Nani Waliomilikiwa Mikono Ya Kuume? Lawama Zipi? Sababu Ya Kuteremka Aayah Yake

SWALI

 

 

ALLAH (swt) awajaze kheri wote wanaoshughulika na Mtandao wa AL~HIDAAYA. ALLAH (SWT) katika Quran 23:6 anasema "Isipokuwa kwa wake zao au kwa (Wanawake) wale waliyowamiliki kwa mikono yao ya kuume (kulia).Basi hao ndiyo wasiolaumiwa"

 

 


1. Je, Wanawake waliomilikiwa kwa mikono ya kuume wepi?

2. Ni lawama zipi alizo sema ALLAH?

3. Kwa nini HAYA hii ilishuka?

 

 

Jazza Allahu~Khaira.

 


 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako   kuhusu Aayah uliyoitaja hapo juu. Ama suala la kwanza la wanawake inayomiliki mikono yenu ya kuume ni   wale watumwa wa kike walioshikwa na Waislamu katika vita vya Jihaad

 

Ama kuhusu lawama ambazo Muislamu anaweza kupata ni kutumia njia nyinginezo mbali na ile ya kufanya mapenzi na mkeo wa halali na iliyomiliki mikono yako ya kuume. Kwa mfano ni kuzini, kufanya kitendo cha kaumu Luutw, kusagana, kumuingilia mkeo kwa nyuma na kadhalika. Hivi ni vitendo lau mtu atafanya basi atakuwa ni mwenye kupata madhambi na kulaumiwa.

 

Ama swali lako la tatu ni kuwa amesema ‘Abdur-Rahman ‘Abdul-Qaari’: Nimemsikia ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) akisema: Ilikuwa pindi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoteremshiwa wahyi inasikika usoni mwake mlio kama wa nyuki. Baada ya hapo tukakaa kwa saa, naye akaelekea Qiblah, akanyanyua mikono yake, akasema: “Ewe Mola wetu! Tuzidishie wala usitupunguzie, tukirimu wala usitudhalilishe, tupe wala usitunyime, tupendelee wala usituathiri na turidhie”. Kisha akasema: “Hakika tumeteremshiwa Aayah kumi, yeyote atakayezitekeleza basi ataingia Peponi”. Kisha akasoma: “HAKIKA wamefanikiwa Waumini”, hadi Aayah ya kumi (al-Haakim Abu ‘Abdillaah katika Swahiyh yake).

 

 

Aayah hiyo ni Aayah Namba 6 katika hizo kumi.

 

 

Maelezo zaidi yamo katika viungo vifuatavyo:

 

 

Waliomiliki Mikono Yao Ya Kiume Ina Maana Inafaa Kufanya Mapenzi Na Wafanya Kazi Wa Nyumbani?

 

House Girl Sio Wale Waliomiliki Mikono Yetu Ya Kuume

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share