Mume Wangu Anataka Kumuoa Mwanamke Amependana Naye Katika Internet Nami Siko Radhi

 

SWALI:

 

A.A

 

Ndugu zangu masheikh na mau'lamaa.

 

 

Mimi nimeolewa na watoto sasa mume wangu asema apenda mwanamke amejuana kwa internet sasa mimi sikubali na hata akitaka kumuoa mimi siko radhi maana Allaah ajua mimi hadi sasa sijampunguzia chochote.  Nifanyeje?

 


 

JIBU:

 

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.]

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu uke wenza. Wanawake hata wakiwa wacha Mungu namna gani wanashindwa kukubali rukhsa moja iliyotolewa na Allaah Aliyetukuka, nayo ni mume kuoa au anataka kuoa mke wa pili. Allaah Aliyetukuka kwa hekima Yake ametoa ruhusa hii pale Aliposema:

 

"Basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili, au watatu wa wane. Na mkiogopa kuwa hamuwezi kuafanya uadilifu, basi oeni mmoja tu" (4: 3).

 

Kitu ambacho ni muhimu kwako kumsaidia mumeo aweze kufanya uchaguzi wa busara kwa kuchagua mwanamke mwenye Dini na maadili ya Kiislamu. Usiwe ndio sababu kwa mumeo kuharibu uhusiano na wewe au kumpelekea kufanya zinaa kwa ajili ya wewe kuifanya hali yake kuwa ngumu katika suala hilo.

 

 

Hakika ambayo wanawake wengi wanaikosa au hawaijui ni kuwa mume hahitaji kisheria kupata idhini ya mkewe anapotaka kuoa mke wa pili au watatu au wane. Wala kutokuwa radhi wewe katika hilo halimpingi yeye kisheria kuoa. Pia kutokuwa na radhi kwako hakiteremshi cheo chake kwa Muumba wake akiwa atakuwa Muumini wa kweli, na mwenye kutenda mema na mwenye Imani thabiti.

Hivyo, shauri letu kwako ni kuwa uwe ni mwenye kumsaidia mumeo aweze kutimiza haki zako na za mke mpya na wala usiwe ndio sababu ya uhasama na kutolewa talaka.

 

Nawe utakaposubiri na ukakubali sheria za dini yako ambayo imemruhusu mume kuoa mke zaidi ya mmoja utapata faida zifuatazo:

 

1.     Utakuwa sababu ya kumzuia mume wako kutokufanya zinaa hivyo utapata thawabu.

2.     Mume wako atazidi kukupenda na kukuthamini, kinyume na utakapomfanyia matatizo huenda akachukiwa na wewe hata mwishowe apoteze mapenzi yake yote kwako ya awali.

3.     Utakuwa miongoni mwa Waumini khaswa wanaopokea na kukubali sheria za dini yao kwa kuwa na yakini moyoni kwamba kila jambo ni majaaliwa kutoka kwa Mola Mtukufu, na hivyo lina kheri na wewe na sio shari.

4.     Utapata thawabu za kuwa subra kwa jambo zito kama hili kwa wanawake wengi kabisa, na malipo ya subira kwa Mola ni mengi mno hadi kupandishwa daraja Peponi..

5.     Utakuwa ni mfano kwa wanawake wengine kukubali mume wako aoe, hivyo kila atakayefuata mfano wako, nawe utapata thawabu kwa kusababisha kufanya hukumu za dini yetu kuwa wepesi na kukubalika kwa wengineo.

 

 

Hatuna shaka kwamba ni jambo gumu lakini tunakuomba uvumilie na umuombe Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akufanyie wepesi na sisi pia tunakuombea Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akupe subra na Akuzidishie Iymaan ya dini Yake tukufu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share