Kumpa Mtoto Jina La Kikristo Inafaa Au Dhambi?

SWALI

 

Assalam Alleykum warahmatullah wabarakat

 

Mimi nimuislam nimetokea kulipenda jina moja zuri la kikristo je ni dhambi? Hilo ndilo swali langu na nililituma week iliyopita lakini sijapata majibu mpaka leo tafadhali naomba nisaidie kwahili.


 

 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 


Hatuoni kwa nini Muislam kulipenda jina la Kikristo na hali kuna majina mengi mazuri katika Uislam?

 


Nini hasa kinaweza kumshawishi Muislam hadi kulipenda jina la Kikristo? Je, ni kuwapenda wao? Je, ni kuwa na mtu mwenye jina hilo kamvutia hadi kulipenda jina lake? Je, ni kutojua mafundisho ua Uislam vizuri?
Inawezekana ikawa ni moja ya hayo, na zaidi ni Muislam kutofahamu vizuri mafundisho mazuri ya Uislam; vipi Uislam unafundisha kuhusu kuitana, na majina yepi yaliyopendekezwa na Mtume wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na yepi majina yanayopendwa zaidi na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) n.k.
 

 


Tunakuwekea hapa chini viungo vya kuonyesha mafunzo ya Uislam kuhusu majina, na umuhimu wa kuwa na majina mazuri ya Kiislam

 


 
Majina Ya Watoto Na Maana Yake

  
Fiqh Ya Kuwaita Majina Watoto
 

 

 


Jina ni utambulisho wa mtu na utambulisho huo bila shaka unapaswa kuwa unawakilisha kitu au maana nzuri kabisa. Hivyo, pamoja na kuwa haikatazwi kuwa na jina lenye maana nzuri japo si katika majina ya Kiislam, lakini lazima ufahamu kuwa utakapokuwa na jina lisilojulikana katika Uislam na ambalo linajulikana katika dini nyingine, basi tayari utakuwa umejiwekea ugumu mwenyewe kutambulika na kufahamika kwa urahisi katika jamii yako ya Kiislam kama ni Muislam na pia kutopata ushirikiano wa haraka na mwepesi na mzuri kutoka kwa ndugu zako Waislam kwa kudhania au kuamini kuwa wewe si mwenzao.
 
Pia jina ni heshima na unapokuwa na jina zuri la Kiislam, basi heshima yako katika jamii inakuwa kubwa kuliko kuwa na jina la Kikristo. Isitoshe kujiita jina la Kikristo ni katika kujifananisha nao na hilo Mtume wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amelikemea sana kwetu kujifananisha na makafiri. Kadhaalika mtu atafufuliwa na kuitwa kwa jina lake, sijui mwenetu utapenda ujulikane kwa jina lisilo la Kiislam?


 

Pia je, umezingatia kuwa mwanao atakapofikia umri wa kutambua kila jambo,  akajua kwamba jina ulompa ni la Kikristo naye akachukizwa nalo?  Je utamjibu nini? Huoni kwamba hapo itakuleteeni matatizo wote pamoja na mihangaiko ya kubadilisha vyeti vyake vyote pindi akiazimia?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share