Mume Ametaka Ndoa Iwe Ya Siri Lakini Hanipi Chochote Na Haji Kwangu Ila Kwa Mahitaji Ya Kimwili Tu

 

SWALI:

Assalam aleikum,

Swali langu ni kuuliza kama ndoa yangu inakubalika? Kwani nimeolewa na mume wa mtu na huyu bwana hataki mtu ajue katika upande wake wote, ila kwangu ndo wanamjua na aliniambia kuwa hataki mkewe ajue na sasa nimegundua kuwa ana mke mwengine na sasa mimi ni wa tatu alishakuwa na wawili kabla yangu na pia hanipi matumizi ya aina yoyote na hajui naishi wapi kwani nimehama hapo aliponiolea na pia mimi sipajui kwake wala hajanionesha huwa tu tunakutana na hataki kunipa makazi wala matumizi anachotaka ni mwili wangu tu na iwe siri kwani yeye ana watoto wawili na sasa weeki imepita sijamsikia kila nikipiga anapoke mkewe na siwezi ongea kitu nakata na toka niolewe huu ni mwezi wa 7 maisha ndo haya na hataki watoto na mimi kabisa tulifunga ndoa msikitini bila ndugu wowote tafadhalini nawaomba ndugu zangu mniokoe maisha yangu sijui nifanyeje ili niwe katika njia ya kheri ya kiislam naomba mnijulishe kama hii ndoa iliswihi au la?

 JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu muuliza swali lakezuri kuhusu uanandoa. Tumekuwa tukipiga makelele kwa nyakati nyingi kuhusu haki ambazo wanawake wamepatiwa na Uislamu na dhuluma ambazo wanafanyiwa na wanaume. Hata hivyo, tumekuwa tukizungumza sana kuhusu uchaguzi katika ndoa zetu lakini inaonekana haya yanapatikana kujulikana pindi tu tatizo linapotokea.

Dada zetu wamekataa kabisa kufuata muongozo tulioachiwa na Uislamu katika uchaguzi wa mume. Yale ambayo tumeagizia lau tungekuwa tunayafuata basi haya matatizo mengi hayangekuwa ni yenye kutusibu. Ndipo Allaah Aliyetukuka Akatuambia:

Na misiba inayo kusibuni ni kwa sababu ya vitendo vya mikono yenu. Naye Anasamehe mengi” (42: 30).

Tungekuwa tukifuata maagizo basi msichana mwenyewe angetaka kumfahamu atakayekuwa mumewe na wazazi nao wangetekeleza wajibu wao katika hilo. Lakini ni sikitiko kuwa umeingia katika mafungamano ambayo hukuyatazamia wala kuyatarajia kwa vyovyote vile. Uchaji Mungu haupo kwa huyo mwanamme ndio maana hakuweza au hawezi kufanya uadilifu baina ya wake (nyinyi watatu), kwani sifa hiyo ni muhimu kwa mume kuongeza mke.

Hayo tuyaache kwa kuwa yashatendeka kwani hatuwezi kuurudisha tena wakati – ushapita. La kufanya ni kuangalia yanayokusibu kwa wakati huu ili kuweza kupata ufumbuzi wa hayo yako. Mwanzo kujua kama ndoa yako ni sawa kisheria au si sawa ni lazima tuangalie masharti. Masharti yakitimia ndoa itakuwa sahihi kisheria na ikiwa hayakutimia kutakuwa hakuna ndoa baina yenu. Masharti yenyewe ni kama yafuatayo:

  1. Wewe ukubali kuolewa na mume huyo.

  2. Awepo walii wako na kukubali kwake. Walii anatakiwa awe ni babako, ikiwa hayupo ndio jukumu hilo litachukuliwa na mwengine aliye karibu nawe kinasaba.

  3. Kukubali mume kukuoa.

  4. Kukulipa mahari mliyosikizana.

Ikiwa masharti hayo yalitimizwa basi ndoa yenu baina yenu ni halali kisheria na hakuna tatizo. Ingawa swali lako halionyeshi kutimizwa masharti hayo ila uhakika unaujua mwenyewe ila sisi ni wenye kujibu kutokana na maelezo ya muulizaji. Ila fahamu kuwa ikiwa hayo masharti hayakutekelezeka, basi huna ndoa.

Tatizo linavyoonekana kulingana na swali lako ni kuwa hakuna uadilifu unaopata kutokana na ndoa hiyo. Kabla ya kutaka kukutatulia tatizo hilo, je, mlikuwa na maagano yoyote kuhusu kuja kwake kwako? Je, mlipangiana vipi kuhusu mas-ala ya unyumba?

Mara nyingi wasichana hudanganywa kuingia katika mafungamano ya uanandoa lakini mume akawa hatimizi ya kwake hivyo ndoa hiyo kuwa haishi matatizo. Inafahamika kuwa ni jukumu la mume kumpatia mke masrufu yake yote hata akiwa na zaidi ya mke mmoja. Masurufu yenyewe ni kulipa kodi ya nyumba, chakula, mavazi, matibabu na kadhalika. Kwa kuwa yeye anakuja tu anapotaka kustarehe nawe ni kuwa alikuwa na malengo yake mengine.

Ushauri wetu kwako ni kama ufuatao; huu ni ushauri ikiwa tu unaona kuwa ndoa yako ilitimiza masharti na ni sahihi:

  1. Anapokuja nyumbani kwako, inatakiwa umweke chini na uzungumze naye kinaganaga kwa jinsi anavyofanya mambo na inavyotakiwa. Na suala muhimu ni je, anataka mahusiano yenu ya kindoa yaendelee au vipi? Hilo ni lazima ulitangulize mbele. Ikiwa jawabu ndio basi umshurutishe akupatie masurufu yako yote kwa mahitaji yako pamoja na kukupangia siku maalumu isiwe anakuja kwako kama mwizi.

  2. Ikiwa hilo halikufaulu itisha kikao baina yako, yake, jamaa zako na wake ili mlizungumzie suala hilo. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke. Wakitaka mapatano Allaah Atawawezesha. Hakika Allaah ni Mjuzi Mwenye khabari” (4: 35).

  3. Ikiwa kikao hicho hakikutoa ufumbuzi wa aina yoyote basi itabidi upeke mashtaka yako kwa Qaadhi au Shaykh au Imaam mwadilifu au yule aliyefunga nikaha (Nikaah) ili awasikilize. Hiyo ya kutopatiwa masurufu ni sababu tosha yako kudai talaka. Ikiwa kumepatikana ufumbuzi barabara itakuwa kheri.

Tunaomba ufumbuzi wa hakika upatikane ili muweze kuendelea kubaki katika uanandoa kwa njia ya masikilizano na maalewano kila mmoja akitekeleza wajibu wake na kupata haki zake.

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share