Zingatio: Muabudu Mola Wako Hadi Ikufikie Yakini

 

Zingatio: Muabudu Rabb Wako Hadi Ikufikie Yakini

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Jaalia wasomi wawili ndani ya chumba cha mtihani kila mmoja akiwa na azma ya kufaulu vizuri mtihani. Mmoja wao amepata alama 85 na mwengine 75 chini ya mia. Yupo mwengine ambaye alitarajia kufaulu bila ya kusoma na akazembea, matokeo yake ameshindwa kufaulu. Watu hawa watatu wanakutana mbele ya Mwalimu mkuu kila mmoja akidai alama zaidi.

 

Ndugu yangu Muislamu, hiyo ndio nafsi ya mwanaadamu isiyotosheka. Hizo ndio hali zetu Siku ya Hisabu. Kwa aliyepata daraja ya pili ya jannah atataka apate ya kwanza na aliyeingia motoni ataomba apate japo daraja ya chini kabisa ya pepo. Kama tumekuja duniani kutafuta mafanikio mbele ya Rabb, tusifanye mzaha na kipande tulichopewa cha keki (saa) ambacho tunakila na bila ya shaka keki unayoipenda huwezi kuiila ukataraji isimalize.

 

Ndugu yangu Muislamu nakuusia pamoja na kuiusia nafsi yangu tumche Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kumuabudu Rabb bila ya kuchoka hadi itakapotufikia saa ya kuondoka duniani kama Alivyosema: 

وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ﴿٩٩﴾

Na mwabudu Rabb wako mpaka ikufikie yakini (mauti). [Al-Hijr: 99]

 

Utumie muda wako katika mambo ya kheri yatakayokusaidia huko uwendako kwenye maisha ya milele. Hebu kaa kitako ufikiri ni masaa mangapi kwa siku unayatumia katika kufanya mambo ya kheri na masaa mangapi unayatupa bure kwa mambo maovu au ya upuuzi ambayo hayatokusaidia chochote akhera. Je katika siku kamili ni kiasi gani umeikumbuka siku ya kutolewa roho? Ni kiwango gani umevuta fikra ya namna adhabu Yake Rabb ilivyo kubwa? Ni kwa mizani gani umeweza kuizuia nafsi yako kuvutwa na ushabiki usio na maana kama vile muziki na mpira?

 

Leo Muislamu unakaa na kushabikia michezo ya bao, mpira, muziki, karata na kadhalika ukilalamika kuwa ni halali? Basi iweje michezo hiyo iwe ni mbadala wa ibada Alizoamrisha Rabb? Kumbuka kuwa haiwezekeani kuiacha michezo hiyo bila ya kumukhofu Rabb kama alivyosema kipenzi chetu Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

Hawi mtu ni katika wenye kumcha Allaah mpaka aache hata lisilokuwa na ubaya kwa kuogopa kufanya lenye ubaya” [At-Tirmidhiy].

 

Fungua kurasa za Siyrah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Taariykh za Salaf-us-Swaalih uone namna walivyoikamata dini hata kula wakisahau.

 

Ndugu yangu Muislam, ni sababu gani inayokufanya usimwabudu Rabb wako wakati mtu hujijui na wala huna hakika kabisa ni wakati gani kifo kitakubishia hodi? Kifo kipo nyuma yako, kwani kinapowadia huna pa kukimbilia. Kila unavyopitisha siku uelewe wazi kuwa ndivyo unavyopiga hatua na kukaribia kifo chako. Hujui kamwe ni miaka mingapi au ni siku ngapi au hata ni dakika ngapi zimebaki za wewe kuishi duniani.

 

Ninachokuomba ndugu yangu Mwislam, tujihesabu kabla ya kuhesabiwa kama Uislamu ulivyotuusia. Kaa kitako ujihesabu ni yepi mema uliyoyatekeleza na mangapi maovu uliyoyafanya katika kila siku yako moja unayoishi.

 

 

Share