kuwepo na mashahidi wawili waadilifu.

  5. Na mume kulipa mahari waliyoafikiana.

 

Kukipatikana hayo ndoa hiyo inakuwa ni halali katika Uislam.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share