Zingatio: Mitihani Ya Walimwengu Na Ulimwengu

Zingatio: Mitihani Ya Walimwengu na Ulimwengu

 

Na: Naaswir Haamid

 

  

Alhidaaya.com

 

 

Mashaka ya dunia yanatokana katika pembe mbili. Ama yawezekana ikawa ni ya kiumbe ama ni katika Qudra Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Viumbe tunavyokusudia hapa ni wanaadamu na majini, kwani wao ndio waliopewa uwezo wa kutii ama kuasi. Na wapo baadhi ya viumbe wanapokosea dhidi ya viumbe wenzao huwa wepesi wa kulifahamu kosa lao bila ya kuambiwa, na iwapo wameteleza basi wanapofahamishwa ni wepesi wa kuelewa. Lakini wapo baadhi yetu ambao ni wagumu wa kuelewa au bora niseme wakaidi. Hapa Uislamu wetu unatutaka kuwachukulia viumbe wenzetu kutokana na udhaifu wao bila ya kununiana, kukasirikiana, kutusiana na aina nyengine zitakazochupa mipaka.

 

Halikadhalika, kuna mitihani inayotokana na Muumba 'Azza Wa Jalla, Aliyetukuka na Asiye na mpinzani katika mitihani Yake. Huenda Muislamu akapata msiba wa kufukuzwa kazi, kukosa makaazi ya salama kutokana na kimbunga ama matetemeko ya ardhi, maradhi na mengineyo. Hizo ni amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na lililo bora kwa hapa ni kuelewa kwamba kila kitu kishakadiriwa na maisha hayatasimama kwako wala kwa mwengine kutokana na mtihani huo. Bali dunia itaendelea hadi amri Yake Allaah iseme kun fayakun (kuwa na liwe)!

 

Katika hali zote za mitihani, ni kurejea kwa Muumba wa hiyo mitihani yote. Ni kumlilia na kuziomba Rahmah Zake zisizo na mfano. Kwani Yeye Ndiye wa kukisikia kilio chetu na kumtaka muongozo. Kurejea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni kupata utulivu wa nafsi kwani moyo hupata subra ya hali ya juu. Muislamu anatakiwa aamini kwamba baada ya dhiki ni faraja na wala hakuna dhiki baada ya dhiki. Hata kama maisha yote hapa duniani yatakuwa tofauti na viumbe vyengine kwa kukosa afya, makaazi, lishe bora na mengineyo. Lakini yatosha kukumbuka neema ya uhai tu ikawa ndio sababu ya kushukuru na kusubiri juu ya mitihani yote.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatuambia ndani ya Kitabu Chake:

 

 وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ

10. Na kwa Allaah watawakali Waumini. [Al-Mujaadalah: 10]

 

 

Na pia Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

  

وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ 

 

3. Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. [Atw-Twalaaq: 3]

 

Naye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufunza du'aa inayotakiwa kusomwa ili kujikinga na shari ya viumbe: 'Auudhu Bikalimati-LLaahit-Taammaati min Sharri Maa Khalaq' (Najilinda kwa maneno ya Allaah yaliyotimia na shari Alichokiumba). [Imesimuliwa na Khawalat bint Hakiym. Imepokewa na Muslim].

 

Kwa hivyo, kama rafiki zako wamekukimbia, familia kukutenga, rudi kwa Rabb ufanye naye urafiki na Yeye Hamsaliti kiumbe Chake. Mapenzi Yake kwetu ni makubwa na huruma Zake hazina mfano.

 

Share