Kuhudhuria Sherehe Za Wanafunzi Zenye Mchanganyiko

SWALI:

Assalam aleikum,

Nimeulizwa kuhuhsu kwenda prom night yafaa? Prom night ni sherehe wanafunzi waenda kusherekea na wanawke kabla ya kuiaga shule kwenda unversity ama college. Naomba uniandikie madhara yake na aya pamoja na hadith.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu hiyo inayoitwa ‘prom night’. Inatakiwa tufahamu kuwa sherehe zozote ambazo tutafanya ni lazima ziende sambamba na mafunzo ya Dini yetu tukufu. Katika yale yaliyokatazwa na Dini ni kuwa na sherehe ya kijahiliya ambazo zinakwenda kinyume na maadili ya Uislamu.

Miongoni mwa yaliyokatazwa ni kuhudhuria michanganyiko baina ya wanaume na wanawake pasi na kuchunga muruwa wa Dini. Katika hali hiyo mwanaume na mwanamke wanakaa na kuzungumza baina yao na hata kuingia katika mengine. Hata ikiwa hawatakaa katika hali hiyo pia itakuwa haifai kwani waliohudhuria watakuwa wameikaribia zinaa iliyokatazwa.

Allaah Aliyetukuka Anasema:

Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya” (17: 32).

 

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akabainisha kuwa macho yanazini, na zinaa yake ni kutazama ya haramu, masikio yanazini, na zinaa yake ni kusikiliza ya haramu. Miguu, mikono na viungo vyengine vyote vinazini kwa njia moja au nyengine kama kwenda katika haramu, kushika vya haramu na mengineo.

Mbali na hilo katika sherehe kama hiyo huwa kuna muziki na ulevi vyote vikiwa ni haramu katika Uislamu. Allaah Anasema yafuatayo kuhusu muziki:

Na wachochee uwawezao katika wao kwa sauti yako, na wakusanyie jeshi lako la wapandao farasi na waendao kwa miguu. Na shirikiana nao katika mali na wana, na waahidi. Na Shetani hawapi ahadi ila ya udanganyifu” (17: 64) na pia,

Na miongoni mwa watu wapo wanaonunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Allaah pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha” (31: 6).

Kuhusu Aayah hii ya pili, Ibn Mas‘uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliapa kwa kusema kuwa makusudio yake ni muziki. Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza suala hilo.

Na ulevi unafahamika umekatazwa sio kunywa tu bali hata kukaa na anayekunywa huku ukisema mimi nakunywa soda au juisi tu.

Kwa ufupi ni kuwa mikusanyiko hiyo ya ‘prom night’ ni haramu katika Uislamu.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share