Utulivu Wa Nafsi (Sakiynatun-Nafs) - 1

 

Utulivu Wa Nafsi (Sakiynatun-Nafs) - 1

 

Imekusanywa na Ukht Haliymah ‘Abdullaah

 

 Alhidaaya.com

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 هُوَ الَّذِي أَنزَلَ السَّكِينَةَ فِي قُلُوبِ الْمُؤْمِنِينَ لِيَزْدَادُوا إِيمَانًا مَّعَ إِيمَانِهِمْ ۗ

Yeye Ndiye Aliyeteremsha utulivu katika nyoyo za Waumini ili Awazidishie iymaan pamoja na iymaan zao.  [Al-Fat-h: 4]

 

 

Anasema mmoja wa daktari mashuhuri Marekani, “Nilipokuwa kijana niliweka ratiba ya vitu vizuri vinavyokubalika katika maisha, nikaandika hali nimejawa na matamanio ya kidunia, navyo ni: afya, mapenzi, ujuzi (kipaji), nguvu, utajiri, umashuhuri. Nikampelekea mzee mwenye hekima.

 

Akaniambia huyo mzee, ratiba nzuri imepangika vilivyo lakini inaonesha umesahau kipengele muhimu akapiga mstari katika ratiba yote na kuandika maneno mawili ‘Utulivu wa Nafsi’.

 

Akasema hii ni zawadi ambayo Anamhifadhia Allaah Aliyemchagua (katika waja wake) Anawapa wengi akili na afya, mali, ama utulivu wa nafsi, Anatoa kwa kukadiria.

 

Akasema: Haya nisemayo si mawazo yangu ila nimenakili kutoka kwa wenye hekima wanasema: (Ee Mola acha neema ya dunia chini ya miguu ya wajinga, na unipe moyo usiotetereka (usiotatizika).

 

Niliona tabu wakati huo kukubali hayo, lakini sasa baada ya nusu karne nimekiri katika majaribio niliyopitia na mazingatio niliyopata, nimejua utulivu wa nafsi ndio lengo la mwongozo wa maisha yenye kupigiwa mfano, na mimi nimejua sasa jumla ya mambo mengine sio lazima yampatie mtu utulivu, nimeona utulivu huu unachanua bila usaidizi wa mali, wala afya. Katika nguvu za utulivu inabadilisha banda kuwa kasri, ama kunyimwa utulivu inabadilisha kasri la mfalme kuwa kiota.”

 

Haya ni maneno ya mtu anayeishi Marekani nchi ya starehe na utajiri, nchi ya uhuru kufanya utakacho. Anayasema haya baada kupitia maisha, hakupata katika maisha neema bora na ghali kama utulivu wa nafsi.

 

 

Hakuna Utulivu Bila Ya Iymaan

 

 

Utulivu wa nafsi ndio chimbuko la furaha (sa’aadah), vipi itafikiwa ikiwa haitokani na akili wala elimu, afya, nguvu, mali, utajiri, umashuhuri, wala neema nyingine ya kimaisha.

 

Jibu lenye matumaini ni Kumuamini Allaah na siku ya mwisho.

 

Imetufundisha maisha kwamba watu wengi wenye wasiwasi, kukosa msimamo, hisia za upungufu na kupotea ni walionyimwa neema ya imani na yakini.

 

Utulivu huu ni matunda ya daraja za Imani na Tawhiyd.

 

Anashusha Allaah (Subhaanah wa Ta’aalaa) katika mioyo ya Waumini waliopo duniani wawe na msimamo watakapopata matatizo watu, waridhike watakapokasirika watu, wawe na yakini watakapotilia shaka watu, wasubiri watakapotetereka watu, wawe wapole watakapokuwa wajinga.

 

 Utulivu huu ndio uliojaa moyo wa Nabiy (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) siku aliyohama. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 

إِلَّا تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّـهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا ۖ فَأَنزَلَ اللَّـهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ لَّمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُوا السُّفْلَىٰ ۗ وَكَلِمَةُ اللَّـهِ هِيَ الْعُلْيَا ۗ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٤٠﴾

Msipomnusuru (Rasuli), basi Allaah Amekwishamnusuru, pale walipomtoa (Makkah) wale waliokufuru akiwa wa pili katika wawili; walipokuwa katika pango, alipomwambia swahibu yake: Usihuzunike, hakika Allaah Yu Pamoja nasi. Basi Allaah Akamteremshia utulivu Wake, na Akamsaidia kwa majeshi msiyoyaona, na Akajaalia neno la waliokufuru kuwa chini. Na Neno la Allaah kuwa ndilo lililo juu. Na Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [At-Tawbah: 40]

 

 

Ulimpata uoga Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) juu ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na uendelevu wa Da’awah na kusema, “Ee Rasuli wa Allaah, lau mmoja wao akitizama chini atatuona.” Akasema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): “Je, unafikiria nini wawili watatu wao ni Allaah?.”

  

 

Sababu Za Utulivu Kwa Muumin

 

 

1. Muumin Kuutikia Wito Kimaumbile

 

 

Mwanzo wa sababu ya utulivu kwa Muumin ni kwamba ameongozwa katika umbile Alilomuumba nalo Allaah, linaloshikamana na kuwepo kwake na kumuwezesha kuishi kwa amani na upendo sio ugomvi na vita.

 

Anasema Ibnul Qayyim (Rahimahu-Allaah) katika kitabu chake Madaarij As-Saalikiyn:

“Katika moyo kuna mtawanyiko (sha’itha) huwezi kukusanya ila kuelekea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Na kuna ubaya hauondoki ila kujibembeleza kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Na kuna huzuni haiondoki ila kufurahika kwa kumjua (Allaah), kuwa mkweli katika matendo.

 Na kuna wasiwasi hautotulia ila kwa kukutana Naye na Kuwa kimbilio lako.

 

Na kuna moto wa majuto hauzimiki ila kwa kuridhia Amri Yake, makatazo, na Qadhwaa Yake, na kuikumbatia subra juu ya hilo mpaka utakapokutana Naye.

 

Na kuna uwazi hauzibiki ila kwa kumpenda, kurejea Kwake na kumtaja daima, ukweli wa kumtakasa. Lau mtu atapewa dunia na vilivyomo hautoziba huo uwazi.”

 

Hilo ndilo umbile la mwanaadamu la asili hapati utulivu ila kwa kumfuata Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), kumuamini na kumuelekea.

Ni umbile (fitwrah) walilokiri washirikina enzi za ujahiliya. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ ۖ فَأَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ ﴿٦١﴾

  Na ukiwauliza: Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi, na akatiisha jua na mwezi? Bila shaka watasema: Allaah. Basi vipi wanavyoghilibiwa? [Al-‘Ankabuwt: 61]

 

 

 

Akipatwa mwanaadamu na shida mara anamkimbilia Allaah kisha akiondoshewa matatizo anamsahau kama vile hakumuomba.

 

Kwa ajili ya kupata utulivu huu ikawa kazi ya Manabii kuamrisha ‘Ibaada ya Allaah na kujiepusha na twaaghut.

  

 

 

2.    Muumin Kuongoka Kutokana Na Siri Ya Kuwepo Duniani

 

 

 Ndani ya kila mwanaadamu kuna sauti iliyojificha inamuita, na maswali yanayompitia kutaka jawabu litakalomuondoshea hofu na kumtuliza nafsi, ni nini ulimwengu? Nani mwanaadamu, amekuja kutoka wapi? Nani kamtengeneza? Nani anamsimamia mambo yake? Nini lengo lake? Vipi ameanza na ataishia vipi? Ni nini maisha na mauti? Ni nini kinamsubiri baada ya maisha haya? Je, inapatikana kitu baada ya maisha haya? Na ni nini uhusiano wake na kudumu (al-khuluwd)?

 

Maswali haya yaliyomsumbua mwanadamu tangu kuumbwa kwake mpaka yatakapomalizika maisha hayakupata na hayatopata majibu yanayotosheleza ila katika Dini.

 

Uislam ndio Dini bora inayotupa majibu.

 

Qur-aan imeeleza kwamba hii Dini ni ya kimaumbile, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا ۚ فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا ۚ لَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٠﴾

Basi elekeza uso wako kwenye Dini yenye kujiengua na upotofu inayoelemea haki. Umbile la asili la kumpwekesha Allaah Aliyowaumbia watu. Hakuna mabadiliko katika uumbaji wa Allaah. Hiyo ndio Dini iliyonyooka sawasawa, lakini watu wengi hawajui. [Ar-Ruwm: 30]

 

 

 

Share