Zingatio: Baina Ya Udugu Na Uadui

 

Zingatio: Baina Ya Udugu Na Uadui

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Ni kutokana na ujinga na dharau zetu ndio tumeufikisha Uislamu kwenye hali iliyopo sasa. Sio tu kwa kukosa dira ya kufuata au Kitabu cha kusoma, la sivyo! Bali pia ni kwa kuwafanya maadui wa Uislamu kuwa ni wenzetu wa karibu mno kuliko hata ndugu wa Kiislamu walio na imani thabiti.

 

 

Tunakosa kupata taathira ya kumsujudia Muumba mara 34 kwa siku kwa kuwa hatujayakinisha kuwa Uislamu ni dini ya haki. Iweje basi Muislamu atamke kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ndiye Rabb wake na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndie kiongozi wake lakini bado akawa hana tofauti na Manaswara na Mayahudi? Iwapi tofauti yao? Ndio maana Muislamu huyu anaona ni sawa kupitishwa pombe mbele yake na kuyatoa nuru macho kwa kukodolea wanawake watembeao uchi. Ni Muislamu huyu huyu anayedhamini mashindano ya urembo na hata kutia saini mikataba ya pombe. Na ndio maana hata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akikashifiwa kwa kuchorwa kikatuni au kutusiwa kwa namna nyengine yoyote, yeye anakuwa hana mshituko wowote! Subhaana Allaah.

 

 

Ni lazima tukumbuke kuwa tupo ndani ya mpambano na wala hautaisha hadi Qiyaamah kisimame. Tutakapoelewa muongozo sahihi wa dini yetu ndipo tutakapoweza kupambana na hila hizi. Sio kabisa kuitamka Shahaadah hali ya kuwa hakuna hata maendeleo yoyote ya ulinganiaji au elimu inayofundishwa. Na hata kama zikifanyika zinakosa usahihi wa Sunnah.

 

 

Waislamu tuelewe kwamba kufanya urafiki na Muislamu mwenzetu mwenye imani thaabit ni bora zaidi kuliko kuwaweka nyoyoni wasiokuwa Waislamu. Sisi ni jengo moja lililo imara na haitakikani kuwaingiza maadui ndani ya harakati zetu abadan.

 

 

Hatuna haja ya kuwaorodhesha ni nani maadui wa Uislamu, kwani ni wengi. Kinyume na uadui ni kufanya nao urafiki. Kitu ambacho katu hakikubaliki ndani ya Uislamu. Tuishi nao kwa usalama na ubinaadamu pale wanapoheshimu miiko ya dini yetu. Kinachoamrishwa hapa chini sio amri ya fulani bali ni kanuni ya Muumba Anayetuamrisha:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا عَدُوِّي وَعَدُوَّكُمْ أَوْلِيَاءَ تُلْقُونَ إِلَيْهِم بِالْمَوَدَّةِ وَقَدْ كَفَرُوا بِمَا جَاءَكُم مِّنَ الْحَقِّ 

Enyi walioamini! Msifanye adui Wangu na adui wenu kuwa marafiki wandani mkiwapa mapenzi, na hali wamekwishakufuru yaliyokujieni ya haki;  [Al-Mumtahinah: 1]

 

 

Tufahamu ya kwamba kampuni zilizo nyingi zinaongozwa na Mayahudi wakisaidiana na Manaswara. Kuanzia vyombo vya habari, vyakula, vivazi na mengineyo chungu nzima. Tuwe makini na kinachozalishwa humo kwani ni mara nyingi kinakuwa ni chenye kuleta madhara kwa Waislamu na Uislamu wao. Hata kazi kadhaa zinazofanywa humalizia kukejeli dini tukufu ya Uislamu. Tuzifuatie hila hizi na kuzipinga angalau tu kwa kutozitumia.

 

 

Kuna mengi ambayo yanafanywa na sisi wenyewe tunayashuhudia. Maadui zetu wanachora vikatuni vya kumkashifu[1] Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wengine wanaandika vitabu maalum[2] ambavyo ndio vinawapatia tuzo za heshima kwa kumkashifu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tu! Maoni ya kupunguza kasi ya Ukimwi yamefanywa kuwa ni chambo ya kuutukana Uislamu kwa kueleza kwamba mgao wa mirathi unachangia kumtelekeza mwanamke na kumsababishia kuingia kwenye biashara haramu.[3]Inafikia hatua ya Mbunge kupeleka mapendekezo maalum kwenye bunge kwa ajili ya kuudumaza Uislamu tu[4].

 

Tukumbuke kwamba kuendelea kunyamaza kimya ndio tunapoendelea kudhalilika na kudhoofika. Wengi wetu ndio tunaangukia kwenye udhaifu wa imani kwani twaona maovu yanayotendwa mbele yetu lakini hatuna tunachokemea.

 

 

Kutoka kwa Nabiy wetu mpenzi (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Hadiyth iliyosimuliwa na Abuu Sa'iyd Al-Khudriy (Radhwiya Allahu  'anhu) ambaye amesema: Nilimsikia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akisema: "Yeyote yule atakayeona kitendo kiovu basi akiondoe (akibadilishe) kwa mkono wake, ikiwa hawezi basi kwa ulimi wake (alikemee au kukataza), na ikiwa hawezi basi kwa moyo wake (achukie) na huo (yaani kuona baya na kunyamaza) ni udhaifu wa Imani)) [Muslim]

 

 

Hivyo, tuelewe ndugu zangu wa Kiislamu kwamba tupo baina ya mstari mwembamba ndani ya mapambano ya Udugu wetu Waislamu na Maadui ambao ndio wengi mno. Nao wanashambulia kutoka kila kona ya ulimwengu huu na kwa hila tofauti zilizo dhaahir na zilizo siri.

 

 

Tushikamane na tufuate Sunnah sahihi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuisoma vyema Qur-aan na kufuata maadili mema ya Uislamu wetu. In shaa Allaah tukiwa imara, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atatupatia ushindi kwa nia na vitendo vyetu.

 

[1] Gazeti la Gulf News la 14/02/08 uk. 23 limetangaza kwamba magazeti 17 ya Denmark yamemtukana Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

[2] Salman Rushdie, Aya za Shetani SATANIC VERSES, (1988).

[3] Rudia Ripoti ya Jumuiya ya Wanasheria Wakike Tanzania, REVIEWS AND ASSESSMENT OF LAWS AFFECTING HIV/AIDS IN TANZANIA, TAWLA, Magdalena K. Rwebangira na Maria Tungaraza, (2003), uk. 29, 30 na 43.

[4] Pamoja na mambo mengine, Ibara ya 2 (c) ya Hati ya Uingereza kwa Uislamu na Waislamu inaeleza kwamba taasisi za Kiislamu ziwaeleze vijana wa Kiislamu kwamba sheria za kijamii za nchi ni bora kuliko Shariah (Qur-aan na Sunnah). Rudia A Proposed Charter of Muslim Understanding by Sam Solomon, Foreword by Gerard Batten, UK Independence Party, Member of the European Parliament for London, December 2006.

 

Share