Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Alipokelewa Madiynah Kwa Nashiyd?

 

SWALI:

Kwanza kabisa nakushukuruni sana kwa majibu mazuri mnayotujibu kwa masuali yetu.

Ningependa kuwauliza suali langu kama hivi, Inasemekana wakati Mtume Muhammad (S.A.W) alivyohama Makka kuja Madina; ummati wa watu ilikuja kumpokea huko Madina wakiwemo men, women and children na alipofika Mtume (S.A.W) wote walimuimbia nasheed moja ya 'TALA AL-BADRU'. Jee! Vipi kuhusu suali hili wakati wanawake tu ndiwo wanaoruhusika kuimba nasheed? 

JAZAAKUMU LLAAH KHEYR   

 



 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Suala la kupokewa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Nashiyd ni jambo ambalo wametofautiana wanazuoni wa Siyrah. Pia kuhusu Nashiyd aliyoimbiwa wametofautiana wanazuoni kuhusu hilo.

Kuhusu Nashiyd wengi wanasema aliimbiwa: 

Twala‘al Badru ‘alayna         Min Thaniyaatil Wada‘i

Lakini Safiyur-Rahmaan Mubarakpuri amesema: 

Ashraqal Badru ‘alayna         Min Thaniyaatil Wada‘i 

 Mubarakpuri katika kitabu chake cha Siyrah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kiitwacho ar-Rahiyq al-Makhtuum amesema: “.. Majumba na njia zilijaa kishindo kwa sauti za kumsifu Allaah na kumtakasa. Mabinti wa Kianswaar waliimba beti zifuatazo kwa shangwe na furaha. Ibn al-Qayyim amesema, ‘Mashairi haya yaliimbwa alipokuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akirudi kutoka Taabuk (Zaad al-Ma‘ad, juzuu3, uk. 10).”

Mwenye Nurul Yaqiyn, Sh. Muhammad al-Hadhr Bek amesema: 'Hapa hadithia kuhusu furaha waliokuwa nayo watu wa Madinah bila ya tatizo … walifurahi kuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na walitoka wanawake, watoto na vijakazi wakisema: Twala‘al Badru ‘alayna, Min Thaniyaatil Wada‘i'. Naye Sh. Sirajur-Rahmaan an-Nadwiy al-Qaaadhiy katika al-Mustafaa amesema: 'Na walikuwa mabinti wa Kianswaari wakiimba beti zifuatazo: Twala‘al Badru ‘alayna, Min Thaniyaatil Wada‘i.

Na Abul Hasan ‘Aliy Nadwi katika Muhammad Rasulullah amesema maneno kama hayo ya Sh. Sirajur-Rahmaan.

Ibnul Qayyim asema kwamba mashairi haya yaliimbwa wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akirejea kutoka Taabuk'

Ibnul Qayyim amesema Thanayaatul Wada‘i iko katika njia ya kuelekea Syria kutoka Madiynah na kutoa dalili kuwa njia hiyo iko katika njia ya Makkah kuelekea Madiynah. Na Imaam Al-Bukhaariy alizungumzia hili na kusema wimbo huo uliimbwa wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akirudi kutoka Taabuuk. 

Hali kadhalika Imaam Muhammad ‘Abdul-Wahhaab amesema kuwa yaliimbwa alipotoka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  Taabuuk.

Allaamah Shibli Nu‘mani katika Siratun Nabiy amesema: “Wanawake waliokuwa ndani walijitokea kwenye mapaa yao na maghorofani wakiimba mashairi yafuatayo: Twala‘al Badru ‘alayna, Min Thaniyaatil Wada‘i. Watoto wa kike walitoka na matwari huku wakiimba: ‘Sisi ni mabinti wa Bani Najjaar, Uzuri ulioje kuwa na jirani kama Muhammad’.  

Ibn Hishaam katika as-Siyratun Nabawiyyah na Muhammad bin ‘Abdul-Wahhaab katika Mukhtaswar Siyratun Nabiy wametaja kisa cha Hijrah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuingia kwake Madiynah bila kutaja Nashiyd hiyo. Japokuwa Ibn ‘Abdul-Wahhaab ameitaja Nashiyd hiyo kuwa iliimbwa wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anarudi kutoka Taabuuk.

Qaadhi Sulaymaan Mansuurpuri katika Rahmatul Lil-‘Aalamiyn amesema: “Wasichana wadogo wasio na hatia waliimba mashairi yafuatayo kwa sauti nzuri: Twala‘al Badru ‘alayna, Min Thaniyaatil Wada‘i…”

Ama kuhusu swali lako ni kuwa walioruhusiwa kuimba Nashiyd ni kweli ni wanawake na haswa kwa kupigia dufu (matwari), lakini Nashiyd kwa maana ya mashairi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na washairi wake ambao walikuwa ni wanaume waliokuwa wakiutetea Uislamu kwa mashairi yao. Mfano ni Hassaan bin Thaabit na ‘Abdullaah bin Rawaahah (Radhiya Allaahu ‘anhuma).

Bila shaka katika kauli za wanazuoni ambazo tumezinukulu juu zote zinaonyesha wale walioimba walikuwa ima ni wasichana wadogo, vijakazi na riwaya nyingine wanawake.

Na hata kama mtu akidai kuwa walikuwepo wanaume, jibu litakuwa, kama kuna dalili walikuwepo wanaume basi si hoja ya wanaume kuruhusiwa kuimba na kupiga dufu kwa sababu mafundisho yaliyotufikia hayakutuonyesha popote kuwa wanaume walifanya hivyo, na pia Maswahaba hawakuwa wakifanya hayo. Na kama walifanya wanaume wakati huo, basi si hoja kwani wakati huo ndio Uislamu mwanzo unakita mizizi na yapo mambo ambayo yalikuwa yanafanyika kisha yakaharamishwa polepole kama pombe, riba na kadhalika.

Halikadhalika maelezo kuhusu kupokelewa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah kwa Nashiyd hiyo kuna utata katika usahihi wake kwa kutofautiana kukubwa kwa wasimulizi wa Siyrah kuhusu kuimbwa Nashiyd hiyo Madiynah au Taabuuk.

Na Allaah Anajua zaidi

Share