Ana Tabia Za Za Kutazama Wanawake Na Picha Chafu Anashindwa Kujizuia Nazo- Afanyeje?

 

Ana Tabia Za Kutazama Wanawake Na Picha Chafu

Anashindwa Kujizuia Nazo- Afanyeje?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Nina tabia tatu Nimeshindwa kujizuia. Kuwatazama wanawake kwa matamanio. Kutazama picha zao kwenye t.v. Na kuwachezea. Yaani vitendo kabla ya jimai. Lakini si waingilii. Kila siku namuomba Rabb anitowe katika makosa haya nashukuru amenipa nguvu za kujizuia kuwaingilia lakini hayo matatu nimeshindwa na sababu kubwa ni kuwa yanapatikana kwa urahisi. Nifanye nini.

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Awali ya yote ni kuwa mwanaadamu anaposema juu ya jambo lolote kuwa ameshindwa basi atashindwa kwa kuwa ashajiwekea udhaifu kuwa hawezi. Linalotakiwa ni kuwa na moyo thabiti na bila shaka Allaah Aliyetukuka Atakusaidia. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ ۗ 

Hakika Allaah Habadilishi yale yaliyoko kwa watu mpaka wao wenyewe wabadilishe yale yaliyomo katika nafsi zao.  [Ar-Ra’d: 11].

 

Ikiwa unaweza kuchezecheza na wanawake bila ya kuzini nao ni kuwa wewe una uwezo wa kujizuia na hata hilo la kutazama televisheni na kuchezacheza na wanawake. Hiyo ni ishara tosha, hivyo fanya juhudi na Allaah Aliyetukuka Atakusaidia kwani Yeye Humsaidia mwenye kujisaidia.

 

Kisha linalotakiwa ni uwe mbali na vishawishi vyovyote ambavyo vinaweza kukuweka karibu na zinaa. Allaah Aliyetukuka Ametumia neno kali lenye uzito wa kumfanya mtu ajiepushe na uzinzi huo pale Aliposema:

وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا ﴿٣٢﴾

Na wala msiikaribie zinaa. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya kabisa. [Al-Israa: 32].

 

Na kila wakati unapotaka kufanya kosa usitazame kosa lakini angalia unayemkosea. Wewe unamkosea Allaah Aliyetukuka, je, utamjibu nini utakaposimama mbele Yake Siku ya Qiyaamah siku ambayo hakutakuwa na mkalimani baina yako na Allaah Aliyetukuka.

 

Pia inaonyesha una wakati mwingi wa kupoteza, jaribu sana kujishughulisha na mambo ambayo yatakusahilishia kujiepusha na maovu hayo. Badala ya kuwa unapoteza wakati kwa kukaa na kutazama picha mbaya katika televisheni, nunua filamu za Kiislamu ambazo zitakufundisha kuhusu Dini yako na za mawaidha ambazo zitakuwa zinakukumbusha kuhusiana na wajibu wako juu ya hilo.

 

Chukua wakati mwingi katika kusoma Qur-aan, jua maana yake, zingatia yaliyo ndani, fanya juhudi kuyatekeleza hayo. Bila shaka ukifanya hayo utajikuta unakuwa karibu na Allaah Aliyetukuka na hivyo kujiepusha na mengi maovu.

 

Jikurubishe katika kufanya ‘Ibaadah na huku unamuomba Allaah Aliyetukuka kwa dhati Akuepushie matatizo hayo ya kujiingiza katika madhambi hayo makubwa. Na pia ulimi wako uwe na rutuba ya kumtaja Allaah Aliyetukuka kila wakati. 

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo na manufaa zaidi:

 

Anapenda Kuangalia Machafu Kisha Anatubu, Kisha Anarudia Tena, Naye Anachukiwa Jambo Hili

 

Nataka Kutubu Lakini Shaytwaan Kanivaa Nifanye Nini?

 

Kijana Anaishi Nchi Zenye Maasi Mengi, Anajaribu Kujizuia Anaomba Toba Kila Mara Anasumbuliwa Na Khofu Aliyonayo

 

Anajaribu Kufanya Mema Lakini Ana Tabia Chafu Ya Kuondosha Matamanio Kwa Mkono Na Vifaa, Afanyeje Kujiepusha Shaytwaan ?

 

 

Tunakuombea tawfiki katika kufanikisha kujiondoa katika hayo madhambi.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share