Kutoa Aibu Ya Mwenzio Ni Ghiyba (Kusengenya)
SWALI:
allah akulipeni kila ya kheri kwa kuanzisha nafasi hii yakuweza kuuliza masuali yetu.
nilikuwa nauliza hili:-
ukiwa watu tumekaa pamoja. na mwezetu miongoni mwa sisi akatoa aibu ya mtu mwengine bila ya kumtaja jina sasa je hii hukumu yake nini? yaani itakuwa ndo tayari ushasengenya au vipi?
JIBU
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Bila shaka kutoa aibu ya mtu mwingine itakuwa ni kujichumia dhambi na vile vile itaanguka katika hukmu ya ghiyba (kusengenya) ambayo mtu huadhibiwa na vile vile ni kupoteza mema yako unayofanya kuwa anapewa huyo unayemsengenya. Mwenye kuzidi kusengenya huendelea kupoteza thawabu zake hadi anapokuwa hana kilichobakia katika mema yake, hapo tena hujazwa madhambi ya wale aliowasengenya.
Tumeonywa
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((وَيْلٌ لِّكُلِّ هُمَزَةٍ لُّمَزَةٍ))
((Ole wake kila safihi, msengenyaji!)) [Al-Humazah: 1]
Ibn 'Abbaas (Radhiya Allahu 'anhu amesema: "Humazah ina maana yule anayetukana na kufedhehesha wenzao" [At-Twabariy 24:596]
Waislamu tunatakiwa tuheshimiane na kusitiriana aibu zetu. Kwani Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
عن ابن عمر رضي اللَّه عنهما أَنَّ رسول اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم قال : (( المُسْلِمُ أَخُو المُسْلِمِ ، لا يظْلِمُه ، ولا يُسْلِمهُ ، منْ كَانَ فِي حَاجَةِ أَخِيهِ كَانَ اللَّهُ فِي حاجتِهِ ، ومَنْ فَرَّج عنْ مُسْلِمٍ كُرْبةً فَرَّجَ اللَّهُ عنْهُ بِهَا كُرْبَةً مِنْ كُرَبِ يوْمَ الْقِيامَةِ ، ومَنْ ستر مُسْلِماً سَتَرهُ اللَّهُ يَوْم الْقِيَامَةِ)) متفقٌ عليه
Kutoka kwa ibn 'Umar (Radhiya Allahu 'anhuma) kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Muislamu ni ndugu wa Muislamu, haimpasi kumdhulumu wala kumsalimisha kwa adui, atakayemsaidia haja ndugu yake Allah Atamkidhia naye haja yake, atakayemuondoshea dhiki Muislamu mwenzake, Allah Atamuondoshea dhiki katika dhiki za Qiyaamah, atakayemsitiri Muislamu (duniani), Allah Atamsitiri siku ya Qiyaamah)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
عن أَبي هريرة رضي اللَّه عنه قال : قال رسول اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم : ((المُسْلِمُ أَخُو الْمُسْلِم لا يخُونُه ولا يكْذِبُهُ ولا يخْذُلُهُ ، كُلُّ الْمُسْلِمِ عَلَى الْمُسْلِمِ حرامٌ عِرْضُهُ ومالُه ودمُهُ التَّقْوَى هَاهُنا ، بِحسْبِ امْرِىءٍ مِنَ الشَّرِّ أَنْ يَحْقِرَ أَخاهُ المسلم)) رواه الترمذيُّ وقال : حديث حسن
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Muislamu ni ndugu wa Muislamu, hamkhini wala hamuongopei, wala hamuudhi. Muislamu kwa Muislamu mwenzake ni haramu (kuvunja) heshima yake, (kula) mali yake, (kumwaga) damu yake. Taqwa iko hapa. Kila mtu inampasa atahadhari na haya kwani inatosheleza pekee kumdhararu nduguye Muislamu kuwa ni kutenda ovu)) [At-Tirmidhiy na kasema ni Hadiyth Hasan]
Bonyeza hapa upate maelezo zaidi yanayohusu uovu wa ghiybah;
Kusengenya (Ghiybah) Japo Anayesengenywa Anayo Sifa Yenyewe Ni Dhambi
Na Allah Anajua zaidi
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


