Ameachika Kisha Mume Kamuingilia Baada Ya Mwezi Bila Ya Kumtamkia, Itakuwa Ni Talaka Rejea?

SWALI

Assalamu 'alaykum warahmatullah wabarakatu. Mwanamke kuachwa na mume wakatengana kwa muda wa mwezi mmoja baadaye mume akaja akakuingilia bila ya kukutamkia je! Atakuwa amekurejea?


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu talaka rejea. Hapa dada yetu hukututajia kamwe hiyo talaka ni ya ngapi. Je, ni talaka ya kwanza, ya pili, au ya tatu? Kawaida mwanamke akipatiwa talaka anafaa akae palepale nyumbani kwa mumewe mpaka amalize eda yake.

 

Kukaa eda pale nyumbani ni kuyarudisha mambo katika hali ya kawaida na pengine kila mmoja aone kuwa amekosa ili hao wawili wapate kurudiana. Ikiwa mume atamwingilia mkewe kabla ya eda kumalizika katika talaka ya kwanza au ya pili, atakuwa mume tayari amemrudia. Lakini ikiwa ni talaka ya tatu hao wanandoa hawawezi kurudiana hivyo itakuwa ni haramu wao kukutana kimwili.

 

Ikiwa amekuingilia baada ya talaka ya kwanza au ya pili basi atakuwa amekurudia, nawe ni mkewe tena. Linalotakiwa ni mfanye bidii msiwe ni wenye kuachana kwani talaka zikifuatana huenda ikawapeleka nyinyi katika hali hamuwezi tena kurudiana (yaani talaka ya tatu) mpaka uolewe na mume mwingine kisha uachwe.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share