Tiba Gani Zimo Katika Qur-aan?

SWALI

1. Sura gani ndani ya Quran ukiisoma, yaondosha mawazo ao stress?

2. Naomba nifahamu dawa za Blood pressure( high or low) na ya kisukari zilizomo ndani ya Qurani

3.Nimepata kusikiya asali ni dawa, je yatibu nini?

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Salah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wasallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Jibu la kwanza:

Hakuna Surah maalumu inayoondosha mawazo au dhiki bali Qur-aan nzima ni dawa ya ugonjwa kama huo kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى :

 

((وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاء وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ))

((Na tunateremsha katika Qur-aan yaliyo ni matibabu na Rehma kwa Waumini)) [Al-Israa:82]

 

((قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ ءامَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ))

((Sema: Hii Qur'ani ni uongofu na poza kwa wenye kuamini)) [Fuswilat:44]

 

 Amesema Shaykh 'Abdur-Rahmaan As-Sa'adiy رحمه الله "Poza  iliyokusanywa katika Qur-aan, kwa ujumla ni poza ya moyo, na poza ya mwili kutokana na maumivu yake na huzuni". 

 

Ama Suratul-Faatiha imethibitika kwamba ni poza ya magonjwa hasa kama ilivyokuja katika usimulizi kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudhriyyi رضي الله عنه kwamba:  "Kundi la Maswahaba walielekea katika safari hadi wakafika karibu na kabila fulani la Waarabu wakawaomba wawapokee kuwa wageni wao lakini walikataa kuwapokea. Mkuu wao akatafunwa na nyoka (au nge) na wakampa kila aina ya tiba lakini hazikumfaa. Baadhi yao wakasema: "Hebu waendeeni kundi la wasafiri walioteremka karibu yetu na waulizeni kama wanajua  tiba yoyote?". Wakawaendea Maswahaba na kuwaambia: "Enyi watu! Mkuu wetu ametafunwa na nyoka (ametafunwa na nge) na tummetibu kwa kila aina ya tiba lakini hakuna kilichomfaa. Je, kuna mmoja wenu anayejua cha kumfaa?" Mmoja wa Maswahaba akasema: "WaLLaahi najua kutibu kwa Ruqya. Lakini WaLLaahi nyie mmekataa kutupokea kama wageni wenu. Kwa hiyo hatutamtibu mgonjwa wenu hadi mtulipe".

 

Wakakubali kuwapa wasafiri (Maswahaba) kundi la kondoo. Akaenda Swahaba (pamoja na watu wa kabila) akamtemea mate (alipotafunwa) na kumsomea Suratul-Faatiha hadi mgonjwa akapata nafuu na akaanza kutembea kama kwamba hakuwa akiumwa. Kabila hili lilipowalipa malipo walioyokubaliana, baadhi yao (Maswahaba) wakasema:   "Gaweni  (kondoo)" Lakini yule aliyefanya Ruqya alisema: "Msifanye hivyo hadi kwanza tuelekee kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na kumuelezea yaliyotokea ili tuone atatuamrisha nini". Wakaenda kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na kumuelezea kisa chao naye akasema: ((Mmejuaje kuwa Suratul-Faatiha ni Ruqya? Mmefanya jambo la haki. Gaweni (mliyopewa) na munipe na mimi sehemu yangu)) [Al-Bukhaariy]

 

 Vile vile katika Sunnah Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametufundisha Du'aa za kuondosha dhiki, huzuni na hamu nazo ni:

اللّهُـمَّ إِنِّي عَبْـدُكَ ابْنُ عَبْـدِكَ ابْنُ أَمَتِـكَ نَاصِيَتِي بِيَـدِكَ، مَاضٍ فِيَّ حُكْمُكَ، عَدْلٌ فِيَّ قَضَاؤكَ أَسْأَلُـكَ بِكُلِّ اسْمٍ هُوَ لَكَ سَمَّـيْتَ بِهِ نَفْسَكَ أِوْ أَنْزَلْتَـهُ فِي كِتَابِكَ، أَوْ عَلَّمْـتَهُ أَحَداً مِنْ خَلْقِـكَ أَوِ اسْتَـأْثَرْتَ بِهِ فِي عِلْمِ الغَيْـبِ عِنْـدَكَ أَنْ تَجْـعَلَ القُرْآنَ رَبِيـعَ قَلْبِـي، وَنورَ صَـدْرِي وجَلَاءَ حُـزْنِي وذَهَابَ هَمِّـي

Allaahuuma Inniy 'Abduka ibnu 'Abdika ibnu Amatika. naaswiyatiy Biyadika, maadhwin fiyya  Hukmuka, 'adlun fiyya Qadhwaauka. As-aluka Bikullismin Huwa Laka, Sammayta bihi Nafsaka aw Anzaltahu fiy Kitaabika, aw 'Allamtahu Ahadam-Min Khalqika, aw Istaatharta bihi fiy 'Ilmil-Ghaybi 'Indaka, An Taj-'alal-Qu-raana Rabiy'a Qalbiy wa Nuura swadriy, wa jala-a huzniy, wa dhahaaba hammiy.  

 

“Ewe Allah, hakika mimi ni mtumwa Wako, mtoto wa mtumwa Wako, mtoto wa kijakazi Chako, utosi wangu uko mikononi Mwako, yaliyopita kwangu yako katika hukumu Yako, ni usawa kwangu kunihukumu Kwako, nakuomba kwa kila jina ambalo ni Lako Ulilojiita kwako Mwenyewe au uliloliteremsha katika kitabu Chako, au Ulilomfundisha yeyote yule kati ya viumbe Vyako, au Ulilolihifadhi Wewe Mwenyewe (na kujihusisha kulijuwa) katika ilimu iliofichika Kwako, nakuomba Ujaalie Qur-aan kuwa ni rabiy' (uhuisho, raha, furaha na ustawisho) wa moyo wangu na nuru ya kifua changu, na ufumbuzi wa  huzuni yangu, na sababu ya kuondoka wahka wangu.

 

اللّهُـمَّ إِنِّي أَعْوذُ بِكَ مِنَ الهَـمِّ وَ الْحُـزْنِ، والعًجْـزِ والكَسَلِ والبُخْـلِ والجُـبْنِ، وضَلْـعِ الـدَّيْنِ وغَلَبَـةِ الرِّجال.

Allaahumma Inni A'uudhu Bika minal-Hammi wal-Huzni, wal-'Ajzi wal-Kasali, wal-bukhli wal-jubni, wa dhwal'id-dayni wa ghalabatir-Rijaal

 

 “Ewe Allah,  hakika mimi najilinda Kwako kutokana na hamu, na huzuni na kutoweza, na uvivu, na ubakhili, na uoga, na uzito wa deni, na kushindwa na watu”

 

Jibu la pili na la tatu:

Magonjwa yote Aliyotuletea Allaah سبحانه وتعالى yana dawa zake kutokana na dalili za Hadiyth zifuatazo:

 

Hadiyth ya kwanza:

عن أبي الدرداء رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : ((إن الله تعالى أنزل الداء والدواء وجعل لكل داء دواء فتداووا ولا تداووا بالحرام))

Imetoka kwa Abu Ad-Dardaa رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Allaah Ameteremsha maradhi na dawa zake. Kwa kila maradhi kuna dawa yake, basi jitibuni wala msijitibu kwa yaliyo haraamu)) [Al-Bukhaariy na Abu Daawuud]

 

Hadiyth ya pili:

   عن عبدالله بن مسعود :قال رسول الله صلى الله عليه وآله وسلم  (( ما أنزل الله داء إلا أنزل له دواء فعليكم بألبان البقر فإنها ترم من كل الشجر))

Imetoka kwa 'Abdullah bin Mas'uud رضي الله عنه : Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Allaah Hakuteremsha maradhi ila Ameteremsha dawa zake, basi juu yenu (kunyweni) maziwa ya ng'ombe  kwani yanatokana na kila aina ya miti)) [Hadiyth sahiyh au hasan- Shaykh Al-Albaaniy]

 

Na dawa iliyo bora kabisa kutumia ni asali na habbatus-sawdaa (mbegu nyeusi) kama ilivyotajwa katika Qur-aan na Sunnah: 

Katika Qur-aan:

((وَأَوْحَى رَبُّكَ إِلَى النَّحْلِ أَنِ اتَّخِذِي مِنَ الْجِبَالِ بُيُوتًا وَمِنَ الشَّجَرِ وَمِمَّا يَعْرِشُونَ))

((ثُمَّ كُلِي مِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ فَاسْلُكِي سُبُلَ رَبِّكِ ذُلُلاً يَخْرُجُ مِن بُطُونِهَا شَرَابٌ مُّخْتَلِفٌ أَلْوَانُهُ فِيهِ شِفَاء لِلنَّاس))

((Na Mola wako Mlezi Amemfunulia nyuki: Jitengenezee majumba yako katika milima, na katika miti, na katika wanayojenga watu))

 

((Kisha kula katika kila matunda, na upite katika njia za Mola wako Mlezi zilizofanywa nyepesi kuzipita. Na kutoka matumbo yao kinatoka kinywaji chenye rangi mbali mbali; ndani yake kuna matibabu kwa wanaadamu)) [An-Nahl:68-69] 

 

Katika Sunnah:

يقول رسول الله  - صلى الله عليه وسلم  ((إن في الحبة السوداء شفاء من كل داء إلا السام))   اخرجه البخاري

Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ((katika habbatus-sawdaa kuna shifaa (matibabu) ya kila maradhi isipokuwa mauti)) [Al-Bukhaariy]

 

Mtu pia asome du'aa ya Mtume kama hii:

 

Unaweka mkono pale kwenye maumivu kisha useme:

 

بِسْمِ اللهِ

Bismillah   (mara tatu)

 

Kisha usema mara saba :

أَعُوذُ باللهِ وَقُدْرَتِهِ مَنْ شَرِّ مَا أَجِدُ وَأُحَاذِرُ

A'udhu BiLLahi wa Qudratihi Min sharri maa ajidu wa uhaadhiru.

 

“Najilinda kwa Allah na kwa uwezo Wake kutokana na shari ya ninachokisikia na ninachokiogopa” 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share