Mvulana Hodari Sana Lakini Mtundu Sana Wafanyeje Hata Apunguze Utundu?

 

SWALI:

Natumai nyote ni wazima wa afya, Inshaallaah Allaah (Subhanahu wataala) atakuongozeni kwa hali na mali katika kuindeleza website hii yenye manufaa kwetu sisi waislam

Swali lang ni hili; kuna mtoto wa rafiki yangu ana umri wa miaka 12, ni hodari sana katika masomo yaani ni very bright boy naweza kusema ana akili timamu. Lakini cha kushangaza mtoto huyo ni mtundu ajabu, unapomwambia usifanye hili yeye hasikii, anaweza kutoka kwao jioni bila ya kusema na husababisha wazee wake kuhangaika mpaka saa nane za usiku. Kwa ufupi ameshashinda kwao. Jee mtoto km huyo afanywe nini au kuna dua gani ya kumsomea ili atulie na huo utundu wake



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo zuri kuhusu malezi. Hakika ni kuwa swali lako hili lina upungufu kwani umetuelezea kuhusu hali ya utundu wa mtoto lakini hukutuelezea hali za wazazi wake.

Je, wazazi wake wakoje katika amali zao za Uislamu? Je, wao walipatana kwa misingi gani? Je, maadili yao yakoje, je, huyo ni mtoto wa kwanza au wazazi hao wana mtoto mwengine?

Haitarajiwi kwa mtoto kuwa na tabia njema ikiwa wazazi wenyewe hawana hayo maadili mema wala amali njema za Uislamu. Ikiwa wazazi wanafanya mambo ambayo si mema mtoto huenda akaiga kisha ikawa ngumu kumfanya kijana huyo aache. Ikiwa wazazi wenyewe hawakupatana kwa njia ya Uislamu basi haitarajiwi kuwa kijana wao anaweza kupatiwa maadili mazuri na mema. Mara nyingi ikiwa kijana ni wa kwanza au wa mwisho au ni wa pekee, baadhi ya wazazi huwa wanamshauza (wanamtendekeza/ wanamdekeza). Hali hiyo huwapelekea wazazi wasiwe ni wenye kumpatia adabu au adhabu wakati kijana huyo anafanya makosa. Hilo humfanya kijana aone kuwa anaweza kufanya chochote na hakuna lolote litakalokuwa.

Katika hali hiyo, kijana anaweza kuwa hapelekwi hata Madrasah ili aweze kufundishwa maadili mema ya Kiislamu. Katika mazingira hayo unatarajia vipi kijana awe ni mwema na aache utundu. Jambo ambalo linatakiwa kufanywa na wazazi ni kubadilisha mazingira wanayoishi kwani huenda yakawa si munaasib kwao. Pengine katika mazingira hayo wapo watoto wengi watundu, hali inayompelekea naye kijana kufuata tabia za wenziwe.

Jambo ambalo tunaweza kutofautiana nalo ni kuwa kijana anaweza kuwashida wazazi. Inatakiwa wazazi hao watazame njia muafaka ya kumtoa kijana wao katika maangamivu hayo yaliyo makubwa. Wakifanya juhudi basi watakuwa ni wenye kupata msaada kutoka sehemu wasiyotarajia. Wazazi wasichoke kufanya juhudi juu ya kijana wao na Aliye juu atawapatia tawfiki.

Kwa nasaha zaidi kutoka kwetu itabidi mambo mengi yafunuliwe ili tuweze kujua mazingira hayo na dawa muafaka kwa hilo.

Anaweza pia kufanya yafuatayo na kusoma du’aa mbalimbali tutakazoziorodhesha chini.

Inaweza pia kuwa mtoto huyo labda hakufanyiwa 'Aqiyqah alipozaliwa kwani hiyo pamoja na kuwa ni kafara ya mtoto pia baadhi ya Maulamaa wanaona ni kinga ya kumlinda mtoto na Shaytwaan.

Du'aa za kumsomea kutoka Qur-aan:

Suratul-Faatihah na amwache mtoto mwenyewe asome.

Ayatul-Kursiy na Aayah mbili zinazofuatia.

Aayah mbili za mwisho za Suratul Baqarah

Suratul Ikhlaasw x 3

Suratul-Falaq x 3

Suratun-Naas x 3 

Du'aa za kusoma mzazi:

  رَبَّنَا وَاجْعَلْنَا مُسْلِمَيْنِ لَكَ وَمِن ذُرِّيَّتِنَا أُمَّةً مُّسْلِمَةً لَّكَ وَأَرِنَا مَنَاسِكَنَا وَتُبْ عَلَيْنَآ إِنَّكَ أَنتَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ  

Rabbana Waj-'alnaa Muslimayni Laka Wamin Dhurriyyatinaa Ummatam-Muslimatal-Laka Wa Arinaa Manaasikanaa Watub 'Alaynaa Innaka Antat-Tawwaabur-Rahiym.

Ewe Mola Mlezi wetu! Tujaalie tuwe ni wenye kusilimu Kwako, na pia miongoni mwa vizazi vyetu wawe umma ulio silimu Kwako. Na Utuonyeshe njia za ibada yetu na Utusamehe. Bila shaka Wewe Ndiye Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. [Al-Baqarah: 127 – 128].

Kila baada ya Swalah asome du'aa ifuatayo:

رَبِّ اجْعَلْنِي مُقِيمَ الصَّلاَةِ وَمِن ذُرِّيَّتِي رَبَّنَا وَتَقَبَّلْ دُعَاء

Rabbij-'alniy Muqiymas-Swalaati Wa Min Dhurriyaatiy Rabbanaa Wa Taqabbal Du'aa.

Mola wangu Mlezi! Nijaalie niwe mwenye kushika Swalah, na katika dhuriya zangu pia. Ewe Mola wetu Mlezi, na ipokee du'aa yangu [Ibraahiym:  40]

رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَاماً   

Rabbanaa Hab Lanaa Min Azwaajinaa Wa Dhurriyaatinaa Qurrata A'yuniw-Waj'alnaa Lilmuttaqiyna Imaamaa.

Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na Utujaalie tuwe waongozi kwa wacha Mungu [Al-Furqaan: 74]

 

رَبِّ أَوْزِعْنِي أَنْ أَشْكُرَ نِعْمَتَكَ الَّتِي أَنْعَمْتَ عَلَيَّ وَعَلَى وَالِدَيَّ وَأَنْ أَعْمَلَ صَالِحًا تَرْضَاهُ وَأَصْلِحْ لِي فِي ذُرِّيَّتِي إِنِّي تُبْتُ إِلَيْكَ وَإِنِّي مِنْ الْمُسْلِمِينَ 

Rabbi Awzi'niy An Ashkura Ni'matakal-Latiy An'amta 'Alayya Wa 'Alaa Waalidayya Wa An A'amala Swaalihan Tardhwaahu Wa Aswlih Liy Fiy Dhurriyatiy Inni Tubtu Ilayka Wa Inniy Minal Muslimiyn.

Mola wangu Mlezi! Niwezeshe nishukuru neema Zako Ulizonineemesha mimi na wazazi wangu, na nitende mema unayo yapenda. Na unitengenezee dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu Kwako, na mimi ni miongoni mwa Waislamu. [Al-Ahqaaf: 15]

Kutoka katika Sunnah amsomee:

Imepokelewa na Ibn 'Abbaas amesema alikuwa Mtume wa Allaah  akiwakinga wajukuu wake (Hassan na Husayn) akisema :

أُعيـذُكُمـا بِكَلِـماتِ اللهِ التّـامَّة، مِنْ كُلِّ شَيْـطانٍ وَهـامَّة، وَمِنْ كُـلِّ عَـيْنٍ لامَّـة

"Nawakinga kwa maneno ya Allaah yaliyotimia awakinge kutokana na kila shetani na uvamizi na kila jicho lenye kudhuru"

Tunamuombea mtoto huyo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ampe utulivu na Amjaalie kuwa miongoni mwa wachaMungu Insha-Allaah.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share