Zingatio: Dunia Imejaa Ghururi

 

Zingatio: Dunia Imejaa Ghururi

 

 Naaswir Haamid

 

 

  Alhidaaya.com

 

 

Hakika dunia imejaa ghururi, basi yasikudanganyeni maisha ya dunia wala asikudanganyeni yule mdanganyi mkubwa (Ibilisi) katika (mambo ya) Allaah. Dunia itupeni mbali kama vile Allaah Alivyotutaka na itafuteni akhera yenu, kwani Allaah Ameipigia mfano dunia [Khotuba ya Sayyidna ‘Uthmaan bin ‘Affaan aliposhika madaraka]

 

وَاضْرِبْ لَهُم مَّثَلَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا كَمَاءٍ أَنزَلْنَاهُ مِنَ السَّمَاءِ فَاخْتَلَطَ بِهِ نَبَاتُ الْأَرْضِ فَأَصْبَحَ هَشِيمًا تَذْرُوهُ الرِّيَاحُ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ مُّقْتَدِرًا ﴿٤٥﴾الْمَالُ وَالْبَنُونَ زِينَةُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَالْبَاقِيَاتُ الصَّالِحَاتُ خَيْرٌ عِندَ رَبِّكَ ثَوَابًا وَخَيْرٌ أَمَلًا ﴿٤٦﴾

Na wapigie mfano wa uhai wa dunia kama maji Tuliyoyateremsha kutoka mbinguni, yakachanganyika kwayo mimea ya ardhi (ikasitawi), kisha yakawa makavu yaliyovurugika yanapeperushwa na upepo. Na Allaah daima ni Mwenye Uwezo wa juu kabisa kwa kila kitu. 46. Mali na watoto ni pambo la uhai wa dunia. Na mema yanayobakia ni bora mbele ya Rabb wako, kwa thawabu na matumaini. [Al Kahf: 45 – 46]

 

 

Nakuusieni waja wa Allaah kumuogopa Allaah, kwani taqwa ni jambo bora la kunasihiana baina ya waja wa Allaah, na ndiyo amali Anayoridhika nayo Allaah kutoka kwa waja wake.

 

 

Mumeamrishwa kumcha Allaah na kwa ajili ya wema mumeumbwa, kwa hivyo ogopeni yale Allaah Aliyokutahadharisheni nayo, kwa sababu Amekutahadharisheni na adhabu kali kabisa.

 

 

Muogopeni Allaah kuogopa kwa kweli na tendeni matendo yenu bila ya kujionesha kwa watu wala kutaka sifa au umaarufu, kwani mwenye kufanya amali yoyote ile kwa ajili ya kujipendekeza kwa mwengine asiyekuwa Allaah, basi Allaah Humsukumiza nazo amali zake kwa huyo aliyemfanyia amali hiyo.

 

 

Ogopeni adhabu ya Allaah, kwa sababu Hajakuumbeni kwa upuuzi, na wala Hakuacha chochote kiende ovyo. Keshataja athari zenu na Keshajua siri zenu na kuzihesabu amali zenu na kuziandika ajali zenu. Kwa hivyo dunia isikubabaisheni kwani inawaghururisha watu wake, na ameghurika yule atakayebabaishwa nayo.

 

 

Na jueni ya kuwa Aakhirah ndiyo makazi ya milele [Khotuba ya Sayyidna ‘Aliy bin Abi Twaalib aliposhika madaraka]

 

 

Share