Nimeshindwa Kuvumilia Mume Wangu Kuoa Mke Wa Pili, Je Naweza Kudai Talaka?

SWALI:

 

Assalaam alaykum warahmatu llahi taala wabarakaatu. Swali langu ni hili: kama mumeo kaoa na alipokwambia ukakubali na ukastahamili lakini kila ukikaa unajiona huna uwezo wa kustahamili unaumia sana na unaona bora uachike kuliko maumivu unayoyapata na huwezi kusubiri tena, unaweza kudai talaka?

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu uke wenza.

 

Awali ya yote tunakupongeza sana kwa kuweza kuyashinda matamanio yako pamoja na Shaytwaan kwa kuweza kukaa muda wa mwanzo katika uke wenza. Hakika hiyo ndio sifa ya Muislamu mwema na mzuri wa kuweza kutekeleza maagizo ya Allaah Aliyetukuka pamoja na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Hata hivyo, yaonyesha baadaye umeshindwa kuendelea na hilo la kumridhisha Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kukaa kwa wema. Si vizuri Kiislamu kwa mwanamke kuomba talaka kutoka kwa mume wake ambaye hana makosa yake binafsi. Ikiwa mume anakutazama kwa yote na kutimiza haki zako zote basi ni kwa nini uvunje ndoa yako. Kwa hilo, ikiwa mume anakupatia makazi yako, chakula chako na wanao, matibabu na kukugawiya siku yako basi inabidi ushindane na matamanio yako pamoja na vitimbi vya Shaytwaan ili kubakia katika ndoa hiyo. Na ni muhali kwa mume kumuomba mkewe aoe mke wa pili na ikiwa mumeo alikupatia fursa hiyo na wewe ukakubali ni kuwa amekukirimu kwa daraja ya juu kabisa.

 

Kwa hali moja au nyingine ikiwa mume ameegemea upande mmoja kwa kumpendelea mke wa pili (au mdogo) inatakiwa utumie njia za kisheria kuweza kupata haki zako za uke. Ikiwa hupatiwa basi utumie njia za kisheria kuweza kuzidai na ikiwa mume amekaidi utakuwa na haki ya kudai talaka.

 

Na ikienda kuwa unaona huoni raha bila ya makosa yoyote kutoka kwa mumeo unaweza kuomba talaka kwa sharti umrudishie mumeo huyo mahari aliyokupatia. Na hiyo inaitwa Khul’u katika sheria.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi kuhusu mas-ala haya:

 

Kuomba Talaka Bila Sababu

 

Sababu Gani Zinamruhusu Mke Kuomba Talaka?

 

Hata hivyo, nasaha yetu kwako ni ubakie katika ndoa yako, kwani waume hawapatikani kwa rahisi hasa wale ambao ni wema.

 

Tunakutakia kila la kheri katika kubakia katika ndoa hiyo yako. Na Allaah Aliyetukuka Akupatia mafanikio mema.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share