Michezo Ya Watoto Masanamu Na Vinyago Vinafaa?

 

SWALI:

Assalaam ' Alaykum Warahmatullah Wabarakatu,

Tunashukuru sana kwa tovuti ya Alhidaya kwani tunaelimika na mengi na inshalla Allah atakulipeni ujira wenu, Amin.

Nilikua nina masuala mawili kuhusu vitu vya kuchezea watoto (TOYS), jee tunaweza kuwanunulia vitu kama watoto wa sanamu au picha picha nyengine kwa ajili ya kuchezea??  Ukizingatia toys nyingi za watoto ni za  vinyago vinyago.

Na jee vipi kuhusu programm za watoto, nyingi zao zinawafunza lakini hutumia njia za nyimbo kwa kutoa mafunzo fulani na pia zimejaa vikatuni.

Jee utatupa ushauri gani kwa vitu viwili hivi na nini tufanye kwa watoto wetu kama ni wazazi??

 


JIBU:

AlhamduliLLah,  Waswalaatu Was-salaam 'alaa RasuulilAllaah  صلى الله عليه وآله وسلم Amma ba'ad,

 

Kuhusu swali lako, Maulamaa wameona kuwa jambo hili sio haraam kuwaachia watoto wachezee watoto wa sanamu kutokana na Hadiythi ya Bibi 'Aishah رضي الله عنها  ambaye amesema ((Nilikuwa nachezea watoto wa sanamu mbele ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na nilikuwa na rafiki zangu ambao walikuwa wakicheza na mimi.  Ilikuwa anapoingia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم huwa wanajificha na yeye huwaita waje kucheza na mimi))  [Al-Bukhaariy na Muslim]

Ingawa imeonekana kuwa sio haraam au makruuh kuchezea watoto wa sanamu na michezo mingine ya watoto, lakini Maulamaa wamegusia kuwa michezo ya zamani kama watoto wa sanamu walikuwa hawana macho, pua na midomo na sio kama watoto wa sanamu wa siku hizi,  kwa hiyo ni bora kujiepusha nayo michezo hiyo.

Shaykh Ibn 'Uthaymiyn amesema,

"Kama michezo in umbo kamili kama vile unamtazama mtu, na khaswa kama huo mchezo unaweza kutembea na kusema, basi sioni kama ni sawa kuiruhusu kuchezewa, kwa sababu hii ni kiigo kamili cha maumbile ya Allaah. Michezo aliyokuwa akichezea 'Aishah رضي الله عنها haikuwa kama hivi, kwa hiyo ni bora kujiepusha. Lakini siwezi kusema kama ni haraam, kwa sababu ruhusa waliyopewa watoto sio ruhusa waliyopewa watu wazima katika mambo haya.  Ni desturi kuwa watoto kucheza na kufurahi na wao hawakulazimishwa na vitendo vyovyote vya ibada, kwa hiyo hatuwezi kusema kuwa wao wanapoteza wakati wao katika kucheza. Lakini kama mtu anataka kujiepusha na kubakia katika usalama kwenye mambo hayo, ni bora kukikata kichwa cha sanamu na kukilainisha kwa kukiweka karibu na moto mpaka kiwe laini, kisha akibane mpaka ipotee sura yake.

[Majmu'ul-Fataawa Al-Shaykh Muhammad Ibn 'Uthaymiyn (Allaah Amrehemu) 2/277 ]

Hata hivyo, haifai watu kuweka masanamu hayo na yale ya wanyama kama dubu (bear) na wengine ambazo zinatumika sana katika jamii za Ulaya, Marekani na kwengineko, na kuzifanya ni mapambo ya vyumba vya watoto na wengine wakawa wananunua masanamu ya dubu na kulala nayo. Wengine wamewazoesha watoto wao kutolala hadi wakumbatie hizo sanamu, na hali hiyo imewakuza watoto na kuwalemaza hadi wengine washavunja ungo na kuwa wasichana wakubwa na bado wamezoea kulala na visanamu hivyo. Kadhalika kuna wanawake watu wazima wakilala na sanamu hizo kujiliwaza nazo kama vile wako na wanaume. Na hayo ni makosa makubwa na ni mambo yenye kupelekea kwenye uchafu wa zinaa.

Ama kuhusu programu zenye vikatuni lakini zina mafundisho ya Kiislamu na hazina muziki wala mambo yenye kwenda kinyume na shari'ah, Maulamaa wameona kuwa hakuna ubaya kwani lengo itakuwa ni kuwapa mafundisho. Na pia kutokana na fitna zilizojaa katika televisheni, itakuwa ni bora kuliko kutazama michezo ya kikafiri ambayo huenda ikaweletea athari ya kufuata mila hizo za kikafiri.

Shaykh ibn 'Uthyamiyn alijibu swali kama hili kuwa, "Hakuna ubaya kwani hii itawaepusha na kutazama maovu".

[Fataawa za Shaykh Muhammad ibn Swaalih Al'Uthaymiyn, Majallat Ad-Da'awah, toleo namba 1823, Ukurasa 54]

Wa Allaahu A'alam

Share