Aina Za Laana Na Wepi Waliolaaniwa na Allaah?

 

SWALI:

Kwanza kabisa namshukuru ALLAAH Sub haanahu wata'al. na kumtakia rehma Nabii Muhammad kiongoza wa Umma S.A.W.na Masheikh wote ambao usiku na mchana wako macho kujibu maswali yetu/ya waislaam.

Baada ya hapo ningependa kuuliza maswali yafuatayo.NI NANI HASWA ANASTAHIKI KUAMBIWA LAANA ZA ALLAAH ZIWE JUU YAKO. JE NI MAKAFIR AU MURTADINA AU WANAAFIQ? JE KUNA LAANA YA MTU MMOJA MMOJA UA WENGI WENGI?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mas-ala ya laana. Laana si kitu kumpata mtu yeyote yule na hasa akiwa ni Muislamu. Laana kutoka kwa Allaah au Mtume Wake inampata mwenye kuacha amri na yule aliyekengeuka na maagizo yao. Allaah Aliyetukuka na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) wametutajia watu waliteremshiwa laana hizo.

Hebu tutazame baadhi ya mifano:

 

a)            Allaah Aliyetukuka Anasema: "Hakika Allaah Amewalaani makafiri na Amewaandalia Moto mkali" (33: 64).

b)           Allaah Aliyetukuka Anasema: "Kama wanafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao na watangazao uovu mjini, hawataacha upotofu, kwa yakini Tutakusalitisha juu yao, kisha hawatakaa humo karibu yako ila muda kidogo tu. Maluuni (wamelaaniwa) hao popote waonekanapo wakamatwe na wauawe kabisa" (33: 60 – 61).

c)           Allaah Aliyetukuka Anasema: "Bila shaka wale wanaomuudhi Allaah na Mtume Wake, Allaah Amewalaani katika dunia na akhera, na Amewaandalia adhabu ifedheheshayo" (33: 57).

d)           Anasema tena Aliyetukuka: "Basi kwa sababu ya kuvunja kwao ahadi yao, Tuliwalaani na Tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu …" (5: 13).

e)          Anasema tena: "Jua kuwa laana ya Allaah iko juu ya madhalimu" (11: 18).

f)           Anasema tena: "Kishaa tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Allaah iwashukie waongo" (3: 61).

g)         Anasema tena Aliyetukuka: "Wamelaaniwa waliokufuru miongoni mwa Bani Israili kwa ulimi wa Daawuud na 'Iysaa mwana wa Maryam kwa sababu waliasi na wakapindukia mipaka" (5: 78).

Tukizitazama Aayah hizi utapata ya kwamba waliolaaniwa na Allaah Aliyetukuka ni wengi miongoni mwao ni makafiri, madhalimu, walioasi, waliotupa mipaka, wanaomuudhi Allaah na Mtume Wake, wanafiki, waongo, watangazao uovu, wenye kuficha Aliyoteremsha Allaah, na kadhalika.

Ama hawa watakaopata laana ya Allaah, basi Aliyetukuka Anatueleza: "Hao ndio Allaah Aliowalaani. Na ambaye Allaah Amemlaani basi hutamwona kuwa na mwenye kumnusuru" (4: 52).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share